2016-07-01 14:43:00

Papa Francisko aanza likizo ya kipindi cha kiangazi!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Baba Mtakatifu Francisko ameanza likizo ya kipindi cha kiangazi. Kumbe, kuanzia sasa katekesi zote siku ya jumatano zimefutwa, isipokuwa Baba Mtakatifu ataendelea kutoa tafakari ya Injili, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kila Jumapili kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ratiba inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Julai 2016 atakutana na Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lyon, Ufaransa ambaye ataambatana na wagonjwa pamoja na walemavu 200 kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Lyon, Ufaransa.

Tarehe 27 Julai 2016, Baba Mtakatifu Francisko ataondoka mjini Roma kuelekea nchini Poland kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland kuanzia tarehe 26 – 31 Julai 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Baba Mtakatifu atarejea tena mjini Roma Jumapili jioni, tarehe 31 Julai 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.