2016-07-07 08:44:00

Kanisa lina matumaini katika maisha na utume wa familia!


Kardinali Christoph Schonborn, aliyemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika Jubilei ya miaka 25 tangu Jimbo kuu la Minsk- Mohilev huko Bielorussia lilipoanzishwa katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa uhuru wa kuabudu kama nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya kijamii: kiroho na kimwili. Kardinali Schonborn akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Budslav amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga matumaini yao katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama mhimili mkuu wa maendeleo ya binadamu.

Kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa mabavu nchini Bielorussia na kama hali inavyojionesha kwa sasa, bado familia inakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto zinazokumbatia utamaduni wa kifo na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mambo ambayo ni hatari kwa maisha na utume wa familia duniani! Kanisa lina amini na kutumaini nguvu ya familia kama nyenzo muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko kwa familia kuhakikisha kwamba, zinamwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu.

Kardinali Schonborn akiwa nchini Bilorussia amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa kwa kukazia umuhimu wa uhuru wa kuabudu sanjari na mahusiano bora kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya huduma makini ya familia ya Mungu nchini Bielorussia. Viongozi wa serikali wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba wanakuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na mahusiano bora kati ya Serikali na Kanisa.

Viongozi wa Serikali ya Bielorussia wamemhakikishia Kardinali Schonborn kwamba, Serikali itaendelea kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu pamoja na uhusiano mwema na Kanisa Katoliki. Ukomunisti ulileta athari kubwa kwa maisha ya wananchi wengi nchini Bielorussia, lakini waamini walisimama kidete kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, heri taifa ambalo lina imani thabiti anasema Kardinali Christoph Schonborn, aliyemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Minsk-Mohilev, huko Bielorussia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.