2016-07-02 15:30:00

Utu, ukarimu na ushirikiano mambo msingi kwa ujenzi wa Bara la Ulaya!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya Video, Jumamosi, tarehe 2 Julai 2016 ameungana na wanachama wa vyama na mashirika ya kitume kutoka  katika Makanisa na sehemu mbali mbali za Ulaya huko Bavaria, Munich, Ujerumani ili kwa pamoja kuweza kutafakari juu ya Ulaya. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Kukutana, Upatanisho na Yajayo” ili kuweza kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazoendelea kulikumba Bara la Ulaya.

Kuna kuta za utengano zinazoonekana na zile zisizoonekana zinazoendelea kuligawa Bara la Ulaya. Kuna kuta zinazoendelea kujengeka katika nyoyo za watu. Ni kuta za woga na wasi wasi; ukatili na hali ya kutofahamiana kutokana na mahali anapotoka mtu, dini na imani za watu. Hizi ni kuta za ubinafsi wa kisiasa na kiuchumi zisizoheshimu wala kuthamini maisha na utu wa watu. Bara la Ulaya kwa sasa linajikuta njia panda, daima likijikita katika utandawazi lakini pasi na kuwa na moyo wa Ulaya.

Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama Bara la Ulaya litatambua matatizo na changamoto hizi, lazima liwe na ujasiri wa kufanya mabadiliko yanayojikita katika upembuzi yakinifu kuhusu amana yake inayobubujika kutoka katika Ukristo na wala si kama Jumba la makumbusho na kuangalia ikiwa kama bado linaweza kuwa chachu ya utamadunisho, ili kuwalishirikisha walimwengu amani na utajiri wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwapongeza wajumbe hawa kwa ushiriki wao unaopania kukabiliana na changamoto za Bara la Ulaya, ili kuonesha ushuhuda wa mwanga kwa jamii inayojikita katika ukarimu na mshikamano kwa maskini na watu wanaohitaji msaada zaidi; wanataka kujenga madaraja ya watu kukutana ili kuvuka kinzani na mipasuko ya wazi na ile ambayo inajificha katika nia za watu! Ulaya bado inapaswa kuwa ni mahali ambapo mbingu na dunia zinakutana; kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kielelezo makini cha mtu kutoka Ulaya na dunia ni alama ya uwezo wa kupambana na magumu pamoja na changamoto za maisha.

Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wa vyama na mashirika haya yalioasisiwa Barani Ulaya, ambao wamekirimiwa zawadi na mapaji mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kuyatumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Sote kwa pamoja kwa ajili ya Ulaya ni nguvu inayowaunganisha huku wakiwa na lengo maalum la kuhakikisha kwamba, wanamwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama jibu muafaka kwa Bara la Ulaya ambalo kwa sasa linakabiliwa na kinzani.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuhakikisha kwamba mtindo wa maisha yao unajikita katika upendo unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo, kwa kujenga na kudumisha utamaduni unaoheshimu na kuwathamini wengine; utamaduni unaoonesha ukarimu na kusaidiana. Hapa kuna umuhimu wa kutambua na kuthamini karama mbali mbali ili kujenga na kuimarisha umoja.

Uwepo wa Kristo Yesu kati yao, unawajengea imani na ushuhuda wa kuamini. Pale umoja na utofauti unapoheshimiwa na kuthaminiwa, hapo mchakato wa ujenzi wa familia moja unaanza, kwa kushirikiana na kushikamana pasi na wasi wasi. Ikiwa kama Bara la Ulaya linataka kuwa familia moja ya watu, lazima litoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu; kwa kujikita katika ukarimu, ushirikiano katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wajumbe hawa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anawakirimia mambo mapya, kumbe, wanapaswa kuwa tayari ili kuweza kushangazwa na matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Wawe ni mashuhuda wa matendo mapya yanayotekelezwa na Mungu katika maisha yao ili matunda ya Injili yaweze kuendelea na kukomaa kwani kwa takribani miaka elfu mbili mizizi ya Ukristo imelirutubisha Bara la Ulaya. Wanapaswa kuendelea kuzaa matunda makubwa zaidi na kuendelea kupyaisha karama zao huku wakipanua na kudumisha Bara la Ulaya.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, nyumba zao, jumuiya na miji yao inakuwa ni maabara ya umoja, urafiki na udugu, huku wakiwa na uwezo wa kushirikiana na wengine, wazi kwa ajili ya ulimwengu mzima! Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya ni changamoto pevu kwa wakati huu. Bara la Ulaya ambalo linajengwa na nchi mbali mbali, wao wawe ni mashuhuda kwamba, ni watoto wa Baba mmoja na ndugu wamoja. Waendelee kuwa mbegu ya matumaini ili Bara la Ulaya liweze kugundua wito na kusaidia kuchangia katika umoja wa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.