2016-07-06 13:37:00

Watoana nyongo kwa ajili ya kugombania mirathi!


Kuna kiongozi mmoja wa nchi alitangaza kuwa serikali yake haina ubaguzi wa dini, wa kabila, wa rangi wala wa vyama vya siasa. Serikali hiyo ilijikita katika kuwatumikia watu wote na kuwainua wanyonge. Wataalamu na wanazuoni mbalimbali wakalifuatilia tamko hilo kwa kufanya majadiliano ya kitaalamu na wananchi wakakaa mkao wa kusubiri hatima ya tamko la kiongozi wao ili kuona kama kweli lina lipa au kama kawaida ni mbwembwe za wanasiasa!

Leo tunakaribishwa katika jukwaa la majadiliano ya maswali na majibu kati ya Mwanasheria mmoja aliyebobea katika sheria za nchi na kidini, na Jalimu, Gwiji, mtaalamu wa hali ya juu wa mambo mengi ambaye leo hii watoto wa mjini wanaimtwa “Mr. Google”. Kwa hiyo, huo ni mjadala wa kitaalamu wa kuwanufaisha wasikilizaji. Mada nyeti ya majadiliano inahusu mirathi. Hebu nasi tuwasikilize na tuone hatima yake.

Anayetuingiza katika mjadala huo ni mwanasheria: “Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu” Neno lililotumika hapa la kujaribu, ambalo kwa kiingereza ni to tempt au, to test, kwa kigiriki limeandikwa ekpeirazōn na tafsiri yake ni kupotosha, kuchepusha au kupindisha ukweli na kuuelekeza kwenye maana unayoijua na kuitaka wewe. Mwanasheria huyu anafahamu fika kwamba Yesu anayajua Maandiko, lakini anataka kumwelewesha kadiri anavyotaka yeye na utamaduni wake.

Hapo ndipo unaposhuhudia majibizano ya moto. Kuna jumla ya maswali matano wanayojibizana. Mwanasheria anatupiwa maswali matatu, na Yesu anarushiwa maswali mawili. Mwanasheria anazingatia itifaki na kukiri cheo cha Yesu cha mwalimu hivi kabla ya kumrushia swali la kwanza anataja sifa yake: “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Neno hili kurithi limechaguliwa kwa umakini mkubwa sana kabla ya kulitumia. Kuna mirathi ya mali ya hapa duniani hasahasa urithi wa maisha au uhai wa kibaolojia tunaopokea kama zawadi ya Mungu kwa njia ya wazazi waliotuzaa na kutuelea, kwani haitoshi tu kuzaa!

Lakini mwanasheria huyu hazungumzii urithi huo, bali anasema kurithi maisha ya milele kwa Kigiriki zoe aionios. Yaani anawania maisha ya milele anayotegemea kuyarithi au kuyapata kama zawadi.  Sisi tungepata fursa ya kukutana na Yesu nadhani tungeomba kuwa  na mafanikio ya maisha ya hapa duniani kwa kuwa na “Vijisenti” na afya bora. Lakini mwanasheria huyu anawania mirathi ya maisha ya milele. Mwalimu anamjibu kwa kumwuliza maswali mawili mfululizo kusudi ajipatie jibu mwenyewe. Hizo ndizo mbinu nzuri za mwalimu bora katika kuelimisha. Swali la kwanza: Imeandikwa nini katika Torati?

Kwa swali hili Yesu anamtaka mwanasheria apate jibu alilogundua mwenyewe kutoka kwenye Torati kwani siri ya sanda anaitambua maiti!. Kisha anamwongezea swali la pili: “Wasomaje?” Hapa sasa anataka kujua mwanasheria ameifanyia utafsiri au “exejesis” gani hiyo Torati, yaani ameielewaje yeye. Mwanasheria alikuwa makini, hayumbishwi na maswali hayo, na anayapangua yote kwa mpigo akinukuu vitabu viwili kutoka Maandiko matakatifu: Kumbukumbu la Torati linasema:“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.” Halafu kitabu cha Mambo ya Walawi palipoandikwa “na jirani yako kama nafsi yako.” Hizi ndizo fasuli zilizo msingi wa Torati nzima. 

Mwalimu akazima “fegi” na akamvulia kofia na kumwambia: “Umejibu vyema,” akimaanisha kwamba mwanasheria huyu alifahamu maisha maana yake ni kupenda kwa moyo wote. Aidha kupenda huko yabidi kumwelekee zaidi Mungu. Mwanasheria anaendelea kuuliza swali la pili: “Na jirani yangu ni nani?” Swali hili ni zito na limefumbika kidogo, yaani nani ni jirani wa kutendewa jema na nani anayetakiwa kutenda jema hilo.

Mwanasheria huyu pamoja na Marabi wote walishajua ni nani hasa wa kumtendea mema kadiri ya Maandiko Matakatifu. Watu wa kutendewa mema nao ni wapita njia, na wale wenye hati rasmi ya kukaa nchini mwao, kama alivyoainisha Mungu mwenyewe ilivyoandikwa: “usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri, kwa kuwa ninyi nanyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.” (Kutoka 22:21). Kumbe,  mwanasheria huyu alitaka bado kujua kwake yeye binafsi nani hasa ni jirani yake. Yesu anamtolea uvivu kwa kumpa mfano ili ajijibu tena mwenyewe.

“Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko” Mji wa Yeriko ulikuwa bondeni umbali wa km 27 kutoka mji wa Yerusalemu uliokuwa milimani. Yesu aliijua sana barabara ile inayopita katika jangwa la Yuda na kwamba ilishamiri kila aina ya ujangili. Hivi ilibidi kusafiri katika vikundi. Lakini kwa bahati mbaya hatujui chochote juu ya mtu huyu, kwani hatajwi jina. Kwa vile alitokea Yerusalemu pengine alikuwa kwenye ibada. Halafu haisemwi alikuwa mwema au mbaya. Mbaya zaidi alikuwa peke yake. Ama kweli humu ulimwenguni kila mmoja ni msafiri tena anasafiri peke yake. Sifa pekee ni kwamba alikuwa binadamu mwenye haki na hadhi ya kuishi na kuheshimiwa kama inavyopasika kwa binadamu wote.  Kumbe binadamu mwenzetu huyu katika safari zake za hapa duniani anapambana na majangili, wakamvua nguo yaani kumdhalilisha; wakamtia majeraha, (kumjeruhi) wakaenda zao wakimwacha nusu kaputi yaani walitaka kumwua.

Yaliyompata mwenzetu yanawakilisha maisha anayokumbana nayo  binadamu yeyote yule hapa duniani, yaani kupambana na watu wanaokudhalilisha yaani kukuvua nguo mbele za watu kwa njia ya maneno ya madharau nk, au wanaokudhulumu na mwisho kukuacha hoi. Hadi hapa Yesu angeweza kumaliza mazungumzo na kutoa fundisho la maisha. Lakini kwa vile anamtaka huyu mwanasheria afikie kupata jibu yeye mwenyewe hapo anawaingiza watu wa kanisa wanaotegemewa kumsaidia binadamu huyu aliyepigika ndipo anapoendelea:

Kwa nasibu kuhani mmoja (padre au mchungaji) alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando.” Waisraeli waliwagawa makuhani katika ngazi ishirini na nne za kuendesha madhehebu hekaluni kwa wiki moja, kwa mwaka mara mbili. Kila kuhani aliishi sehemu yake na ilipokuwa na zamu yake alifika Yerusalemu. Yaonekana kuhani huyu alitoka hekaluni kusali na anarudi nyumbani baada ya huduma “alishuka kwa njia ile.” Huyu kuhani ndiyo kwanza ametoka hekaluni kusali na kutenda mambo ya Mungu. Tungetegemea amepata roho ya Mungu ya kupenda wajane, kuonea huruma wagonjwa, vilema, maskini nk. kumbe hana lolote, ni kuhani hewa.

Kadhalika mlawi alipofika pale akamwona, akapitia kando. Mlawi alikuwa kama msakrastani katika hekalu, yaani alikuwa mtu wa kushika mambo matakatifu ya hekalu na kushika sheria kama kuhai, kumbe naye maisha yamemshinda.  Baada ya kuwataja watu hawa wa dini, mwanasheria yule nadhani akasubiri kwa hamu labda Mwalimu atamtaja mlei atakayeweza kuokoa jahazi, kwa sababu walei ndiyo wanaofuata dini kwa matendo yao mema. Kinyume chake, Yesu anamwingiza mtu wa kuja, kafiri tena mpagani, asiyeenda hata kusali. Wao walikuwa wanafuata vitabu vitano tu vya Torati ya Musa.

Ilikuwa ni dharau kubwa sana kwa Myahudi kuitwa Msamaria, kwani Wasamaria hawakuwa katika orodha ya kuitwa watu. Kumbe, huyu kafiri asiyeshika dini “mtu wa kuja” Mnyamahanga” “Kyasaka” ndiye aliye na roho na huruma ya Mungu. Hapa unaona kuwa katika kila binadamu kuna mbegu au zawadi ya kimungu ya maisha ya milele. Hali hiyo ya Mungu ni kama amri kumi mpya kwa anayetaka kuwa mtu kadiri ya moyo wa Mungu. Ukiruhusu nguvu uliyopewa na Mungu ijitokeze hapo utafanya matendo ya huyu msamaria. Hali inayojidhihirisha katika matendo haya kumi yafuatayo: “Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia.”

Tendo la kwanza, alipomwona. Kuona ni jambo muhimu. Binadamu wa kweli anafungua jicho na kuona matatizo ya wengine. Kumbe kishawishi kikubwa ni kutotaka kuona matatizo ya wengine. Badala yake tunatazama juu kwa Mungu. Kumbe Mungu anataka tusimtazame kwa sababu yeye hahitaji macho yetu, na yeye anaangalia waliko binadamu. Msamaria anaangalia anakoangalia Mungu, yaani chini kwa watu na anamwona binadamu mwenzake aliyepigika.

Tendo la pili, akamhurumia yaani anavutwa na roho ya Mungu inayomsukuma kuonja kama Mungu. Roho hiyo inamsukuma huyu msamaria na anawajibika sawasawa kama anavyoonja Mungu. Tendo la tatu anamkaribia. Baada ya kupata roho ya huruma haogopi tena, anamsogelea bila woga, kwani anasukumwa na damu ya kimungu ya upendo na huruma iliyoko ndani yake. Mkristu wa kweli anamkaribia jirani ili kuona kinachomsibu. Tendo la nne, Akamfunga jeraha zake. Tendo la tano, akazitia mafuta na divai. Sita, akampandisha juu ya mnyama wake. Saba, akampeleka mpaka nyumba ya wageni. Nyumba hiyo haikuwa ya wageni yaani guest house, ambayo kwa kigiriki wanaita xenodokheion ambako hupokewa wageni au wakimbizi na watu wa kuja.

Kumbe, msamiati uliotumika hapa ni pandocheion yaani mahali wanapopokewa watu wote. Maana hii ya pandecheion – yaani nyymba ya wote inatudokezea kuwa msamaria huyo ni Yesu mwenyewe aliyefika kumsaidia binadamu ambaye ameshindwa kusaidiwa na makuhani wala walawi. Naye Yesu hakumpeleka nyumba ya wakimbizi bali  nyumba ya watu wote. Hivi Yesu anawabeba wote na kuwapeleka kwenye ukombozi yaani nyumbani kwa Baba.

Tendo la nane, Akamtunza, na tendo la tisa, siku ya pili akatoa dinari mbili akampa pandochei. Tendo la kumi, akamwagiza pandecheos, amtunze mgonjwa wake kwa siku mbili na atakaorudi itakuwa siku ya tatu atakuja kumaliza kulipa deni. Yesu kweli alifika kuokoa ulimwengu na kulipa gharama yote na kama kuna zaidi ya kulipa analipa yeye kwa kufa na kufufuka kwake siku ya tatu. Kumbe Yesu anaacha roho ya Mungu iliyo ndani ya kila mtu ijitokeze. Kisha Mwalimu anauliza swali lake la tatu: waonaje wewe, katika hao watatu, ni nani aliyekuwa jirani yake yule aliyeagukia kati ya wanyang’anyi?. Mwanasheria hajibu moja kwa moja kuwa alikuwa ni msamaria, bali anasema: “Ni huyo aliyemwonea huruma.” Yesu anamwambia, “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Kuonea huruma maana yake ni kuona, kuonja kama Mungu na kuingilia kati. Kila mmoja anahitaji kukaribiwa na ndugu zake na kuonewa huruma. Anayemhurumia mwenye shida yuko katika vionjo vya Mungu hata kama angekuwa wa dini gani. Hii ndiyo Sheria ya mirathi hasa ya ile uzima wa milele.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB!








All the contents on this site are copyrighted ©.