2016-07-01 15:58:00

Usalama barabarani kwanza!


Heri wenye rehema maana hao watapata rehema ndiyo kauli mbiu inayoongoza Siku ya Usalama Barabarani Kitaifa nchini Hispania, inayoadhimishwa Jumapili tarehe 3 Julai 2016. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaialika familia ya Mungu nchini Hispania kuwa makini na kuwajibika kikamilifu wanapokuwa barabarani, ili kuwa na furaha pamoja na matumaini ya maisha.

Askofu Josè Sànchez Gonzàlez, Mwenyekiti wa Idara ya Usalama Barabarani, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa pia kwa watumiaji wa barabara kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma kwa waja wake. Anawataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuokoa maisha na mali za watu. Wanapokuwa barabarani wawe makini, watulivu, waelewa na watu walioelimika.

Iweni na huruma kama Baba ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kutohukumu bali wajenge utamaduni wa kusamehe pamoja na kuiga mfano wa Msamaria mwema aliyemhudumia yule mtu aliyekuwa amevamiwa na wanyang’anyi! Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaendelea kusema kwamba, hata leo hii kutokana na sababu mbali mbali, familia ya Mungu nchini Hispania inaweza kukutana na watu waliopigwa na kujeruhiwa, watu wanaohitaji msaada wao wa hali na mali.

Maaskofu wanasema kama ilivyokuwa nyakati zile za Yesu, hata leo hii kuna watu wataendelea kushika hamsini zao bila kujali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Ni watu ambao wanasongwa na mambo mengi kiasi cha kushindwa kumwilisha imani yao katika matendo. Hizi ni dalili za ukavu wa maisha ya kiroho. Yesu anatoa changamoto kwa wafuasi wake kuiga mfano bora wa Msamaria mwema kwa kuwa jirani wema kwa watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Umwilishaji wa matendo ya huruma kiroho na kimwili ni ushuhuda wa imani tendaji inayomsukuma mtu kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na watu wenye shida zaidi; kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa na wafungwa. Lakini bado kuna maelfu ya watu wanaoendelea kupoteza maisha yao na hata wakati mwingine kupata vilema vya kudumu kutokana na ajali barabarani. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaiombea familia ya Mungu nchini humo ili kuwa na huruma kwa jirani zao kwa kuwasaidia na kuwa makini wanapokuwa barabarani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.