2016-06-27 06:28:00

Wakristo wanaendelea kujizatiti kujenga umoja wa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku ya Jumapili, tarehe 26 Juni 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu aliyoiadhimisha binafsi pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Vatican nchini Armenia. Amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki wa Armenia ambao kwa sasa wako 14 pamoja na wawakilishi wa Wakleri bila kusahau wajumbe walioko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu nchini Armenia.

Baadaye, Baba Mtakatifu ameshiriki katika Ibada ya Liturujia Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Mtakatifu Tiridate wa Etchmiadzin iliyoongozwa na Patriaki Karekin II. Baba Mtakatifu katika tafakari yake kwenye Liturujia hii takatifu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia fursa ya kuweza kutembelea nchi ya Armenia na kuonja ukarimu wa upendo, udugu na mshikamano kutoka kwa Patriaki Karekin II. Kimekuwa ni kipindi cha sala na tafakari na muda wa kushirikishana: zawadi, matumaini na wasi wasi wa Makanisa haya, kwa matumaini ya kuweza kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo unaofumbatwa katika Bwana mmoja, imani na ubatizo mmoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Maneno haya ya Mtakatifu Paulo ni kisima cha furaha kilichowakutanisha viongozi hawa wakuu wa Makanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Watakatifu Bartolomeo na Thaddeus waliojisadaka kwa mara ya kwanza kutangaza na kushuhudia Injili katika maeneo haya, Watakatifu Petro na Paulo, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, sasa wanatawala na Kristo huko mbinguni na bila shaka watafurahi sana kuona siku moja Makanisa haya yameungana na kuwa kitu kimoja. Pamoja na yote haya, Baba Mtakatifu Francisko anamtolea Mwenyezi Mungu utukufu na shukrani.

Liturujia Takatifu imeutukuza utakatifu wa Mungu na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, Watakatifu na waalimu wa sheria; mashahidi na wafiadini, hasa wale ambao wametangazwa kuwa watakatifu mwaka 2015. Yesu, Mwana wa Mungu aliyeshuka hapa duniani, abariki hija inayofanywa na wafuasi wake, Roho Mtakatifu awasaidie waamini kuwa na roho na moyo mmoja pamoja na kuwakirimia umoja. Roho Mtakatifu anayewaenzi watakatifu na kuwatakasa wadhambi awajalie moto wa upendo na umoja, ili kuunguza yale yote yanayosababisha kashfa ya utengano miongoni mwa Wakristo.

Baba Mtakatifu ameliombea Kanisa la Kitume la Armenia ili liweze kutembea katika amani na umoja kamili, ili kupokea na kumwilisha karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kuzitolea ushuhuda ili kuonesha ukuu wa Fumbo la ukombozi ambalo limetekelezwa na Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusikiliza kwa makini wito wa watakatifu na sauti ya maskini pamoja wahanga wa chuki na uhasama, wanaoendelea kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wawe wasikivu kwa vijana wa kizazi kipya wanaotamani kuwa huru na utengano wa kihistoria. Anamwomba Roho Mtakatifu awajalie waamini mwanga angavu wa imani, mapendo, msamaha na upatanisho. Hata katika mashaka na wasi wasi kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, Siku ile ya Pasaka, waamini waweze kuwa na furaha na matumaini mapya, ili kuharakisha na hatimaye, kufikia umoja kamili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.