2016-07-01 15:28:00

Huduma makini kwa wahamiaji na wakimbizi toka Syria na Iraq


Katika shida na mahangaiko ya kibinadamu kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee nchini Syria, Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum linaendelesha kozi maalum kwa Wakleri na wafanyakazi wa Mashirika ya misaada, ili kuwajengea uwezo wa kutoa huduma makini kwa waathirika wa vita. Kozi hii imefunguliwa rasmi, tarehe 29 na inafungwa tarehe 2 Julai 2016, huko Beirut, nchini Lebanon.

Kozi hii imegharimiwa na Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki. Monsinyo Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Cor Unum pamoja na Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria wanashiriki katika kozi hii. Lengo ni kuweza kupembua kwa kina na mapana mahitaji ya waathirika wa vita nchini Syria ili kuyapatia uzito unaostahili. Washiriki wa kozi hii pamoja na mambo mengine wanagusia kuhusu taalimungu ya huduma pamoja na kuwajengea uwezo wa kuratibu shughuli na huduma za misaada huko Mashariki ya Kati: kwa kubuni, kutekeleza na hatimaye kuthaminisha huduma iliyotolewa.

Takwimu zinaonesha kwamba, tangu kulipotokea vita nchini Syria kunako mwaka 2011 zaidi ya watu laki nne wamekwisha kupoteza maisha yao na wengine millioni mbili wamepata majeraha makubwa na ya kudumu na kuna watu zaidi ya millioni kumi na mbili wanaohitaji msaada wa dharura nchini Syria. Wakimbizi kutoka Syria na Iraq kwa sasa idadi yao imefikia millioni tisa na kati yao millioni nne ni wakimbizi kutoka Syria. Cor  Unum inayoratibu misaada ya Kanisa Katoliki huko Mashariki ya Kati, imekwisha kutumia zaidi ya millioni 150 kwa ajili ya waathirika wa vita huko Mashariki ya Kati katika kipindi cha mwaka 2015. Maeneo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza ni: elimu, msaada wa chakula; huduma ya afya, makazi pamoja na huduma za kupanga. Taarifa ya msaada kwa kipindi cha mwaka 2015- 2016 inaendelea kufanyiwa kazi na itatolewa kwa wakati muafaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.