2016-06-26 15:44:00

Papa Francisko Armenia: Tamko la viongozi wa Makanisa


Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Karekin II wa Kanisa la Kitume la Armenia Jumapili tarehe 26 Juni 2016, wametia sahihi kwenye Tamko la Pamoja kwa kumshukuru Mungu kutokana na uhusiano mwema wa imani na upendo unaoendelea kujengeka kati ya Makanisa haya mawili kama mashuhuda amini wa Injili ya wokovu inayopania kuleta faraja na matumaini katika ulimwengu mamboleo unaokabiliwa na kinzani nyingi. Viongozi hawa wanaimba utenzi wa sifa na shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima ataendelea kuwa msimamizi na wokovu wao.

Kunako mwaka 2001, Kanisa la Kitume nchini Armenia wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1700 tangu nchi hiyo ilipotangaza Ukristo kuwa ni dini rasmi ya Armenia, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Armenia, akawa ni shuhuda wa kurasa mpya za ushuhuda wa uhusiano wa kidugu kati ya Kanisa la Kitume la Armenia na Kanisa Katoliki. Wanamshukuru Mungu pia kwa kuwawezesha kunako tarehe 12 Aprili 2015, kushiriki pamoja katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, maadhimisho ya Liturujia kwa kupinga kwa nguvu mifumo yote ya ubaguzi na dhuluma pamoja na kufanya kumbu kumbu ya Tamko la Pamoja kati ya Papa Yohane Paulo II na Patriaki Karekin II kuhusu mauaji ya kimbari yaliyojitokeza mwanzoni mwa karne ya 20, tamko ambalo lilitiwa sahihi kunako tarehe 27 Septemba 2001.

Viongozi hawa wanamshukuru Mungu kwa imani miongoni mwa Wakristo nchini Armenia ambayo inaendelea kung’ara na kubeba dhamana ya moyo wa udugu na ushirikiano kati ya Makanisa, kwa kuendelea kuwaenzi Wakristo katika mchakato wa wa ujenzi wa ulimwengu unaofumbatwa katika mshikamano, haki na amani. Wanasikitika kusema kwamba, mbele ya macho yao wanaendelea kushuhudia mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wananchi wasiokuwa na makazi maalum au wale ambao wamelazimika kukimbilia uhamishoni kutokana na kinzani za kikabila, kidini na kisiasa pamoja na hali ngumu ya kiuchumi huko Mashariki ya Kati na sehemu mbali mbali za dunia.

Kutokana na mwelekeo huu, waamini pamoja na makundi ya makabila madogo madogo wamekuwa ni walengwa wakuu wa madhulumu na nyanyaso za kidini, kiasi kwamba, mateso ya kidini yamekuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku. Huu ndio Uekumene wa damu unaovuka mipaka ya utengano wa kihistoria kati ya Wakristo na kuwahamasisha kujenga umoja wa wafuasi wa Kristo! Viongozi hawa wa Makanisa wanasali kwa watakatifu na mitume Petro na Paulo; Thaddeus na Bartolomeo, kusaidia kubadili nyoyo za watu wanaosababisha dhuluma na nyanyaso pamoja na viongozi wenye dhamana kuhakikisha kwamba, wanasitisha dhuluma hizi.

Wanawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza kilio cha watu wanaotafuta haki na amani; kuheshimu haki zao msingi na kwamba, wanahitaji chakula na wala si bunduki. Wanasikitika kuona jinsi ambavyo tunu msingi za maisha ya kiroho zinazotekelezwa kwa njia ya misimamo mikali ya kiimani, hali inayotaka kuhalalisha kuenea kwa chuki, ubaguzi, dhuluma na nyanyaso. Uhalalishaji wa matendo haya kwa misingi ya kidini ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo, kwani Mungu si chanzo cha vurugu bali chemchemi ya amani. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuheshimu tofauti za kidini na kikabila zinazojitokeza ndani ya jamii changamoto na mwaliko wa kujikita katika mchakato wa upatanisho na amani. Ni matumaini ya viongozi wa Makanisa kwamba, suluhu ya amani itaweza kupatikana katika mgogoro wa sasa huko Nagorno- Karabakh.

Viongozi hawa wakiwa wameguswa kwa namna ya pekee na changamoto za kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili, wanawaalika waamini wa Makanisa yote kufungua nyoyo na mikono yao kwa ajili ya waathirika wa vita na vitendo vya kigaidi; wakimbizi na wahamiaji pamoja na familia zao, ili kuwaonesha utu, mshikamano, huruma na ukarimu. Wanapongeza juhudi zote ambazo hadi sasa zimefanyika kwa ajili ya  kuwahudumia maskini na wahitaji zaidi lakini wanasema, bado viongozi wa kisiasa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wao wanapaswa kuhakikisha kwamba, watu wanaishi katika amani na usalama; wanaheshimu na kuzingatia utawala wa sheria; waamini wa dini na makundi ya kikabila yalindwe pamoja na kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu na magendo.

Viongozi hawa wa Makanisa wanakaza kusema katika Tamko lao kwamba, ukanimungu unaojionesha kwa kiasi kikubwa katika jamii ya watu unataka kuwapoka watu tunu msingi za maisha ya kiroho na Kimungu, kiasi cha kuwatumbukiza watu kwenye mwono potofu wa binadamu na familia ya binadamu na matokeo yake ni kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia katika nchi nyingi duniani. Makanisa haya yanashirikiana na kutambua kwa dhati kuhusu mwono wa familia unaojikita katika ndoa kati ya bwana na bibi.

Viongozi wa Makanisa katika hija yao ya majadiliano ya kiekumene wametambua kwamba, kuna mambo mengi yanayowaunganisha zaidi kuliko yale yanayowatenga kama inavyojionesha katika utashi wa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja. Majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kitume la Armenia yameingia katika awamu mpya kwa kujikita katika sala pamoja na kusimama kidete ili kukabiliana na changamoto za maisha. Makanisa haya kwa sasa yanataka kuimarisha uhusiano huu wa kiekumene si tu katika masuala ya kitaalimungu, bali pia katika sala na ushirikiano wa dhati katika Jumuiya mahalia kama kielelezo makini cha ushuhuda wa umoja wa Wakristo.

Makanisa haya mawili yataendelea kushikamana kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa haki, amani na mshikamano, kwa kufumbata njia ya upatanisho na udugu ambayo iko mbele yao. Viongozi hawa wanahitimisha tamko lao la pamoja kwa kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu ili asaidie ujenzi wa upendo na umoja kati ya Makanisa haya mawili. Wanawaalika waamini wao kujiunga pamoja nao katika kumshukuru Mungu pamoja na kundi zima la Manabii, wafiadini, watakatifu na mashuhuda wote wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.