2016-07-04 14:21:00

Papa Francisko kutembelea Assisi tarehe 4 Agosti 2016


Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa hapo tarehe 4 Agosti 2016 kutembelea Kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi majira ya jioni. Tukio hili linakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu atatembelea Kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi kama hujaji na hii ni safari binafsi. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kusali na kutafakari kwenye Kanisa Bikira Maria wa Malaika mjini Assisi na baadaye kutoa tafakari kidogo kwa waamini watakaokuwepo Kanisani hapo!

Taarifa hii imetolewa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya ambalo limepewa dhamana na wajibu wa kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Askofu Domenico Sorentino, viongozi wa Shirika la Wafranciskani pamoja na familia ya Mungu Jimboni Assisi wamepokea taarifa hii kwa matumaini makubwa, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, hija ya maisha ya kiroho ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ilianza kwenye Kanisa la Mtakatifu Damiani, mahali muhimu sana kwa Mashirika ya Wafranciskani kwani hapa ndio asili yao. Ni mahali ambapo Mtakatifu Francisko aliguswa kwa namna ya pekee na neema ya Mungu, kiasi cha kujisadaka na kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika kona hii ya maisha, Mtakatifu Francisko alionja upendo wa Bikira Maria, ambaye vizazi vyote vinamwita Mwenyeheri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.