2016-07-07 08:23:00

Utume wa maskini ndani ya Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa, maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutoka Jimbo kuu la Lyon, Ufaransa amekaza kusema, hata maskini katika umaskini wao, wamekabidhiwa dhamana ya kuwa ni vyombo vya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, kwa njia ya sala na majitoleo yao ya kila siku, ili kuenzi maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Zaidi ya mahujaji elfu mbili kutoka Jimbo kuu la Lyon, Jumatano 6 Julai 2016 wamejisikia nyumbani na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzungumza na kuomba kupiga picha za kumbukumbu pamoja na kucheza rumba, kielelezo cha furaha inayobubujika kutoka katika maisha ya watu wa kawaida, watu wasiokuwa na makuu! Ni watu ambao wamemshirikisha Baba Mtakatifu misalaba ya maisha yao kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, makazi bora wala hata senti ya kuweza kujinunulia kiatu mguuni.

Kuna watu ambao wameteseka tangu utotoni kwa kukosa tunza na hifadhi kutoka kwa wazazi na walezi wao kutokana na sababu mbali mbali. Katika kundi hili walikuwepo wale watu ambao wamejikuta wanatumbukia katika umaskini wa kimaadili na kihali kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ulevi wa kupindukia; mambo ambayo yamedhalilisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wote hawa wamebahatika kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kanisa kutokana na juhudi za Padre Joseph Wresinki (1917 – 1988) aliyeanzisha chama cha kitume kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia maskini pamoja na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Padre Wresinki katika maisha yake alionja umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu; akabahatika kupata zawadi ya wito na maisha ya Kipadre, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika safari ya maisha yao hapa duniani!

Padre Wresinki akajifunga kibwebwe ili kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, leo hii kuna mshikamano wa vyama na mashirika ya kitume nchini Ufaransa yanayojikita katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka kwa Kanisa kujitaidi kumwilisha tena na tena matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha maskini kwamba wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Kashfa ya umaskini wa hali na kipato ina madhara makubwa kwa watu, lakini zaidi kwa maisha na utume wa familia, kiasi hata wakati mwingine, watoto kutenganishwa na wazazi pamoja na walezi wao kutokana na umaskini. Kuna mambo mbali mbali ambayo yanapelekea watu kutumbukia katika umaskini, kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha moyo wa toba na wongofu wa ndani; huruma na msamaha.

Waamini wawe na ujasiri wa kuwatafuta maskini kwani daima wanajificha na wala hawataki kujionesha, kwani Kanisa linapaswa kuwa maskini kwa ajili ya huduma makini kwa maskini, wanaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Maskini nao wana kiu na njaa ya Neno la Mungu na kwamba, hata maskini katika umaskini wao bado wanaweza kuchangia katika ustawi, maisha na utume wa Kanisa kwani hakuna maskini asiyekuwa na chochote cha kuweza kuchangia! Uwepo wao ni alama tosha kabisa ya ushuhuda na huruma ya Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha umoja, udugu na upendo; toba, msamaha, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mahujaji kutoka Ufaransa wanamshukuru Mungu kwa maisha na utume wa Papa Francisko kwani kwa sasa wanatambua kwamba, hata wao wanayo nafasi na upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lyon, Ufaransa amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusema kwamba, lengo la hija hii maalum wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kuwawezesha maskini kuonja huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo aliyekuwa fukara, mtii na mseja ili kuwatangazia watu wa mataifa huruma na upendo wa Mungu. Mahujaji hawa wamemzawadia Baba Mtakatifu Francisko kitabu cha maskini, kilichopambwa na shuhuda mbali mbali mintarafu Habari Njema ya Wokovu. Waamini wanahamasishwa kuwasaidia na kuwahudumia maskini wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku na wala hawa si watu ambao wako mbali sana bali wako kati yao, jambo la msingi ni kufungua akili na nyoyo zao kwa ajili ya kuona maajabu na ukuu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.