2016-07-02 15:04:00

Bara la Ulaya: Kukutana, Upatanisho na Yajayo!


Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya “Together 4 Europe” ni hija ya umoja katika utofauti iliyoanzishwa kunako mwaka 1999 inayounganisha vyama, mashirika na makanisa yapatayo mia tatu kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya. Kwa muda wa siku mbili yaani kuanzia tarehe 1- 2 Julai 2016 wanaadhimisha Kongamano la Tatu la “Sote kwa pamoja kwa ajili ya Bara la Ulaya”, huko Bavaria, Munich, nchini Ujerumani kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kukutana, Upatanisho na Yajayo”.

Kongamano hili linaadhimishwa wakati ambapo machungu na athari za Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya yanaanza kuonekana na kuitikisa Jumuiya ya Kimataifa. Kutokana na athari hizi kuna haja ya wajumbe kufanya upembuzi yakinifu, tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Bara la Ulaya. Kardinali Peter Turkson, Rais wa Barza la Kipapa la haki na amani ameshiriki pia katika kongamano  kwa kukazia umuhimu wa kudumisha haki, amani, ustawi na mafao ya wengi.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo amejikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaojikita katika huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama kielelezo cha imani na ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake. Viongozi wakuu wa kidini wameshirikisha pia mawazo yao kwenye kongamano hili. Kwa upande wao viongozi wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wanasema wanaendelea kuifanyia kazi changamoto ya upatanisho miongoni mwa Makanisa sanjari na kujielekeza zaidi katika mchakato wa Umoja wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.