2016-06-26 09:54:00

Waamini tunzeni kumbu kumbu, matumaini, imani na huruma!


Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wananchi wa Armenia kujikita katika mchakato wa upatanisho wa dhati, ili kukuza na kudumisha haki, amani na msamaha wa kweli, tayari kuanza kuandika kurasa mpya za matumaini kwa wananchi wa Armenia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 25 Juni 2016 ametembelea na kusali kimya kwenye Ukumbi wa kumbu kumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Waarmenia.

Baba Mtakatifu ametia sahihi kwenye kitabu cha watu mashuhuri ili kuonesha mshikamano wake wa dhati na wote walioguswa na kutikiswa na mauaji haya ya kimbari, kwa matumaini kwamba, wataweza kuwa na ari, moyo mkuu na matumaini ya kujenga msingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa. Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye mji wa Gyumri, amewakumbuka na kuwaombea wahanga wa tetemeko la ardhi lililosababisha watu zaidi ya 25, 000 kupoteza maisha katika mji mmoja tu. Ni tetemeko ambalo lilisababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na waamini wa madhehebu mbali mbali, kielelezo cha umoja na mshikamano katika mambo makuu. Baba Mtakatifu ndiye aliyekuwa kiongozi wa Ibada, lakini pia wakuu wa Makanisa ya Kikristo pamoja na Maaskofu kadhaa wamehudhuria, kielelezo cha furaha ya maisha ya kiroho miongoni mwa wafuasi wa Kristo! Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kudumisha kumbu kumbu katika maisha ya Kikristo, ili kuwa na matumaini kwa siku za usoni; zawadi ya imani na huruma ya Mungu, mambo ambayo ni utajiri mkubwa katika Mapokeo ya familia ya Mungu nchini Armenia.

Padre Lombardi anasema, imefurahisha kuona kwamba, Patriaki Karekin II wakiwa pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakitembea na kuwabariki waamini katika umoja wao. Haya ni mambo ya kawaida, lakini yanaonesha moyo wa ukarimu,  umoja na udugu. Waamini wa Kanisa Katoliki ni kundi dogo sana nchini Armenia, lakini Baba Mtakatifu amewakusanya watu wengi kutoka ndani na nje ya Armenia ili kushiriki tukio hili la kihistoria. Hii ni karama ya pekee kabisa ya Baba Mtakatifu katika  ujenzi wa madaraja ya kukutana na watu. Baba Mtakatifu kwa kuzungumzia mauaji ya kimbari pasi na woga, ni tukio ambalo limewagusa wananchi wengi wa Armenia na kuonja ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko katika mahangaiko na matumaini yao kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.