2016-06-28 06:56:00

Mfuko wa Joseph Ratzinger unapania kudumisha utume wa Kanisa!


Mfuko wa Joseph Ratzinger – Benedetto XVI, ulioanzishwa kunako mwaka 2010 ulipania kwa namna ya pekee kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mfuko ambao unajikita katika kumwilisha Injili ya upendo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kumi na wawili kila mwaka kupata nafasi za masomo kutoka ndani na nje ya Italia. Katika kipindi cha mwaka 2015, Mfuko huu umegharimia kiasi cha Euro 120, 000 kwa ajili ya wanafunzi kadhaa.

Taarifa ya Mfuko wa Joseph Ratzinger unaendelea kufafanua kwamba, unasaidia pia kugharimia makongamano ya kitamaduni na kisayansi kadiri ya katiba ya mfuko huu kwani unatambua kwamba, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali muafaka pa kukuza na kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Mfuko huu pia unatoa tuzo kwa wasomi waliojipambanua katika huduma kwa ajili ya kushuhudia na kueneza Injili ya Kristo kwa watu wa mataifa, ili kweli Injili iweze kuingia na kugusa mila, desturi na tamaduni za watu dhamana inayoweza kutekelezwa kwa dhati kabisa kwa njia ya weledi wa kitaaluma, kisayansi na kielimu.  Monsinyo Giuseppe Scotti, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger anasema, mfuko huu sasa utasimamiwa na Baba Mtakatifu Francisko na utaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mfuko huu unamkabidhi Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha Euro millioni 4 kama kielelezo na ushuhuda wa umoja, udugu na utume kutoka kwa Papa Mstaafu Benedikto XVI ili kuendeleza mchakato wa utangazaji wa Injili ya furaha kwa watu wa mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.