2016-06-25 11:03:00

Mauaji ya kimbari ni changamoto ya kujikita katika ujenzi wa amani!


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hotuba yake kwa viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchini zao Armenia, Ijumaa, tarehe 24 Juni 2016 ametua neno “mauaji ya kimbari” ili kukumbuka madonda ya muaji haya, ili kuweza kuyaganga na kuyaponya, na wala siyo kuyafunua na kuyaacha wazi; bali hii ni kumbu kubu hai inayopania kukoleza mchakato wa upatanisho nchini Armenia.

Padre Lombardi anasema, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kitume la Armenia; uhusiano ambao unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili; mchakato ambao ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ulioendelezwa kwa namna ya pekee na Mwenyeheri Paulo VI na Patriaki Vasken wa kwanza. Hapa kuna uekumene unaojikita katika uhalisia wa maisha ya waamini. Baba Mtakatifu Francisko amepata nafasi ya kwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Etchmiadzin, mahali ambako Kanisa limejengwa kwa maelekezo ya Mtakatifu Gregori mwangavu.

Baada ya shughuli za kutwa nzima, Ijumaa jioni, Baba Mtakatifu aliweza kuzungumza na mwenyeji wake Patriaki Karekin wa pili pamoja na Maaskofu 40 kutoka katika Kanisa la Kitume la Armena, kielelezo cha majadiliano ya kiekumene yenye mwelekeo sahihi, kwa matumaini kwamba, iko siku kwa baraka za Mwenyezi Mungu Makanisa haya yataweza kufikia umoja kamili kadiri ya mpango wa Mungu sanjari na kuadhimisha pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Padre Lombardi anasema familia ya Mungu nchini Armenia ina watu wengi pamoja na utajiri mkubwa wa imani na Mapokeo ya Kanisa, lakini daima imejikuta ikiogelea katika kinzani na mipasuko ya kijamii, kiasi cha kuwafanya watoto wake wengi kukimbilia uhamishoni. Kuna maelfu ya watu waliuwawa kikatili na wale waliosalimika waliamua kwenda kuishi uhamishoni kama wakimbizi na wahamiaji, lakini wakaendeleza imani na mapokeo yao kama Wakristo. Uwepo na utambulisho wao wa kitaifa unajikita katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuyasadaka maisha yao kama alama ya ushuhuda wa imani.

Mauaji ya kimbari kama yanayovujulikana nchini Armenia ”Metz Yeghèrn” ni tukio muhimu sana katika historia na maisha ya wananchi wa Armenia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2015 ameadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu mauaji haya yalipotokea, tukio ambalo liliwashirikisha viongozi wa Kanisa, Serikali na waamini wa kawaida kutoka katika Kanisa la Armenia. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 25 Juni 2016 ametembelea katika eneo hili ili kutoa heshima zake za dhati kwa watu waliopoteza maisha yao kutokana na mauaji ya kimbari.

Lengo kuu hapa anasema Padre Lombardi ni wananchi wa Armenia kujifunza historia yao, kutubu na kumwongokea Mungu pale walipokosea kama binadamu, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa historia na maisha yao unaojikita katika misingi ya amani na upatanisho wa kweli. Ni kumbu kumbu inayolenga kuganga, kuponya na kuvuka  madonda ya chuki na kinzani za kijamii.

Hapa familia ya Mungu inahamasishwa kusafisha kumbu kumbu na dhamiri zao, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha unaojikita katika amani, ili kutorudia tena makosa yaliyopita. Baba Mtakatifu Francisko anapofanya kumbu kumbu ya mauaji ya kimbari huko Armenia, anawakumbuka pia watu waliouwawa kikatili nchini Burundi, Barani Afrika kama ilivyokuwa pia kwa huko Bosnia na bado kuna mauaji ya kimbari yanaendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbu kumbu ya mateso n amahangaiko ya watu waliopita, ili kujenga na kuimarisha amani kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.