2016-07-07 06:52:00

Faraja ya Papa Francisko kwa wazazi wa Beau Solomon


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 6 Julai 2016 kabla ya kukutana na kuzungumza na mahujaji wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutoka Jimbo kuu la Lyon, Ufaransa, ambao amewasihi kuwaombea matajiri wenye moyo mgumu kama jiwe wasiokuwa na huruma waweze kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuwaonesha maskini huruma na upendo, amekutana na wazazi wa Marehemu Beau Solomon, kutoka Marekani aliyekutwa amekufa maji kwenye mto Tevere mjini Roma katika mazingira ya kutatanisha.

Baba Mtakatifu amewapatia pole na faraja kwa kuondokewa na kijana wao mwenye umri wa miaka kumi na tisa aliyekuwa amefika mjini Roma kwa ajili ya masomo ya kipindi cha kiangazi kwenye Chuo kikuu cha John Cabot, kilichopo hapa mjini Roma. Bwana na Bibi Nick na Jodi wamefarijika sana na maneno ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewapatia Rozari takatifu, ili Bikira Maria, faraja na matumaini ya waamini aendelee kuwasindikiza katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko ameahidi kuendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake, ili waweze kuupokea msiba huu mzito kwa imani na matumaini ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.