2016-06-30 15:12:00

Makada uchwara hawana nafasi tena!


Leo hapa kuna kivumbi! Si bure! “Mfanyakazi hewa” ni usemi ulioshamiri sana, ukimaanisha orodha ya wafanyakazi feki lakini wanapokea mishahara minono. Kwa hiyo wako “Wafanyakazi hewa, Walimu hewa, wanafunzi hewa nk” Msamiati huo unaweza pia kutumika kwa viongozi na wafanyakazi wasiowajibika katika kazi na hata kwa wale wasioishi kadiri ya miito yao mbalimbali ya kazi na ya kidini. Katika kundi hilo tunawakuta, “Wachungaji hewa, maaskofu hewa, mapadre hewa, watawa hewa, masista hewa, waseminari hewa, makatekista hewa, hadi wakristu hewa, nk. Tunaweza pia kuorodhesha dini hewa endapo waumini wake hawaishi kadiri ya maadili yapasikayo. Juma lililopita tulishuhudia mitume kumi na wawili waliotumwa kuandaa ujio wa Yesu, lakini wakamwangusha, kwani alikataliwa. Tungeweza kuwaita hao kuwa walikuwa wajumbe hewa, kwani hawakumwelewa sawasawa Yesu na wakamwakilisha vibaya.

Leo tutaviona vigezo vinavyomtofautisha mkristu aliye kada halisi wa Yesu na mkristu hewa. Kila mmoja ajikosoe mwenyewe. Baada ya Yesu kujieleza kinaganaga na kuwahesabia gharama ya kumfuata, akawatuma tena makada sabini na wawili kwenda kuandaa ujio wake kama tunavyosoma: “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini.” Idadi hii ya wafuasi inawakilisha mataifa ya kipagani, kwa hiyo inahusu umisionari wetu sisi wakristu wote. Ni muhuimu kwetu kutafakari jinsi Yesu anavyotaka tujipange tunapoenda ulimwenguni kupeleka Injili yake tusijekuwa watumishi hewa.

Yesu “akawatuma wawili wawili.” Idadi hii ina maana tatu muhimu: Mosi, kwamba utume wa Yesu siyo shauri la mtu binafsi peke yake eti ndungulindunguli kwenda kueneza Injili, bali ni tendo la kijumuia, kwani “umoja ni nguvu.” Hata mitume walienda wawili wawili, kama vile Petro na Yohane walitumwa Samaria (tulisikia Jumapili iliyopita); Paulo na Barnaba walipelekwa jumuia ya Antiokia (Yuda) katika ufalme wa Kirumi. Petro na Paulo ni miamba ya imani huko Roma.

Kwa hiyo, wanaomtangaza Yesu wanatakiwa wajisikie daima kama jumuia ya kikristu yaani kanisa. Kwa mantiki hiyo wakristu tunayo bahati nzuri kuwa na jumuia ndogondogo. Jumuia zinazowajibika, ni tegemeo kubwa sana katika kumhubiri Yesu na Injili yake, vinginevyo ni “Jumuia hewa.” Pili, namba hiyo inamaanisha ushahidi wa kweli wa ujumbe unaotangazwa katika biblia. Kama jumuia haimshuhudii Yesu, hiyo ni jumuia hewa. Tatu, idadi hiyo inarejea kwenye ujumbe muhimu zaidi aliosema Yesu: “Pale walipo wawili au watatu walioungana kwa ajili yangu nami nipo kati yao,” wale walio katika jumuia, budi wajisikie kuwa Yesu yu pamoja nao. Kama wanajumuia hawapendani na hawana mikakati ya kuwatumikia na kuwapenda wengine, hapo Yesu hayupo na hivi ni jumuia hewa.

Kisha Yesu “akawatuma wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.” Kwa hiyo lengo la kwanza la kila mfuasi ni kutangulia kwenda kuandaa mioyo na akili ya watu kumpokea Yesu na siyo kwenda kujinadi na  kujionesha utaalamu wako wa kuongea. Hapa wachungaji wanaotafuta sifa zao tu wajue kwamba wao ni hewa. Yesu anasema tena kwamba: “Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache;” Kwa manabii wa Agano la Kale neno kuvuna lina maana ya kuhukumu kwani mvunaji anatumia fyekeo kuvuna na kutoa hesabu ya mavuno. Katika Agano jipya mavuno ni ujumbe wa ukombozi. Yesu anatutuma kuvuna na siyo kupanda. Mazingira ya kuvuna ni mapana na mavuno ni mengi sana. Aidha unapovuna hasa ngano baadaye unasaga unga na kutengeneza mkate. Chakula hicho ndicho anachotegemea kukiona Yesu anapowatuma wafuasi wake. Anawategemea wakayatekeleze mapendekezo yake, yaani wawe mkate  kama yalivyokuwa maisha ya Yesu mwenyewe katika Ekaristi, aliposema: “Huu ni mwili wangu, hii ni damu yangu.” Kwa hiyo ni muhimu kwa wafuasi kujihusisha katika upendo wa Yesu usio na mipaka na kuwa mkate.

“Basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake” Neno la kigiriki lililotumika hapa la kupeleka watenda kazi ni ekballein halimaanishi kupeleka bali ni kufukuza na kwa kiingereza ni casting out, / ejecting out yaani ni kufukuzia mbali au tungeweza kusema kuitumbulia mbali roho ya uvivu iliyoko ndani ya wafuasi (wakristu). Yaani kumhimiza mbatizwa kuacha uvivu, kutojiamini na ya kutokukata tamaa kwamba ulimwengu hauwezi kubadilika. Kwa hiyo Mungu anaweza tu kututumbua wavivu na tuliokata tamaa kwa njia  ya sala. Kwani sala itamfanya Mungu atutie tafu wabatizwa ili tuache uvivu, na tuishi kadiri ya hadhi ya mbatizwa, tupokee mapendekezo ya Yesu na tuwajibike katika utume. Kisha Yesu akawaagiza: “Enendeni, angalie, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwamwitu.” Mbwamwitu ni alama ya utawala wa kale wa mabavu, wa ukatili, wa uharibifu na unaotegemea mali. Kondoo ni alama ya unyenyekevu na upole. Mwanakondoo ataweza tu kumshinda mbwamwitu, akijiaminisha kwa mchungaji wake. Kwa hiyo mbatizwa yaani mfuasi wa Kristu asiwe na alama za kiumbwamwitu kama vile kubeba silaha halafu awe kama mwanakondoo mpole na mwenye upendo.

Yesu anawakataza wafuasi wake wasiwe na sifa za wafuasi hewa anawambia: “Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu, wala msimwamkie mtu njiani”. Kutochukua Mfuko wa kubeba mali maana yake wasiwe na sifa ya kukusanya na kujilimbikizia mali. Kujilundikia mali ni sifa ya mafisadi. Kumbe anayemfuata Yesu anaridhika na mahitaji muhimu tu, na mali nyingine anatoa kwa ajili ya wengine. Kutobeba Mkoba au pochi ya kuweka akiba ya pesa, Mfuasi anahubiri na anamtegemea Mungu na kusali “utupe leo mkate wetu wa kila siku.” Kutochukua Viatu, bali kuridhika na kiatu ulichovaa. Aidha, utume bora ni ule wa ana kwa ana kwani mbinu mbalimbali tegemezi za kueneza neno la Mungu pengine zinaweza kuzima hali ya ubunifu wa kulitangaza Neno kiufanisi. Yesu anaagiza tena: Msimwamkie mtu barabarani: kwani kuamkia wakati mwingine kunapoteza muda. Hivi mfuasi anaagizwa kutopoteza muda barabarani kwa michapo, badala ya kuharakisha kwenda kulitangaza Neno. Kuhuni kazi ni sifa za mjichunga hewa.

Halafu, akawaagiza wanapoingia katika nyumba kuamkia hivi: “amani katika nyumba hii.” Nyumba ni mahali ambapo mtu anajisikia huru, na yuko katika umwandani wake binafsi, na ni mahali anapoweza kumkaribisha Yesu. Kwa hiyo anasema mfikapo nyumbani semeni “Tulieni na muwe na amani. Nimefika kuleta amani, na furaha siyo kuwakatisha watu tamaa ya maisha na kuwafarakanisha. Halafu Yesu anasema: “na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la hayumo, amani yenu itarudi kwenu.” Yaani inabidi kurudiarudia kuionesha hiyo amani pengine itaweza kupokelewa.

Endapo kuna watu wanaonesha nia ya kutaka bado kulisikia na kulitafakari neno linalowatuliza katika maisha, basi hapo pokea mwito na ubaki:“Basi, kaeni katika nyumba hiyo hiyo,” ila anaagiza “mkila na kunywa vya kwao;” yaani mle wanavyowapa hapo, msichague aina ya chakula. Kila mhubiri hana budi kuheshimu utamaduni wa mahali kama hawana chakula unachopendelea basi ridhika na unachopewa.  Yesu anakitambua kishawishi cha wafuasi hewa cha kupenda kulowea pale panaponoga na mwisho kupoteza imani ya watu anasema: “Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii.”Halafu anaagiza kupeleka habari njema kila mahala kwani ni ujumbe huo unawachokoza jamii kubwa ya watu anaposema: “Na mji wowote mnaoingia.” Wakishaingia humo mjini, anawaagiza:“Waponyeni wagonjwa.” Maana yake, anayehubiri budi atoe alama halisi za upendo, ambao ni ufalme wa Mungu, alama hizo ni kama vile kuwashughulikia walio dhaifu na wagonjwa nk.

Katika mahusiano na ulimwengu usiosadiki, yawezekana unaweza kuathirika na vumbi fulani fulani ikiwa ni pamoja na lugha au matendo mbalimbali uliyoyashuhudia yanayoweza kukuathiri kiwito au kiuchungaji hapo Yesu anaagiza: “Kama hawawapokei kung’uteni mavumbi ya miguu yenu.” Aidha kama mahubiri yako yanakataliwa wewe using’ang’anize bali ingia moyoni mwako, na subiri wakati mwafaka pengine utakubalika.

Katika kuhitimisha Yesu anasema “Nilimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme.” Hii ni picha ya watawala unaoonekana kutawala ulimwengu, kutoka juu. Hao ni watawala hewa wanaofananishwa na mashetani, kumbe hao wataanguka. Kisha anawatuliza wafuasi wake kwa kuwaambia: “Tazama nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” Hizi zote n ni nguvu za ubaya zitashindwa mbele ya Bwana: “Kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Utawakanyaga simba na nyoka, mwanasimba na joka utawaseta kwa miguu.” (Zab. 91:11-13). Kwamba wanaowajibika, wanalindwa na Bwana mwenyewe.

Ujumbe wa leo unawapatia matumaini ya maisha wale wanaomfuata Yesu na wenye jukumu la kumtangaza Kristu ulimwenguni. Unawalenga wale wanaokata tamaa kwamba pengine ujumbe wa Yesu hautaweza kuenea na kwamba ulimwengu mpya hautakuja. Yesu anatuhakikishia kwamba mavuno ni mengi, isipokuwa wanaomwangusha ni wafuasi au wabatizwa hewa wasiowajibika. Tujaribu kwa pamoja kutumbua majipu kwa njia ya sala na kuwajibika kutangaza Injili ya amani, upendo na huruma kwa maisha na matendo yetu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.