2016-06-27 06:49:00

Matumaini mapya kwa familia ya Mungu nchini Armenia


Patriaki Karekin II ndiye aliyeandaa chakula cha mchana Jumapili tarehe 26 Juni 2016 kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na msafara wake, wakashiriki pia Maaskofu wa Kanisa la Kitume la Armenia na Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kuweza kukutana na kuzungumza wajumbe pamoja na wafadhili wa Kanisa la Kitume la Armenia. Baada ya kusalimiana nao, viongozi hawa Kanisa wakawapatia baraka zao za kitume!

Baba Mtakatifu kabla ya kuondoka nchini Armenia amepata nafasi ya kutembelea Monasteri ya Khor Virap, ambako Baba Mtakatifu pamoja na Patriaki Karekin II wamesali kwa pamoja na baadaye kuwapatia baraka zao za kitume. Baba Mtakatifu Francisko katika sala yake ameomba zawadi ya haki na amani, ili kweli waamini kwa msaada wa huruma ya Mungu waweze kupita katika njia ya Mungu, ili hatimaye, siku moja waweze kufika katika bandari ya maisha na wokovu kwani Mwenyezi Mungu ndiye msaada na Mkombozi wao; mwingi wa utukufu, nguvu na heshima, anayeishi na kutawala daima na milelle. Amina. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.