2016-06-21 10:36:00

Tanzania yazindua matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi, mtoto na malaria!


Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Dr. Mpoki M. Ulisubisya, Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika uzinduzi wa matokeo muhimu ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto pamoja na Malaria nchini Tanzania kwa Mwaka 2015- 2016 (TDHS- MIS), uliofanyika tarehe 20 Juni 2016 kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Ndugu Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshuru Mungu kutumia fursa hii kuwashukuru wote kwa kuitikia mwaliko na kuungana na Wizara yangu kwa lengo la kuzindua Matokeo Muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2015, yaani "2015-16 Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey".  Aidha, napenda niwashukuru waandaaji wa hafla hii kwa kunialika kufanya uzinduzi wa tukio hili muhimu. Kama mnavyofahamu, Sekta ya Afya ni miongoni mwa Sekta muhimu sana katika jamii yetu katika kuchangia uboreshaji wa uchumi wa Nchi na kupunguza Umaskini. Ni dhahiri kuwa, ukiwa na taarifa sahihi za afya za Wananchi, ni fursa ya pekee ya kuboresha na kuimarisha ustawi wa uchumi wa Taifa letu.

 Ndugu Mwenyekiti, kutokana na matokeo ya utafiti huu tunapata takwimu za kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali katika kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo yale ya Kitaifa na Kimataifa.  Taarifa hizi zitaisadia Wizara yangu, watunga sera, waratibu wa miradi na wadau wengine katika kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi iliyopo, na kujua miradi ipi inatekelezeka na ipi ambayo bado ina changamoto ili pale inapobidi tujiandae upya na kuainisha mikakati mipya kuhusiana na taarifa za Sekta ya afya hapa Nchini.

Ndugu Mwenyekiti, binafsi nimepata wasaa wa kuipitia Ripoti ya Matokeo Muhimu ya Utafiti huu na kutokana na nilichosoma, naweza kusema kuwa, kuna mambo mengi katika matokeo haya ambayo tunaweza kupongezana kwayo. Lakini pia kuna maeneo ambayo bado kuna changamoto na hivyo tunahitaji kujitathmini.  Kwa mfano, maeneo tuliyofanya vizuri ni:  Kuendelea kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, yaani chini ya mwaka mmoja kutoka vifo 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai katika Utafiti wa mwaka 2010 kufikia vifo 43 mwaka 2015/16.  Kuendelea kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 81 mwaka 2010 na kufikia vifo 67 mwaka 2015.

Kupungua kwa vifo hivi kumewezesha serikali kutimiza lengo la Nne (4) katika yaliyokuwa Malengo ya Millenia ya 2015:  utafiti huu umetuonyesha kuongezeka kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo kiwango cha utumiaji wa njia za uzazi kwa wanawake walio kwenye ndoa au wanaoishi na wenza wao kimefikia asilimia 38 kutoka asilimia 29 Mwaka 2010.  Asilimia 32 ya wanawake hawa katika utafiti huu wa 2015/16 wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango na asilimia 6 wanatumia njia za asili mwaka 2010. Ongezeko la matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni dalili nzuri inayoashiria uwezekano wa kushuka kwa kiwango cha uzazi pamoja na kuongezeka nafasi ya uzazi kati ya watoto.

Taarifa nyingine ambazo zimetokana na juhudi za makusudi za Serikali ni kiwango kikubwa cha akina mama wajawazito wanaohudhuria kliniki na kuhudumiwa na mtaalamu aliyesomea (asilimia 98):  Kuongezeka kwa kiwango cha akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya, kutoka asilimia 51 mwaka 2010 kufikia asilimia 60 mwaka 2015 na kuongezeka kwa kiwango cha akina mama wanaosaidiwa na wataalam waliosomea wakati wa kujifungua kutoka asilimia 50 kufikia asilimia 60 mwaka 20015/16.  Matokeo mengine muhimu ni kupungua kwa kiwango cha watoto waliodumaa kutoka asilimia 42 ya watoto walio chini ya miaka mitano katika Utafiti wa mwaka 2010 na kufikia asilimia 34 kwa mwaka 2015/16.

Ndugu Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa matokeo niliyoyataja yanatokana na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuwaletea Wananchi huduma bora za afya na zilizo karibu na maeneo wanayoishi na ikichangiwa na mpango wa Serikali katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na Zahanati kila Kijiji na Kituo cha Afya kila Kata.  Kama mtakumbuka vyema, matokeo ya Utafiti wa Kutathmini Utoaji wa Huduma za Afya Nchini (Tanzania Srvice Provision Assessment Survey TSPA) uliofanyika mwaka 2014/15 yalionesha kuongezeka kwa upatikanaji na utoaji wa huduma mbali mbali za afya ikiwemo huduma kwa matibabu ya watoto na kuongezeka kwa vituo vinavyotoa huduma za uzazi wa mpango.

Kwa huduma za kisasa za uzazi wa mpango ilionekana kuwa asilimia 80 ya vituo vyote vinavyotoa huduma za afya vinatoa huduma hii ya Uzazi wa Mpango. Kwa upande wa huduma zinazohusiana na Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto, matokeo yalionesha kuwa asilimia 85 ya vituo vyote vinatoa huduma zinazohusiana na Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto.

Ndugu Mwenyekiti, pamoja na matokeo haya mazuri, Utafiti umeonesha kuwa kuna baadhi ya maeneo yanapaswa kuangaliwa upya na kutiliwa mkazo zaidi. Kwa mfano:- kupitia Utafiti huu tunaona kuwa kwa sasa wanawake Nchini Tanzania wanazaa wastani wa watoto watano (5) katika vipindi vyao vya uzazi. Kwa kweli kiwango hiki bado ni kikubwa.  Wastani wanawake wa vijijini huzaa watoto wawili zaidi ya wanawake wanaoishi mijini. Yaani watoto Sita kwa wanawake wa vijijini na watoto Wanne kwa Wanawake wa Vijijini.

Bado juhudi zaidi za Serikali na wadau wengine zinahitajika hasa maeneo ya vijijini ili kuweza kuondoa tishio la ongezeko kubwa la watu hapo baadae. Katika matokeo haya pia tunaona ongezeko la mimba kwa wasichana wadogo. Utafiti wa 2015/16 umeonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana wa miaka 15-19 wameshaanza kuzaa, hii ikiwa imeongezeka kutoka asilimia 23 katika Utafiti wa mwaka 2010. Hii sio taarifa nzuri kwani inatishia kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaokatisha masomo na hivyo kuongezeka kwa umaskini. Aidha watoto ambao huzaliwa na wasichana hawa wadogo wana uwezekano mkubwa kupoteza maisha ukilinganisha na wengine. Hivyo, bado tunahitajika kutoa elimu zaidi ili kupunguza kiwango hiki na kuwezesha watoto wetu wa kike waweze kupata muda wa kusoma na kujiendeleza katika kujiandaa na maisha. Hivyo Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa wasichana kuzaa wakiwa bado wadogo. Aidha, serikali in ania ya makusudi ya kuhakikisha Sheria na Ndoa inafanyiwa marejeo ili kuhakikisha baadhi ya changamoto hizo zinashughilikiwa.

Ndugu Mwenyekiti, utafiti huu pia uliangalia kiwango cha maambukizi ya Malaria kwa watoto chini ya mwaka mmoja, na wote tunatambua kuwa Malaria bado ni mojawapo ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo Tanzania na inachangia pia asilimia kubwa ya vifo vya watoto na akina mama wajawazito.  Utafiti huu unaonyesha kuwa asilimia 14 ya watoto wa chini ya miaka 5 ambao walipimwa Malaria kwa kutumia kipimo cha kutoa matokeo kwa haraka yaani Rapid Diagnostic Tests (RDT) walikuwa na Malaria. Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango kilichopatikana wakati wa Utafiti wa UKIMWI na Malaria wa Mwaka 2011-12.

Japokuwa yawezekana ongezeko hili linatokana na vipindi tofauti vya kufanya utafiti katika tafiti hizi mbili, bado hatuwezi kukwepa ukweli kuwa Malaria bado ni tishio kwa watoto wetu na Wananchi kwa ujumla.  Hivyo nitoe rai kwa wenzangu katika Serikali na wadau wetu wa Maendeleo kuwa bado tunapaswa kuendelea na juhudi zilizopo za kuhakikisha Malaria inamalizwa hapa Tanzania.  Natambua Mpango wa Kudhibiti Malaria Tanzania (NMCP) upo katika utekelezaji wa awamu ingine ya kusambaza vyandarua katika Kaya za Tanzania, na ni mategemeo yangu kuwa vitatumiwa kama ilivyokubaliwa tunategemea juhudi hizi na nyingine zinazofanywa na wadau wengine zitachangia kupunguza kiwango cha Malaria.  Hata hivyo mapambano dhidi ya malaria ni ya kila mmoja wetu, kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kutekeleza ushauri wa wataalam ili kujiepusha na kupata Malaria mfano matumizi ya vyandarua vyenye dawa, kukata majani na kuzuia madimbwi ya maji kwenye makazi yetu.

Ndugu Mwenyekiti, nimegusia tu baadhi ya viashiria lakini natambua kuwa hali halisi ya viashiria muhimu vya afya kutoka katika ripoti hii itawasilishwa na watoa mada walioandaliwa hapo baadae kidogo na pia mtaweza kusoma katika ripoti ambayo nimetaarifiwa mtapewa hivi punde. Hivyo, niwaombe msikilize vizuri mada hizo na pale ambapo mtaona kunahitajika uchambuzi wa namna ya kipekee basi msisite kutoa taarifa kwa wahusika na hii itachangia katika kuboresha taarifa ya kina ya hapo baadae mwezi Oktoba 2016.

Ndugu Mwenyekiti, Utafiti huu, kama zilivyo tafiti nyingine nyingi unatupatia matokeo muhimu ambayo yanaakisi hali halisi ilivyo katika mfumo wetu mzima wa afya. Ni jukumu letu sote kama wadau kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo yetu ya kazi. Kwa mantiki hiyo, napenda nitoe wito kwa Wadau wote wa Sekta ya Afya Nchini na Wadau wote kwa ujumla kuyachukulia matokeo haya kama chachu ya kitaifa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya Nchini.  Wananchi pia watimize wajibu wao kwa mfano akina mama kunyonyesha watoto kama inavyoshauriwa, kwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua, n.k. Kwa kuelewa hayo tunatakiwa sote kufanya kazi kwa pamoja na kwenda sambamba na kauli mbiu ya awamu ya Tano ya HAPA KAZI TU ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuboresha huduma za afya na maisha kwa ujumla. Niombe kuwa sote kwa pamoja kutumia takwimu hizi ambazo ni rasmi kwa ajili ya kupanga sera na mipango bora.

Ndugu Mwenyekiti, kabla ya kufikia tamati, napenda kutambua michango mbalimbali iliyowezesha kukamilika kwa utafiti huu. Nianze kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kufanya Utafiti huu. Pili, kuwashukuru wataalam kutoka Wizara zote zilizoshiriki, waratibu, wasimamizi, wadadisi na Wananchi kwa ujumla kwa kuwezesha kufanyika kwa kazi hii.

Tatu, napenda kutambua juhudi zilizofanyika chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Afya - Zanzibar:  Wataalam kutoka Shirika la Macro la Marekani, na pia niwashukuru Shirika la  Misaada la Marekani (USAID),  Idara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo (Glabal Affairs Canada),  Ubalozi wa Ireland, Shirika la Umoja wa Mataifa linahusika na idadi ya watu (UNFPA),  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Watoto (UNICEF) kwa kutoa msaada wa fedha zilizotumika kutekeleza utafiti huu  wadau wengine wa afya kwa kutoa raslimali fedha na wataalam na ufuatiliaji mzima wa utafiti huu. Niwashukuru pia Wananchi waliofikiwa na wataalam na kutoa taarifa za Utafiti huu na tunaomba muendelee na moyo huu kwani takwimu hizi zinasaidia Serikali katika kuwaletea wananchi huduma za afya na ustawi wa maisha ujumla.

 Ndugu Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kwa mara nyingine kutoa wito kwa wadau wote kuwa dhana hasi iliyojengeka kwenye jamii kuhusu matumizi ya takwimu kwamba Serikali ndio inayotumia takwimu tuifute na naomba kwamba wadau wote wa Afya tutumie takwimu hizi ili tuboreshe huduma zaidi na kuongeza uchumi wa Nchi. Vitabu hivi vitumike ipasavyo, visiviweke kwenye makabati ya vitabu. Visomwe kwa makini na kuchambua kwa kina ili kupata majibu ya kukabiliana na changamoto zilizopo za upatikanaji wa taarifa za afya. Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na wadau wengine tutafanya kila linalowezekana ili kumaliza uchambuzi wa kina wa taarifa za Utafiti huu ikiwemo taarifa kuhusiana na Vifo vinavyotokana na uzazi, na kuzitoa hapo mwezi Oktoba 2016 kama ilivyoelezwa awali.

 Baada ya maelezo hayo, napenda kutamka rasmi kuwa, TAARIFA YA MATOKEO MUHIMU YA UTAFITI WA WA AFYA YA UZAZI NA MTOTO NA VIASHIRIA VYA MALARIA MWAKA 2015/16 IMEZINDULIWA RASMI. Niwatakieni majadiliano mema yatakayoboresha Sekta ya Afya Nchini.

Asanteni kwa Kunisikiliza.








All the contents on this site are copyrighted ©.