2016-06-30 14:25:00

Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro!


Dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha umoja wa Kanisa. Kristo Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro madaraka ya kuwa ni mtumishi na mhudumu wa kwanza wa umoja wa Kanisa. “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni na lolote litakalofunguliwa duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu wakati alipokuwa anakabidhi tuzo ya Mtakatifu Petro  “Tu es Petrus” kwa Maaskofu waliojipambanua kwa huduma makini kwa familia ya Mungu katika majimbo yao. Anaelezea nafasi na dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo makini cha Urika wa Maaskofu.

Yesu alitambua fika nguvu na udhaifu wa Mtakatifu Petro akamwambia kwamba, amemwombea ili asitindikiwe na imani ili akiisha imarika aweze pia kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Mababa watakatifu katika historia ya maisha na utume wao, daima wamejitahidi kuimarisha imani ya familia ya Mungu, huku wakitumainia maongozi ya Roho Mtakatifu anayelitakatifuza na kulitegemeza Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Daima wamekuwa mstari wa mbele kusoma alama za nyakati na kuendelea kupyaisha imani ya watu wa Mungu kadiri ya historia na mazingira ya watu, kwa kujikita katika utamadunisho.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume Furaha ya upendo ndani ya familia anapembua kwa kina na mapana changamoto ya maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo, ili kuliwezesha Kanisa kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, tayari kusimama kidete kupambana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kutubu na kumwongokea Mungu; kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano na familia zinazoogelea katika hali ngumu ya maisha na wito wao wa kifamilia, ili ziweze kusikilizwa, kusaidiwa na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa, nidhamu ya Sakramenti za Kanisa inayofumbata mikakati ya shughuli za kichungaji zinazosimikwa katika majadiliano.

Baba Mtakatifu anakazia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia sanjari na kutoa malezi makini kwa watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwendelezo wa mafundisho makuu yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yakafanyiwa kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II na kuboreshwa zaidi na Papa mstaafu Benedikto XVI daima akijitahidi kusoma alama za nyakati na sasa Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za usawa wa kijinsia, ili kupata furaha ya kweli inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; ndoa inayojengwa kutokana na upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo.

Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai na huruma ya Mungu. Papa Mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano maalum na mwanataalimungu mmoja anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko amekita maisha na utume wake katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kama ilivyoasisiwa na Mtakatifu Faustina Kowalska na kuendelezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata upendo na huruma yake.

Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo makini cha umoja wa Kanisa pale anapotekeleza dhamana hii huku akiwa ameungana na Maaskofu wenzake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu. Ni kiungo muhimu sana katika Urika wa Maaskofu wanapofundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unafumbatwa katika kutafuta na kudumisha mafao ya familia ya Mungu; kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda, umoja, upendo na udugu.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Fumbo la Umoja, Jumuiya ya imani, matumaini na mapendo. Ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu na umoja miongoni mwa watakatifu. Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, Bikira Maria ni chachu ya umoja na wala si sababu ya mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Mtakatifu Petro ni mwamba na nguzo ya Kanisa.

Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa, tayari kujikita katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, ili kudumisha umoja wa watu wa Mungu anasema Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.