2016-06-28 15:50:00

Fumbo la Msalaba ni chemchemi ya neema na baraka!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amewashukuru viongozi wa Kanisa waliowezesha kufanikisha kumbu kumbu ya miaka 65 yangu walipopewa Daraja Takatifu la Upadre. Anamshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kumshangaza katika maisha yake kutokana na wema na uzuri unaopamba moyo wake kuliko hata bustani za Vatican na kwamba, anajisikia kuwa analindwa na kutunzwa vyema. Anamtakia heri na baraka tele katika hija hii ya maisha ya huruma ya Mungu kwa kuwaonesha watu Yesu anayewapeleka kwa Mungu.

Papa mstaafu Benedikto XVI amewashukuru viongozi wote wa Kanisa waliotoa hotuba ambazo kweli zimegusa wito na maisha yake na jinsi ambavyo alijitahidi kutekeleza dhamana na wito huo wa kipadre. Amewashukuru kwa upendo na urafiki ambao wamemwonjesha katika maisha. Kwa namna ya pekee kabisa amemshukuru Kardinali Gerhard Muller kwa kuzindua kazi zake kuhusu wito na maisha ya kipadre, ili kuwasaidia ndugu zake katika Daraja takatifu anapoendelea na maisha yake katika utume mpya.

Leo kwa hakika anasema Papa Mstaafu Benedikto XVI ni siku ya shukrani kwa Kristo kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha aliyeweza kugeuza mateso ya Fumbo la Msalaba kuwa ni chamchemi ya neema na baraka. Kwa njia hii Yesu mwenyewe ameweza kuleta mageuzi makubwa katika maisha kwa kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni chakula na kinywaji cha kweli, chemchemi ya nguvu na upendo wa Kristo. Anaombea ili ulimwengu ujikite katika zawadi ya maisha na wala si ulimwengu unaokumbatia utamaduni wa kifo kwani upendo wa Kristo umeshinda nguvu ya kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.   








All the contents on this site are copyrighted ©.