2016-06-27 08:33:00

Kanisa nchini DRC laanzisha Benki ya Wanyonge!


Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC hivi karibuni limezindua Benki ya Wanyonge, itakayosaidia mchakato wa kuwawezesha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kupata mikopo nafuu ili kujikwamua kutoka katika hali ngumu ya kiuchumi na umaskini. Benki iliyoanzishwa na Maaskofu Katoliki DRC inapania kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na kusaidia maboresho ya maisha ya wananchi wengi wa DRC ambao licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali na mali ya asili lakini bado wanaogelea katika umaskini wa hali na kipato.

Askofu mkuu Nicolas Djomo, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anasema mchakato wa kuanzishwa kwa Benki ya Wanyonge, “IFOD” ulianza kunako mwaka 2010 na sasa shughuli za Benki hii zimekwisha sambazwa nchi nzima na inatoa huduma ya kuhifadhi akiba ya wanyonge na kutoa mikopo nafuu kwa wananchi wa kawaida wa DRC wanaotaka kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini wa hali na kipato. Benki hii pia inatoa huduma ya ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi wa serikali pamoja na huduma ya fedha. Uzinduzi rasmi wa Benki ya Mnyonge nchini DRC, umehudhuriwa na  Maaskofu kadhaa nchini DRC na kwamba, lengo na wajibu wa Benki hii ni kuwasaidia wanyonge nchini DRC kupambana na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.