2016-06-21 07:12:00

Papa: Mkristo n muhimu kujipima mwenyewe kwanza kabla ya kuhukumu wengine


 Kabla ya kuwahukumu wengine, ni muhimu kwanza kutazama yako mwenyewe, kuona ni jinsi ulivyo. Baba Mtakatifu Francisko amehimiza katika homilia yake, mapema Jumatatu akiwa katika kanisa dogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican.  Hii imetajwa  kuwa  homilia yake ya mwisho,  kabla ya mapumziko ya majira ya joto barani Ulaya. Baba Mtakatifu amehimiza watu kuona tofauti kati ya  hukumu ya Mungu na hukumu ya binadamu  si tu katika uwezo wake, lakini hasa  huruma yake.

Papa aliendelea kufafanua kwamba, ni Mungu peke yake mwenye haki ya  kuhukumu. Na akaonya kama sisi tusivyopenda kuhukumiwa pia nasi tusipende kuhukumu wengine. Na kama ambavyo sisi tungependa Mungu atuhurumie wakati wa hukumu yake ya mwisho, ambamo tutamwomba Bwana autangalie kwa huruma yake, tukiomba atusamehe kwa makosa mengi tuliyoyatenda katika maisha, hivyo kumbe pale tunapohukumu wengine, Yesu anatuona kuwa ni wanafiki. Sisis tunaomba Bwana asituhukumu , lakini twahukumu wengine. 

Hivyo Papa alionya juu ya kosa la kuwahukumu wengine ,  akikumbusha kwamba, kipimo kilekile tunachotumia kuwahukumu wengine ni hichohicho atakachokitumia Bwana kutuhukumu nacho. Kumbe Bwana, anatutaka kuwa waangalifu wakati wa kuhukumu wengine kwamba ni lazima kwanza kujitazama katika kioo cha maisha.

Baba alihimiza na kuongeza kujitazama katika kioo haina maana ya kujitazama jinsi tulivyozeeka, kuyaonya makunyazi ya ngozi usoni , lakini ni kujitazama kwa jinsi tunavyoishi katika mahusiano na wengine. Ni kuyapima maisha yetu wenyewe kwanza kabla hatujaanza kutazama wengine wanaishi je, kama somo la Injili linavyosema si kuanza kutazama kibanzi kidogo kilicho katika jicho la ndugu yake na kumbe jicho letu lina boriti kubwa. Kwa jinsi gani unaweza kumwambia ndugu yako, 'Napenda kutoa kibanzi katika jicho lako,' wakati mwenyewe una boriti jicho lako boriti? Kufanya hivyo Yesu anasema huo ni unafiki, kwanza na tujisafishe kwamba dhambi zetu ili tupate kuwa safi katika kuona makosa ya wengine.

Papa alieleza na kusema, kuwahukumu wengine ni kuchukua nafasi ya Mungu. Ni kuwa kama ilivyokuwa wakati nyoka alivyowashawishi Adamu na Hawa, kula tunda hili ili upate  ufahamu zaidi, alitaka wachukue nafasi ya Mungu.  Na hivyo kwa binadamu kuhukumu wengine inakuwa ni mbaya maana inakuwa ni kuchukua nafasi ya Mungu. Ni Mungu peke yake mwenye haki ya kutuhukumu, na hufanya hivyo kwa upendo na huruma kubwa. Kumbe tunachotakiwa kufanya ni kujiepusha kuwakuhumu wengine badala yake tunapaswa kwa upendo na uelewa, kuwaombea pale tunapodhani wametenda kosa. Badala ya kuwalaumu nyuma ya migongo yao, ni kutafuta nafasi ya kuzungumza nao , si kama hakimu lakini kama rafiki. Kuhukumu wengine ni unafiki Papa amesisitiza, na kumtaka kila mmoja kukumbuka kwamba kipimo  unachotumia kuwahukumu wengine ni hichohocho kitakachotumiwa pia kutoa hukumu kwako. 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.