2016-07-04 10:46:00

Wananchi DRC wanataka haki, amani, ustawi, usalama na demokrasia


Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limehitimisha mkutano wake wa mwaka kwa kuwataka wanasiasa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, usalama na umoja wa kitaifa na kwamba, kuna haja ya kulinasua taifa kutoka kwenye mkwamo wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo. Mambo haya yasipopewa kipaumbele cha kwanza nchi inaweza kujikuta ikitumbukia katika maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Tangu mwaka 2011 Rais Joseph Kabila alipochaguliwa tena, wachunguzi wa mambo wanasema, uchaguzi huu haukuwa huru wala wa haki na mwaka 2015 mchakato wa uchaguzi ukakwama baada ya Rais Kabila kutaka kuwania madaraka kwa awamu ya tatu kinyume cha Katiba ya nchi. Matukio yote haya wanasema Maaskofu yamekuwa ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii nchini DRC na kwamba, kuhailishwa kwa uchaguzi mkuu kutokana na sababu mbali mbali kumepelekea watu kukosa imani na Serikali iliyoko madarakani ambayo inataka kujiimarisha kisiasa kinyume cha demokrasia.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawataka wanasiasa kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa na moyo wa uzalendo ili kujenga na kudumisha mafao ya wengi kama kielelezo cha ujenzi wa demokrasia ya kweli inayopaswa kuwa ni endelevu. Maaskofu wanakaza kusema dhamana na wajibu wao ni kuwahamasisha wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu wao barabara ili kudumisha mafao ya wengi. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni njia muafaka ya kupata suluhu ya shida na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika jamii, ili hatimaye, uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linakaza kusema, mwelekeo wa sasa inaonekana kana kwamba, mchakato wa majadiliano umekufa, hali inayotishia na kuhatarisha haki msingi za binadamu. Kumekuwepo na vitendo vya mauaji ya kinyama na ukosefu wa haki, amani na utulivu miongoni mwa wananchi wengi. Kuendelea kushuka kwa thamani ya fedha ya DRC pamoja na kuibuka kwa vyama vipya kwa kisiasa ni mambo ambayo hayagusi kimsingi matarajio ya wananchi wengi wa DRC. Inaonekana kwamba, uchu wa mali na madaraka unaendelea kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa wananchi wa DRC.

Katika mazingira na hali kama hii wanasema Maaskofu wa DRC, Kanisa halina suluhu ya kisayansi wala kisiasa, bali linawataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira bora zaidi yatakayoiwezesha DRC kufanya uchaguzi huru na wa haki kwa kuzingatia misingi ya amani na utulivu. Katiba ni sheria Mama, kumbe inapaswa kuheshimiwa na wote na kwamba, viongozi waliomaliza muda wao wanapaswa kuachia ngazi kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya kweli.

Viongozi wa kisiasa wanapaswa kusikiliza mateso, machungu na kilio cha wananchi wa DRC, ili kukipatia ufumbuzi wa uhakika. Kamwe wanasiasa wasiwasaliti wananchi kwa kushindwa kudumisha uhuru na demokrasia ya kweli. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana katika kukoleza na kudumisha mchakato wa uchaguzi mkuu ambao unapaswa kuwa wa kidemokrasia, huru, wazi pamoja na kujikita katika amani. Haki jamii kama vile: elimu, afya, maji safi na salama, nisati ya umeme na mishahara ya haki ni mambo ambayo yanapaswa kudumishwa kwa mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali pamoja na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudumisha haki msingi za binadamu, tunu bora za kidemokrasia, utawala wa sheria, haki na amani jamii. Chuki na uhasama kati ya watu ni mambo ambayo yanakwamisha ustawi na maendeleo ya DRC. Umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini humo kujenga na kuimarisha matumaini yanayonesha kwamba, Mwenyezi Mungu yuko katika historia na maisha ya watu, hata kama kwa sasa anaweza kuonekana kana kwamba, hayupo karibu, lakini bado anaendelea kutenda, huku akiwaelekeza watu wenye mapenzi mema kujikita katika haki na amani, kwa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha miiko na maadili ya kazi; demokrasia na utawala wa sheria, ili haki jamii iweze kushika mkondo wake badala ya wananchi kuendelea kuishi katika wasi wasi na mashaka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kwa sasa kipaumbele cha kwanza ni demokrasia katika misingi ya haki na amani na kwamba, Tume huru ya uchaguzi nchini DRC inapaswa kujipanga vyema ili kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara bila kuonesha upendeleo wowote. Vijana wawe makini na kamwe wasitumiwe na wanasiasa ucharwa kwa ajili ya mafao yao binafsi. Wananchi wawe makini katika mchakato mzima wa uchaguzi nchini DRC ili kuimarisha utawala wa kidemokrasia.

Kanisa litaendelea kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema ili kuendesha kampeni ya elimu ya uraia, ili kuwawezesha wananchi kuwajibika barabara katika mchakato mzima wa zoezi la kupigaji kura, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo la Kanisa ni kutaka kuunda dhamiri nyofu kwa wananchi ili kuwajibika barabara katika kukuza na kudumisha demokrasia na utawala wa sheria. Kanisa halina chama, lakini waamini wake ni wanawanachama vyama mbali mbali vya kisiasa. Hapa utawala wa sheria ndio unaotakiwa nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.