2016-06-24 09:22:00

Papa Francisko anakwenda Armenia ili kujichotea hekima ya wahenga!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Armenia wakati wa hija yake ya kumi na nne ya kimataifa, Ijumaa, 24 Juni 2016 ametuma salam na matashi mema kwa wakuu wa Nchi ya Italia, Croazia, Bosnia-Erzegovina, Montenegro, Serbia, Bulgaria Uturuki na hatimaye, Armenia. Baba Mtakatifu Francisko amemwambia Rais Sergio Mattarella wa Italia kwamba, anakwenda nchini Armenia ili kujichotea hekima ya wahenga wa Armenia, kuwaimarisha ndugu zake katika imani pamoja na kuenzi juhudi za udumishaji wa haki na upatanisho. Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wa Italia, ustawi na maendeleo pamoja na kuendelea kuonesha mshikamano, huku wakiwa na matumaini kwa siku za usoni.

Viongozi wengine wote hawa, Baba Mtakatifu amewatakia amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nchi zao na kwamba, anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea katika sala na sadaka yake. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa nchini Armenia kuanzia tarehe 24 – 26 Juni 2016. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Kutembelea nchi ya kwanza ya Kikristo”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.