2016-06-30 07:21:00

Michezo isaidie kudumisha haki msingi za binadamu!


Michezo na kwa namna ya pekee michezo ya Olympic ni fursa na chombo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii kimataifa sanjari na kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi katika Jumuiya ya Kimataifa. Vatican inathamini sekta ya michezo na burudani ndiyo maana mwezi Oktoba 2016, kutafanyika mkutano wa kimataifa kuhusu imani na michezo. Lengo la mkutano huu ni kuliwezesha Kanisa kupembua kwa kina na mapana sekta ya michezo na utamaduni mintarafu maisha ya kiroho kwa mwanadamu.

Haya yamebainishwa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva alipokuwa anashiriki katika mkutano wa thelathini na mbili wa Baraza la haki msingi za binadamu lililokuwa linajadili jinsi ya kutumia michezo na kwa namna ya pekee, mashindani ya Olympic ya mwaka huu huko Brazil. 

Vatican inatambua na kuthamini kwamba, michezo ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na ushiriki mkamilifu katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki katika michezo, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Michezo ya Olympic pamoja na mambo mengine inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Askofu mkuu Jurkovic anakaza kusema, tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia watu hawa kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu.

Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi , michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi.

Askofu mkuu Jurkovic anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba inapambana kufa na kupona ili kung’oa mwelekeo potofu wa michezo katika mashindano ya Olympic pamoja na mambo yote yanayoweza kukwamisha ukomavu na furaha ya mtu. Hapa kanuni maadili na sheria za michezo zinapaswa kuzingatiwa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kudumisha haki msingi za binadamu pamoja na kujenga utamaduni wa kuwashirikisha watu badala ya kuwabagua pamoja na kuendeleza sera na mikakati ya michezo iliyokwisha bainishwa na Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, hata michezo kwa walemavu ni mfano mzuri wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu ili kuonesha karama, vipaji na mapungufu katika maisha.

Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, michezo itaweza kutumiwa vyema na Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu na kwamba, itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika kudumisha sekta ya michezo kama daraja la watu kukutana; ikiwa kama utu na heshima ya mwanadamu vitapewa kipaumbele cha kwanza, kwani hiki ni chombo madhubuti cha kuweza kuwaunganisha watu wa mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.