2016-07-05 12:01:00

Familia Barani Afrika, Jana, Leo na Kesho: Kadiri ya Mwanga wa Injili


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kuanzia tarehe 18 hadi 25 Julai 2016 linaadhimisha mkutano wake wa kumi na saba unaoongozwa na kauli mbiu “Familia Barani Afrika, Jana, Leo na Kesho: kadiri ya Mwanga wa Injili”. Hii itakuwa ni fursa kwa Kanisa Barani Afrika kupembua kwa kina na mapana kuhusu utume wa familia Barani Afrika. 

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia, matunda ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia pamoja na katekesi ya kina,anawaalika waamini kutafakari ya maisha ya ndoa na familia katika mwanga wa Neno la Mungu. Wawe na ujasiri wa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo, daima kwa kuangalia uso wa huruma ambao Yesu Kristo anauelekeza kwa familia ya binadamu kwa nyakati hizi. Lengo ni kulinda, kutetea na kudumisha utume wa familia unaofumbatwa katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi, wanaoendeleza kazi ya uumbaji na elimu na makuzi makini kwa watoto wao.

Padre Joseph Komakoma, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagscar anasema, wajumbe wa SECAM watapata nafasi ya kuchambua wosia wa Baba Mtakatifu Francisko kadiri ya mazingira ya familia Barani Afrika kadiri ya mwanga wa Injili. Hii inatokana na ukweli kwamba, Maaskofu wengi waliguswa na kipaumbele cha pekee kilichotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa familia.

Mkutano wa SECAM unatarajiwa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu Barani Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ni matumaini ya waamini wengi kwamba, wajumbe wa SECAM wataendelea kuhamasisha ukuu, utakatifu na uzuri wa maisha ya ndoa na familia kama kitalu cha miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Mkutano wa SECAM unafanyika mjini Luanda, Angola na kwamba, wajumbe wataonja pia ukarimu wa familia ya Mungu nchini Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.