2016-06-21 11:57:00

Miaka 45 ya Daraja Takatifu si haba! Baba Kardinali Pengo!


Kardinali Polycarp Pengo Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 20 Juni 2016 ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 45 tangu alipopewa Daraja Takatifu la Upadre, kunako tarehe 20 Juni 1971 na Hayati Askofu Karolo Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa na kumweka wakfu tarehe 6 Januari 1984 kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Nachingwea. Mwezi Mei, 1990 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na tarehe 21 Februari 1998 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali.

Kardinali Pengo katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kukazia umuhimu wa kulitegemeza Kanisa Barani Afrika, sera na mikakati aliyoanza kuifanyia kazi mapema tu alipoingia Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kuanzisha “Sera ya Tegemeza Jimbo” Dhamana ambayo ilipaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa na familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kanisa Barani Afrika haliwezi kuendelea kutegemea ufadhili kutoka nje ya Afrika, kumbe kila mwamini anapaswa kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Kanisa Mahalia, ili kuweza kukidhi ongezeko la waamini na mahitaji ya maisha ya kiroho pamoja na changamoto za kichungaji. Kardinali Pengo anaitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajenga ari na moyo wa kimissionari ili kuweza kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali watu, vitu na fedha.

Kardinali Pengo alipoingia Jimbo kuu la Dar es Salaam kulikuwa na Parokia zisizozidi 30 na kwa kiasi kikubwa Jimbo kuu la Dar es Salaam lilitegemea huduma za kichungaji kutoka kwa Wamissionari, hususan Wakapuchini ambao walikuwa na historia kubwa ya maisha na utume wao Jimbo kuu la Dar es Salaam. Leo hii, Jimbo kuu la Dar es Salaam lina Mapadre Jimbo 71 na idadi kadhaa ya Majandokasisi wanaoendelea na majiundo yao kwenye nyumba za malezi na Seminari kuu nchini Tanzania.

Hadi tunakwenda mitamboni, Jimbo kuu la Dar Es Salaam lilikuwa na Parokia 95 pamoja na Parokia teule 5 zinazoweza kutangazwa kuwa Parokia rasmi wakati wowote. Lengo la kuanzisha Parokia hizi ni kukidhi mahitaji ya familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Kwas asa Jimbo kuu la Dar es Salaam linahudumiwa na Kardinali Pengo kama mchungaji mkuu akisaidiwa na Askofu msaidizi Euzebius Nzigilwa.

Kardinali Pengo katika mahojiano na Radio Vatican anakaza kusema, umefika wakati kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuonesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu pasi na aibu. Imani hii inapaswa kujikita katika matendo adili na matakatifu yenye mashiko na mvuto kwa watu wengi. Waamini waunganishe mateso na mahangaiko yao ya ndani na yale ya Kristo anayewafariji, kuwaponya na kuwaganga. Kamwe wasiwe ni watu wenye maisha ya ndumila kuwili, asubuhui Kanisani jioni kwa waganga wa kienyeji! Imani katika matendo ni muhimu sana katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.