2016-06-28 08:02:00

Mwaka mmoja wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican: Mageuzi!


Monsinyo Dario Eduardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, umegota mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanzisha Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican inayounganisha taasisi tisa za mawasiliano zinazoendeshwa na kusimamiwa na Vatican.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja, Sekretarieti hii imetekeleza dhamana na wajibu wake katika shughuli za kila siku kadiri ya Katiba na mwongozo uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Imekuwa ni fursa ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusiana na taasisi za mawasiliano zinazomilikiwa na kuendeshwa na Vatican katika ujumla wake: kwa kuangalia mfumo wa kazi, rasilimali watu na historia ya taasisi hizi katika maisha na utume wa Kanisa.

Lengo ni kuendelea kuunganisha rasilimali watu ili kutengeneza timu ya wadau katika mawasiliano ya jamii watakaolisaidia Kanisa kuendeleza dhamana na utume wake katika Uinjilishaji mpya. Zaidi ya watu 400 wanatekeleza dhamana na utume wao katika vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Ili kufanikisha azma hii, Sekretarieti ya mawasiliano mjini Vatican imeandaa semina elekezi ili kusaidia mchakato wa ukomavu katika kazi za pamoja, sehemu muhimu sana katika mageuzi yanayoendelea kutekelezwa hapa mjini Vatican.

Monsinyo Viganò anaendelea kufafanua kwamba, katika mkutano wa Makardinali Washauri uliohitimishwa hivi karibuni, ulisikiliza kwa makini mchakato wa mageuzi unaoendelea kufanywa katika sekta ya mawasiliano, ili hatimaye waweze kufanya maamuzi magumu yatakayotekelezwa na Sekretarieti. Mageuzi hayana yanajikita katika njia za mawasiliano, jinsi ya kufikisha ujumbe na kwamba, dhamana hii ni wajibu wa kazi ya pamoja kwa kutambua kwamba, hakuna mtu ambaye anaweza kujidai kwamba, ana ukweli wote mfukoni mwake. Kazi ya pamoja inadai fadhila ya unyenyekevu ili kuweka ujuzi, maarifa, uzoefu na mang’amuzi kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa.

Monsinyo Viganò anasema, mwelekeo wa sasa ni kuviwezesha vyombo vya mawasiliano ya jamii kuingia katika mfumo wa digitali kwa kuzingatia historia, tamaduni na mchakato wa utamadunisho, ili kweli imani iweze kugusa akili na nyoyo za watu. Baada ya Vita kuuu ya Pili ya Dunia, Uinjilishaji na Katekesi vilikuwa ni mfumo wa maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Kanisa linaendelea kusoma alama za nyakati ili kuwatambua wasikilizaji na kutafuta njia za kujibu kiu na udadidi wao wa kutaka kumfahamu Mungu kwa njia ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko analihamasisha Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa watu halisi ambao kila siku wanatumia mitandao ya jamii ili kupata habari. Hii ndiyo maana Sekretarieti ya mawasiliano inaendelea kuhamasisha matumizi bora ya mitandao ya kijamii ili kuweza kufikisha ujumbe wa huruma ya Mungu kwa watu wengi zaidi. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko ameanza kutumia Instagram, mtandao unaotumia picha ili kuelezea matukio mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Katika maboresho ya matumizi ya mitandao ya kijamii, tovuti ya Vatican ambayo inaendelea kuboreshwa itaweza kuwapatia watumiaji wake fursa ya: kusoma, kusikiliza na kuona yale yanayotendeka ili kuweza kuwapatia watu mambo msingi wanayohitaji katika maisha yao. Kwa habari za Kanisa, Vatican inataka kuwa ni chanzo cha uhakika. Katika kipindi cha mwaka 2016, Monsinyo Viganò anaendelea kufafanua kwamba, mchakato wa kuunganisha Radio Vatican na Kituo cha Televishen cha Vatican CTV unaendelea ili kupata RadioTelevisheni Vatican.

Kutakuwepo na kitengo cha Radio Vatican kwa ajili ya wasikilizaji wa Italia kwa lugha mbali mbali. Radio Vatican sasa itajikita zaidi katika maboresho ya mtandao utakaowawezesha wasikilizaji na wasomaji kuangalia pia habari zinazotolewa katika mfumo wa digitali. Wafanyakazi wana ari na mwamko wa kutaka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mageuzi haya kadiri ya matakwa ya Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.