2016-07-06 14:08:00

Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa sheria zote!


Amri kuu ya mapendo yaani upendo kwa Mungu na kwa jirani yako ni muhtasari wa maisha yote ya kikristo. Amri zote za Mungu zinatuelekeza katika kuifikia namna hii ya maisha na kuifanya kuwa sehemu ya maisha yetu. Kwa maneno mengine amri ya mapendo inatufanya kuwa wakamilifu katika ukristo wetu na katika maana ya ndani kabisa katika ubinadamu wetu. Lakini pia maagizo, taratibu na amri nyingine za kidunia na kibinadamu ambazo zinapaswa kupata msingi wake katika Mungu nazo zinamwelekeza mwanadamu katika ukamilifu huu huu wa kuwa na mapendo kwa Mungu muumba wake na kwa mwanadamu mwenzake. Dominika hii ya 15 ya mwaka inatupatia nafasi ya kutafakari juu ya dhana hii muhimu ya upendo kama kiungo muhimu katika kuzishika na kuzitenda amri, taratibu na maagizo katika maisha yetu ya kila siku.

Upendo wetu kwa Mungu unapaswa kuwa ule unaopita upendo wa kitu kingine chochote, unaopita hata upendo kwa nafsi yako binafsi. Injili inatuambia kwamba tunapaswa kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa roho yote, kwa nguvu zote na kwa akili zote. Hii inamaanisha kwamba maisha yetu yote, mwanadamu mzima mzima anapaswa kuudhihirisha upendo huo. Hakuna fursa katika maisha ambayo inatupatia simile ya kuacha kuuonesha upendo huo: iwe ni nyumbani wakati wa mazungumzo ya kifamilia, wakati wa chakula, wakati wa burudani au wakati wa usingizini; iwe ni ofisini au katika shughuli mbalimbali za kijamii; iwe ni shuleni na mahali popote utakapokuwepo twapaswa kuonesha upendo huo kwa Mungu. Upendo wetu kwa Mungu unajidhihirisha katika utii wetu kwake na kuyasikiliza maagazo yake. Maagizo hayo tunayasikia katika kila nyanja ya maisha yetu. Ni utaratibu ambao ametuwekea kusudi tuendelee kuionja huruma yake, neema zake na baraka zake tungalipo hapa duniani.

Somo la kwanza la Dominika ya leo linatuonesha ukweli huo. Mungu anatuambia kwamba “maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali”. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatuonesha faida tuipatayo kwa kuwa watii wa sauti ya Mungu. Ingawa hatuisikii wazi kutoka sehemu hii ya Maandiko Matakatifu tuliyoisikia lakini tukijisumbua kidogo na kusoma sehemu ya mwanzo ya sura ya hii ya 30 ya kitabu cha Kumbukubu ya Torati utaona kwamba Mwenyezi Mungu anaweka ufanisi katika maisha ya mwanadamu kama tunu ya udhihirisho wa mapendo yetu kwake yasiyo na kikomo. Neno la Mungu linatuambia kwamba: “nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako, nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao ... ndipo Bwana, Mungu wako atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako. (Kumb 30:1 – 3).

Ni vema tukatafakari mantiki hii ya kumpenda Mungu daima katika kuzishika amri zake. Sisi wanadamu tutakapokuwa tayari kuitambua nafasi ya Mungu tukianzia katika fumbo la uumbaji ndipo tunapoona nafasi na mkono wa Mungu katika kila tendo la maisha yetu hapa duniani. Dhambi ilipoingia ulimwenguni kwa mwanadamu kuindoa nafasi hiyo ya Mungu, pale mwanadamu alipouondoa upendo wake kwa Mungu ili awe huru kama alivyodhania ndipo tunayaona matunda yake katika kadhia zote za ulimwengu wetu wa leo. Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi alipomaliza kazi yake ya uumbaji “akaona kila kitu alichokifanya, na tazama ni chema sana” (Mw 1:31). Lakini leo hii tunashuhudia maovu ya aina mbalimbali yanaitawala jamii ya mwanadamu. Hii inamaanisha kwamba uzuri na ukamilifu uliowekwa na Mungu unaonekana kufifia au kupotea kabisa.

Sasa tujiulize uovu huu umetokea wapi? Kwa nini mwanadamu anaendelea kuubomoa ulimwengu huu kwa mikono yake mwenyewe?, huko wapi upendo wake kwa jirani yake katika mazingira haya ya leo ambayo yamejaa mauaji, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, unyonyaji wa kila aina na maovu mengi yanayozidi kumtafuna mwanadamu? Ni mazingira yanaayoashiria ukosefu wa uhai. Kristo alipomtamkia yule mwanasheria amri hii kuu ya mapendo alimwambia “fanya hivi nawe utaishi”. Hivyo mazingira haya yasiyo rafiki kwa kwa uhai wa mwanadamu ni udhihirisho kwetu kwamba tumeacha kumpenda Mungu. Lakini bado tunakumbushwa kwamba katika utendaji wetu wa maisha ya kila siku ndipo tunakutana na maagizo ya Mungu na kudhihirisha upendo wetu kwake. Lakini upendo huo au mazingira hayo yanamweka jirani yetu mbele yetu ambaye tunakutana naye kila siku. Ndiyo maana upendo wetu kwa Mungu unapaswa kujifungamanisha na upendo wetu kwa jirani zetu.

Upendo kwa Mungu na kwa jirani ni sawa na sehemu mbili za bawaba. Sehemu moja inapokosekana basi sehemu nyingine inakosa umaana wake. Huwezi kusema unampenda Mungu kwa ibada, sala na sadaka wakati unashindwa kumwona mwanadamu mwenzako anayekulilia msaada wako pembeni yako. Mtume Yohane anatuambia kwamba “Mtu akisema, ‘nampenda Mungu’, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” (1Yoh 4:20). Tunapoelekezwa kumpenda jirani kama tujipendavyo ni mwaliko wa kumwona Mungu katika nafsi ya mwenzako iliyoumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tunaalikwa kuepa masengenyo kwa wengine bali daima kuwazungumzia mema ambayo tunapenda kuyasikia yakizungumzwa juu yetu. Hata kama jirani yako amekosa hupaswi kumtangazia ubaya huo ili kuliharibu jina lake bali kumtakasa na kusaidia aendelee kutembea katika utakatifu mbele ya wengine.

Upendo wetu kwa jirani zetu utaendelea pia kuonekana zaidi pale tunapokuwa tayari kuepuka magomvi au mikwaruzano ya namna yoyote, yaani tunapokuwa wapatanishi kwa maana imeandikwa “heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mt 5:9). Katika namna kuu kabisa upendo wetu kwa jirani unajionesha katika mahusiano yetu na wale walio chini ya mamlaka yetu. Upendo huu ujionesha zaidi kwa kuwa watumishi wao. Uongozi au ukuu wa kijamii unapata heshima sana katika utumishi. Namna gani tunawajibu matakwa yao, namna gani tunawaonya na kwa namna gani tunawasaidia. Zaidi ni kuwaangalia wale walio katika utegemezi wa huduma zetu kama yatima, wajane na wengine wengi ambao jamii ya leo imewasukumizia pembeni.

Lakini hasa jirani yangu ni nani? Kawaida ni yule aliye karibu na mimi kwa sababu fulani iwe ni ya kijamii au kidini ila kwa namna ya pekee Yesu anatufundusha fundisho kubwa kuwa jirani yangu ni mwanadamu mwenzangu anayehitaji kuuona ubinadamu wangu bila kujali mipaka ya namna yoyote. Sehemu ya Injili ya leo inaweza kuelezea tafsiri zote hizi mbili. Sehemu ya kwanza ni wanyang’anyi ambao wanamjeruhi mwanadamu mwenzao lakini pia kwa namna iliyofichika kuhani na mlawi yule pia wanaingia katika kundi hilo kwani majambazi wanamjeruhii kimwili na kiuchumi na hawa wengine wanamjeruhi kijamii. Hawamwoni kama mtu huyo ni binadamu mwenzao bali wanaangalia ambacho watafaidika nacho. Hawa wa kwanza wanafungwa na sababu za kiuchumi na kuona namna ya kuujeruhi ubinadamu kusudi wao kuendelea kuneemeka kipesa. Na hawa wa pili wanafungwa na sababu za kijamii iwe ni kidini au kijamaa ili wao waendelee kuwa vema katika afya ya roho na kuuacha ubinadamu huu ukiendelea kudhalilika hapa chini. Sheria, taratibu na mazoea ya kibinadamu yanatufanya tusiweze kuona mbele na kumtazama mwenzetu bali kujingalia wenyewe.

Sehemu ya pili ni yule Masamaria. Msamaria anamwona mwanadamu anayeteseka: aangalii mali atakazofaidika nazo wala uhusiano wa kijamii anaokuwa nao. Makandokando haya hayaondoi hamu yake na kumuona mtu anayeteseka. Kristo anamthibitisha kuwa huyu ndiye jirani wa kweli: “Ni yule aliyemwonea huruma”. Huruma kwa wenzetu ndiyo inatufanya tuwe majirani. Huu ndiyo ujirani wa kikristo ambao unatusukuma daima kumwangalia mwanadamu aliyejeruhiwa na kumrudishia tena afya na hadhi yake.Tunajifunga na mengi leo hii: labda sababu ya mali zetu, labda sababu ya utaifa wetu au rangi yetu, labda sababu ya uwezo wetu kiuchumi nk. Tunajengeana kuta na kushindwa kuona ubinadamu wa wenzetu wanaoteseka. Leo hii tunaalikwa kutafakari Upendo wetu kwa jirani zetu.

Mtume Paulo anatukumbusha katika somo la pili kwamba sote tunaunganishwa katika Kristo. Yeye ndiye mzaliwa wa kwanza wa vyote. Vyote vikiwemo mamlaka na mali za ulimwengu huu zinaunganishwa kwake. Tutalielewa vema hili pale tunapoelewa kuwa yeye ni utimilifu wa ufunuo wa Baba, utimilifu wa huruma yake, huruma ambayo imejumuishwa katika utume wake. Tumwombe Mungu neema ya kumpokea Kristo kama ufunuo na ukamilifu wa sheria yake ili kwa njia yake mapendo yetu kwake na kwa jirani zetu yawe sababu ya kuishuhudia huruma yake ikistawi katika maisha ya wanadamu.

Kutoka studio za Radio Vaticani mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.