2016-06-22 09:12:00

Dini na wajibu wa utunzaji bora wa mazingira


Askofu Marcello Sànchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi anasema, kuna haja kwa dini mbali mbali kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote. Askofu Sorondo ameyasema haya Jumatatu, tarehe 20 Juni 2016 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira lililofanyika huko Torreciudad nchini Hispania.

Askofu Sorondo anasema utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unaweza kuwa ni sehemu ya mkakati wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuziwezesha dini na waamini wao kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya kimaadili na kijamii. Utunzaji bora wa mazingira inaweza kuwa ni kazi ya pamoja kati ya waamini wa dini mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Laudato si, ametoa mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, ili iweze kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora kama sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini, maradhi, vita na mipasuko ya kijamii. Dhana ya ekolojia inapaswa kufahamika katika mapana yake, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali, kiasi cha kunyanyasa utu na heshima ya binadamu anayeendelea kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Askofu Marcello Sànchez Sorondo anahitimisha hotuba yake elekezi kwa wajumbe wa Kongamano la Kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kusema kwamba, kuna haja kwa sayansi kushirikiana kikamilifu na dini, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo kwa sasa inatishia usalama, amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.