2016-06-23 06:54:00

Ninakuja kati yenu kama mhudumu wa Injili na mjumbe wa amani!


Baba Mtakatifu Francisko anaialika familia ya Mungu nchini Armenia kusali kwa ajili ya kuombea hija yake ya kitume kwa nchi ya kwanza ya Kikristo hususan katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili waweze kujichotea hekima na busara kutoka kwa wahenga wao, ili hata yeye pia aweze kuchota imani kutoka katika chemchemi ya maisha yao yaliyochongwa kwenye mwamba thabiti.

Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video alioutuma kwa familia ya Mungu nchini Armenia, anapojiandaa kuanza hija yake ya kumi na nne ya kimataifa nchini humo kuanzia tarehe 24- 26 Juni 2016. Anasema, anakwenda kwao kama ndugu yao anayependa kuona nyuso zao, ili kusali na kushirikishana zawadi ya urafiki. Anaendelea kusema, historia ya Armenia inaamsha ndani mwake mvuto mubwa na machungu: mvuto kwa sababu wameweza kujipatia nguvu ya kuamka tena kutoka katika Fumbo la Msalaba,  hata pale walipokumbana na mateso makubwa yanayokumbukwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Machungu kwa maafa makubwa ambayo wazee wao walikabiliana nayo katika maisha yao. Haya ni matukio ambayo hayawezi kufichika katika sakafu ya nyoyo za watu na kwamba, katika hali na mazingira haya, kamwe wasikate tamaa. Baba Mtakatifu anaialika familia ya Mungu nchini Armenia kutenda kama Nuhu ambaye licha ya gharika kuu, lakini hakuchoka kutazama juu angani, huku akimwachilia njiwa kuruka hadi pale siku moja njiwa aliporejea akiwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, hizi zilikuwa ni dalili kwamba, maisha yangeweza kuanza tena na matumaini kuchipua kama mti wa mtende. Anaendelea kukaza akisema, kama Mhudumu wa Injili na Mjumbe wa amani anatamani kuwaendea, ili kuenzi kila jitihada zinazopania kukuza na kudumisha amani, kushirikiana pamoja nao katika mchakato wa upatanisho unaobubujisha matumaini.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea na kuwaweka wananchi wote wa Armenia chini ya ulinzi na maombezi ya watakatifu wao, lakini zaidi ya Mtakatifu Gregori wa Narek, Mwalimu wa Kanisa. Wote hawa wasaidie kubariki mikutano yao ambayo Baba Mtakatifu mwenyewe anaithamini sana. Anatamani kukutana na kukumbatiana na Patriaki Karekin wa II, ili wote kwa pamoja waweze kuleta ari na mwamko mpya katika majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo! Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mwaka 2015 wananchi wengi kutoka Armenia walifika mjini Roma na kusali pamoja naye, lakini wakati huu anakwenda nchini mwao ili kuimarisha umoja na kukuza njia ya upatanisho unaojikita katika matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.