2016-06-24 15:43:00

Papa Francisko ajikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria!


Hija ya kitume kwa nchi ya kwanza ya Kikristo ndiyo kauli mbiu inayoongoza safari ya kumi na nne ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa, kuanzia tarehe 24- 26 Juni 2016 huko Armenia ambako Baba Mtakatifu Francisko amekwenda kujichotea hekima, kuwaimarisha ndugu zake katika imani na kusaidia kukoleza mchakato wa amani na upatanisho miongoni mwa familia ya Mungu nchini Armenia.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, kama ilivyo desturi kwa Baba Mtakatifu Francisko kwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mjini Roma, Alhamisi, tarehe 23 Juni 2016, Baba Mtakatifu majira ya jioni alikwenda kusali na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji wakati wa hija yake ya kitume nchini Armenia. Shada la maua lililowekwa na Baba Mtakatifu Francisko chini ya sanamu hii lilikuwa na rangi za bendera ya Armenia.

Wachunguzi wa mambo wanasema, Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma ni kati ya Makanisa ambayo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameyatembelea mara nyingi zaidi kwa ajili ya sala ya binafsi: kuomba na kushukuru kila wakati anapoadhimisha matukio makuu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.