2016-07-08 14:52:00

Chuchumilieni utakatifu wa maisha kwa njia ya wito wa Upadre


Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa Mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati, hivyo hii ni Sakramenti ya huduma ambayo ina ngazi kuu tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Kwa nguvu ya Sakramenti ya Daraja, Mapadre hushiriki utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; hawa ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu katika kuadhimisha na kugawa Mafumbo ya Kanisa kwa familia ya Mungu na kwamba, wanaungana kati yao kwa udugu wa kisakramenti na kuunda mwili mmoja katika Jimbo husika.

Sakramenti ya Daraja  huwawezesha Mapadre kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza waamini wao kwa niaba ya Askofu Mahalia. Daraja takatifu ni zawadi ya huruma ya Mungu kwa waja wake, kumbe Mapadre wanaitwa na kutumwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma!

Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Alhamisi, tarehe 7 Julai 2016 kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay, Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa Daraja la Upadre kwa Mashemasi watatu kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kuwataka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia una changamoto na matatizo yake, kumbe familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam inapaswa kuendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea Mapadre ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari na moyo mkuu.

Askofu Nzigilwa anasema, Samaki akiwa majini ni salama, lakini anapotolewa nje ya maji, maisha yake yanakuwa hatarini sana. Kutokana na mantiki hii hata binadamu anahitaji kwa namna ya pekee huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake ili aweze kusonga mbele kwa imani na matumaini. Mapadre wasaidie juhudi za kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na mmong’onyoko wa kimaadili kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili waweze kutubu na kumrudia tena Mwenyezi Mungu anayewataka kuambata njia ya ukamilifu na utakatifu wa maisha! Ni wajibu wa Wakleri kuisaidia familia ya Mungu ili kuweza kuboresha maisha yake: kiroho na kimwili.

Mapadre wajifunge mikanda barabara ili kutoa huduma makini kwa familia ya Mungu, kwa kuwasadikisha waamini kwamba wako kwenye mikono salama kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mapadre waoneshe ujasiri wa kuwakwamua waamini waliomezwa na malimwengu na Ibilisi kwa njia ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa, hususan Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Kitubio, ili kuwapatia nguvu na kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kipimo!

Mapadre watambue kwamba, wao ni wahudumu wakuu wa Neno la Mungu, kumbe wanawajibika kulitafakari, kulitangaza na kulishuhudia katika maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji. Anasema, watu wanavutwa zaidi kwa mifano bora ya maisha ya Kikristo na shuhuda za Kiinjili kuliko maneno matupu ambayo kimsingi hayaachi kutika!

Daima Neno la Mungu litaendelea kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu, changamoto pia kwa waamini kulifahamu na kulishuhudia Neno, ambalo linapaswa kuwa ni chachu ya mapambano dhidi ya Ibilisi duniani Neno la Mungu lisaidie kujenga na kuimarisha umoja, udugu, upendo na mshikamano wa familia ya Mungu kuanzia kwenye familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Kigango, Parokia, Jimbo na Taifa katika ujumla wake. Hapa ni mahali muafaka pa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Mapadre wawasaidie waamini kupata Sakramenti za Kanisa na huduma za maisha ya kiroho.

Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa amewataka Mapadre wapya kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kutumia vyema karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma. Mapadre wapya Jimbo kuu la Dar es Salaam ni William Singano, James Ngonyani na Francisko Jose. Ibada hii imehudhuriwa na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali.

Wakati huo huo, Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki la Moshi, ametoa Daraja takatifu kwa Mashemasi 20 kwa mpigo! Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu Gabriel Gabuza kutoka Afrika ya Kusini aliyekuja kushuhudia ukuu wa Mungu unaojionesha katika zawadi ya maisha na wito wa Kipadre, kwa vijana kuamua kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao!

Na Rodrck Minja,

Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.