2016-06-28 16:02:00

Wakristo simameni kidete kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 28 Juni 2016 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa kiekumene kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, muda uliokubalika wa kutafakari kuhusu Fumbo la Upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, Mitume Petro na Paulo katika maisha yao ya dhambi wameoneshwa huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Petro alimkana Yesu mara tatu, Paulo akalitesa Kanisa la Kristo, wote wawili wakawa ni watangazaji mahiri wa Habari Njema ya Wokovu na mashuhuda wa zawadi ya wokovu inayotolewa na Kristo Yesu kwa wote pasi na ubaguzi. Kutokana na mwelekeo huu, Kanisa linatambua kwamba, linajengwa na watakatifu wa Mungu pamoja na wadhambi wanaohamasishwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili baada ya kupokea zawadi ya Ubatizo, waweze kusimama kidete kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu.

Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ni muda muafaka wa kupyaisha kumbu kumbu ya msamaha na neema inayoendelea kububujika ndani ya Makanisa ya Roma na Costantinopoli wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, Nidhamu ya Kanisa na katika ulimwengu kama sehemu ya ushuhuda wa ukweli mfunuliwa. Makanisa haya yanaendelea kuonja upendo na huruma ya Mungu, changamoto ya kuwa kweli ni mashuhuda wa upendo huo kwa watu wote pamoja na kumwilisha huruma ya Mungu, tayari kung’oa yale yaliyopita kwa kujikita katika kinzani na mipasuko ya Kikanisa, ili kuanza kuandika ukurasa mpya unaoongozwa na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Makanisa kuongeza bidii ya kuvuka vikwazo vinavyokwamisha ujenzi wa umoja wa Kanisa kwa kuheshimu tofauti na kuendeleza majadiliano ya kitaalimungu. Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wote wa Tume ya pamoja ya Kitaalimungu kwa kazi kubwa wanayoitekeleza hadi wakati huu, takribani miaka hamsini. Majadiliano haya yamesaidia kuboresha mahusiano kati ya Makanisa haya mawili. Baba Mtakatifu anaendelea kusali ili matunda ya Tume hii yaweze kuonekana mapema iwezekanavyo.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kumjalia kukutana na viongozi wa Makanisa mbali mbali wakati wa hija yake ya kitume kwenye Kisiwa cha Lesvos, ili kutembelea wakimbizi na wahamiaji. Ilikuwa ni fursa ya kujionea wenyewe nyuso za watu waliokata tamaa; ili kuwasikiliza na hatimaye kusali kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliokufa maji wakiwa na tumaini la kupata maisha bora zaidi Barani Ulaya.

Changamoto ni kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uwepo wa viongozi hawa wa Makanisa ilikuwa ni faraja kubwa kwa wakimbizi na wahamiaji na kwamba, wanatambuwa kuwa Makanisa haya mawili yanao wajibu wa kushuhudia wito wao kama Wakristo na kuendelea kushirikiana kwa ajili ya huduma kwa binadamu wanaoteseka.

Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu maadhimisho ya Mtaguso wa Kanisa la Kiorthodox, ambao ameshiriki kwa njia ya sala wakati wa maandalizi yake na maadhimisho yake na kwamba, ujumbe kutoka Vatican umeshiriki katika maadhimisho hayo. Ni matumaini yake kwamba, ataweza kupata fursa ya kufahamu mengi zaidi wakati ambapo ujumbe wa Vatican utakaporejea tena mjini Vatican. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu aweze kulisaidia Kanisa kupata matunda yanayokusudiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.