2016-06-24 15:56:00

Rais Mattarella hii ni hija ya kihistoria inayopania kukuza amani!


Rais Sergio Mattarella wa Italia amemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa shukrani na matashi mema wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Armenia. Anasema, Italia na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, inafuatilia kwa karibu sana hija hii ya kitume ambayo ni sehemu ya kwanza ya hija itakayofanyika pia huko Georgia na Azerbaijan, mwezi Septemba 2016. Ni matukio ambayo yana umuhimu wa pekee kihistoria na katika kukuza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kuimarisha msingi wa haki, amani na upatanisho kati ya watu.

Rais Mattarella anakaza kusema, uwepo wa Baba Mtakatifu nchini Armenia wakati huu wa hija yake ya kitume ni kielelezo cha ujumbe wa amani na mshikamano katika eneo zima la Caucaso; eneo ambalo Italia inaliangalia kwa matumaini makubwa licha ya kuitia shime Jumuiya ya Wakristo huko Armenia. Rais Mattarella anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa ujasiri huu wa kitume!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema kwamba, anakwenda nchini Armenia ili kujichotea hekima, kuwaimarisha ndugu zake katika imani pamoja na kuenzi juhudi za udumishaji wa haki na upatanisho. Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wa Italia, ustawi na maendeleo pamoja na kuendelea kuonesha mshikamano, huku wakiwa na matumaini kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.