2016-07-09 07:33:00

Utume wa bahari na changamoto zake!


Mama Kanisa  Jumapili tarehe 10 Julai 2016 anaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Utume wa Bahari. Changamoto na mwaliko wa kwa Jumuiya za Kikristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwatambua na kuwathamini Mabaharia wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, lakini wanachangia kwa hali na mali katika ukuaji wa uchumi kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni siku ya kumshukuru Mungu kwa sadaka na majitoleo yanayooneshwa na Mabaharia sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu kunako mwaka 1975, Mama Kanisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao kwa kuwashukuru kwa mchango wao katika ustawi na maendeleo ya endelevu ya binadamu. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene kwa kuwashirikisha pia waamini wa Makanisa mengine katika sala na tafakari mintarafu mchango wa mabaharia na wavuvi. Lengo ni kuendelea kujenga na kuimarisha uekumene wa sala na huduma, ili kwa pamoja Makanisa yaweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za mabaharia pamoja na wavuvi ambao wanakabiliana na changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa shukrani kwa mchango unaotolewa na mabaharia duniani katika kukuza uchumi wa dunia. Lakini hawa ni watu wanaokabiliwa na hatari nyingi katika maisha na utume wao, wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, mambo ambayo wakati mwingine yanachangia pia athari katika maisha ya kifamilia.

Utu na heshima yao kama binadamu mara nyingi ni mambo yanayowekwa rehani kiasi hata cha kutuhumiwa kwa makosa mbali mbali ya jinai. Baraza la Kipapa linayashauri Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Duniani kuhakikisha kwamba, yanaanzisha utume wa bahari kwa mabaharia kutoka katika nchi zao ili waweze hata wao kupata huduma za kichungaji zinazotolewa na Mama Kanisa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika maadhimisho haya linasikitika kusema, bahari ambayo ni rasilimali kubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu inaendelea kukabiliwa na uchafuzi na uvunaji mkubwa wa rasilimali inayopatikana kutoka baharini hali ambayo inasababishwa na ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na kusahau kwamba, hii ni nyumba ya wote inapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kudumishwa kwa ajili ya ustawi na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kusali na kuwambea mabaharia na wavuvi katika maisha na utume wao, ili waweze kutambua kwamba, hata wao wanapendwa na Baba mwenye huruma licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao wanapokuwa baharini. Matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo mabaharia pengine hazipewi uzito wa pekee katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, lakini matukio ya kigaidi na ajali zinapotokea kwenye uso wa dunia, vyombo vya habari viko makini na haraka kutoa habari za matukio haya.

Uchafuzi wa mazingira uliojitokeza nchini Japan baada ya kuvuja kwa mtambo wa Fukushima, mabaharia walikuwa ni watu wa kwanza kujitokeza kutoa huduma ya kwanza kwa waathirika bila ya kuwa na taarifa kwamba, walikuwa wanakabiliwa na kifo machoni pao. Kutokana na mazingira na hali kama hii zaidi ya watu 2000 waliathirika kutokana na mionzi ya nyuklikia kutoka kwenye mtambo wa Fukushima. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linakumbusha kwamba, kunako mwaka 1954 wavuvi waliokuwa wanavua kwenye Visiwa wa Marshall, walilipuliwa na bomu la nyuklia na mabaharia 23 wakaathirika kutokana mionzi ya nyuklia.

Mabaharia na wavuvi licha ya kukabiliwa na majanga asilia, lakini leo hii bahari imegeuka kuwa ni uwanja wa mazoezi ya majaribio ya silaha za kinyuklia pamoja na shimo la takataka zenye sumu ambazo zina madhara makubwa kwa maisha ya binadamu pamoja na viumbe hai wanaoishi baharini. Haya ni matukio ambayo yamefichama sana kiasi kwamba, si rahisi sana kwa vyombo vya habari kuyatolea taarifa makini. Vitendo hivi vya binadamu visivyozingatia Injili ya uhai vinakumbatia kwa kiasi kikubwa utamaduni wa kifo, usiojali wala kuthamini utu na heshima ya binadamu wala mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, bahari ni kielelezo kikubwa cha sanaa ya uumbaji iliyofanywa na Mwenyezi Mungu na kumkabidhi binadamu aweze kuitunza na kuiendeleza, lakini leo hii, binadamu amekuwa ni mharibifu wa zawadi hii kubwa kutoka kwa Mungu kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Binadamu wengi wanapata riziki yao ya kila siku kutoka baharini na kwamba, binadamu wote wamepanda Meli ya bahari, kumbe wanapaswa kuwakumbuka na kuwaombea manahodha wao, ili watu wote waweze kufika salama bandarini na kutua nanga ya imani, matumaini na upendo anasema Askofu Michael Goro Matsuura, Mwenyekiti wa Tume ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.