2016-06-26 08:40:00

Papa Francisko nchini Armenia: Majadiliano ya Kiekumene na Amani!


Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican anafafanua kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia kwa siku ya Jumamosi, tarehe 25 Juni 2016 ilijikita katika mambo makuu mawili: majadiliano ya kiekumene na amani. Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Armenia na popote pale ilipo kuwa kweli ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho; tayari kuwashirikisha wengine uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya Kikristo hata katika shida na madhulumu.

Huu ndio msingi wa upatanisho wa kweli na majadiliano ya kina yanayofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Hakuna nafasi tena ya kulipizana kisasi, bali kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa kuonesha ujasiri wa kushinda kishawishi hiki katika maisha, tayari kuwa ni manabii na wajumbe wa amani duniani. Matatizo, changamoto na fursa mbali mbali hazipelei katika maisha ya wananchi wa Armenia mintarafu haki, amani na upatanisho. Mfano eneo la Nagorno- Karabakh linakabiliwa na mpasuko pamoja na kinzani za kijamii, kumbe, changamoto ya majadiliano ni kukuza na kudumisha amani inayopaswa kufanyiwa kazi bila kuchelewa hata kidogo.

Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Sala ya Kuombea Amani huko Yerevan, ameitaka familia ya Mungu nchini Armenia kuiga mfano wa Mababa wa imani na Mapokeo kutoka nchini humo ili kuambata kwa kina zaidi mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kujenga umoja wa Wakristo. Kati yao ni Mtakatifu Nerses, moja wa Mapatriaki kutoka Armenia pamoja na Mtakatifu Gregori wa Narek, Mwalimu wa Kanisa aliyejikita zaidi na zaidi katika mchakato wa kutafuta amani na utulivu kwa wananchi wa Armenia.

Padre Lombardi anakaza kusema, mshikamano wa upendo na udugu; ukarimu na ujirani mwema kutoka kwa Baba Mtakatofu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Armenia ni chachu ya matumaini na nguzo thabiti katika mchakato wa ujenzi wa madaraja ya upatanisho. Hapa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua madhara ya dhambi pamoja na changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ujenzi wa amani inayofumbatwa katika: uelewano mwema, majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho na uwezo wa kusamehe na kusahau.

Padre Lombardi anasema, Jumamosi imekuwa ni siku ambayo itaacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi nchini Armenia kwani wameshuhudia Uekumene wa huduma, upendo na mshikamano kati ya viongozi wa Kanisa waliobariki, wakapanda na kumwagilia mti, alama ya matumaini na maisha mapya. Baba Mtakatifu amepewa zawadi ya mashua ya watoto waliokuwa wanaitumia kama kielelezo cha usalama na maisha ya amani na utulivu; majadiliano na udugu kati ya binadamu.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa kutembelea nyumba ya watawa wa Bikira Maria wa Armenia, ili kuwaonjesha wagonjwa na wazee, walemavu na watoto yatima huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna maelfu ya watoto waliopoteza maisha yao wakati wa mauaji ya kimbari na wengine wengi walibaki yatima. Wote hawa wamekumbukwa na kuombewa na Baba Mtakatifu Francisko ili waweze kupata ari na mwamko mpya katika maisha. Baba Mtakatifu amepata bahati ya kukutana na wahanga waliosalimika mauaji ya kimbari kwa kupata hifadhi kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, iliyoko mjini Roma baada ya Papa Benedikto wa kumi na tano kuwaonea huruma na upendo.

Na Padre Richard A.  Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.