2016-06-21 14:17:00

Maamuzi magumu yatolewa!


Wakati wa uchaguzi mkuu wa nchi vyama vilivyokuwa vinagombea kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi, vilikuwa vinatoa lugha ya namna yake ya kuvuta wananchi. Magazeti yalitoa taarifa za vyama mbalimbali kwa kuandika vichwa vyenye mvuto kwa wasomaji. Mathalani, “Kikao kijacho cha Chama kuja na maamuzi mazito” “Kamati Kuu ya Chama yatoa maamuzi mazito.” “Maazimio mazito ya kikao cha kamati kuu.” Lugha hiyo ilitumika pia na viongozi wakubwa. “Mzee Nanhii atoa kauli nzito kwa wananchi.” Mara zote maamuzi hayo mazito yaliwalenga wanachama wao, yaani yaliwaelekea watu wengine. Aidha hayakuwa maamuzi yanayostahili kuitwa mazito kwani yalihusu kutetea uhai wa chama au kutetea maslahi ya mtu.

Leo tutasikia maamuzi mazito anayochukua mtu ya kwenda kufa kwa ajili ya kutetea sera za upendo kamili na kuwataka watakaozipokea nao watoe maamuzi mazito ya kujitoa kutetea upendo, haki na huruma ya Mungu. Maamuzi ya Yesu ni mazito na anayapigania peke yake bila ya mashabiki wala silaha na jeshi la kumlinda wala hata bila wapambe, ambao wakati mwingine ni nuksi. Hebu tuyafuatilie maamuzi hayo na anavyotualika nasi kutoa maazito mazito ya maisha yetu. Yesu anatoa uamuzi wa kusafiri kutoka Galilea kwenda Yerusalemu kupitia Samaria. Safari hii ndiyo ya mwisho anaenda kufa; anakwenda kuyamimina maisha yake ili yawe ni fidia kwa wengi!: “ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia.” Neno hili kupaa linamaanisha kuinuliwa au kuchukuliwa angani kama alivyoinuliwa Eliya au Enoki kama tulivyosikia sikukuu ya kupaa Yesu mbinguni. Kwa hiyo Yesu atainuliwa yaani atakufa na kwenda katika ulimwengu wa Baba yake baada ya ufufuko.

Ili kuonesha uzito wa uamuzi huo wa kwenda Yerusalemu inasemwa “aliukaza uso wake kuelekea Yerusalem. Kwa lugha ya kigiriki ni esterixen tou prosopon. Katika Agano la kale maneno haya yalimhusu mtu anayechukua maamuzi mazito katika maisha. Kama ilivyokuwa kwa nabii Ezekieli alipoambiwa na Mungu atangaze kuangamizwa kwa Yerusalemu. Watu walipinga vikali uamuzi huo, lakini Mungu akamwambia  upinzani wa watu usikubabaishe na kukuogopesha “mimi nitakupa uso mgumu.” Kadhalika Nabii Isaya alisema: Sikuficha uso wangu usipigwe, nitaukaza uso wangu ili uharibiwe.  Kadhalika kwa upande wa Yesu safari hii ni lala salama; ni patashika nguo kuchanika! Kwani anaenda kukabiliana na watu ambao tungeweza kusema ni wakereketwa wa Chama tawala kinachoukandamiza ulimwengu huu.  Kwa hiyo itambidi akaze nia na kushikilia kwa dhati maamuzi ya Baba. Yesu alishakuwa na uzoefu wa kukataliwa. Ingawaje alipoanza kazi watu wengi walimshabikia kwa sababu ilikuwa ni “kipya kinyemi” lakini jinsi alivyoendelea kunadisha sera na mapendekezo yake, watu wakaanza kumwambaa hadi ikambidi kuwatahadharisha: “Ole wako Korazini! Ole wako Kafarnaum.”

Kumbe, hata sasa Yesu anaenda Yerusalemu katika mazingira haya ya kusalitiwa na hatimaye, kukataliwa. Kwa hiyo akiwa anajua hali halisi, kabla ya kuanza safari anatuma kwanza”wapambe” au wajumbe kutangulia “kutikisa kiberiti” na kuandaa mazingira kama ilivyoandikwa: “Akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake.” Neno la kigiriki lililotumika ni angelous, yaani malaika yaani ni hao wajumbe au mitume waliotumwa. Kumbe ni muhimu sana kuiandaa safari ya Yesu aweze kuingia katika jamii, katika hali halisi ya ulimwengu huu unaotakiwa ubadilike na kuwa mpya. Hao wajumbe na malaika ndiyo mitume wake, wafuasi wake, wanaweza pia kuwa makatekista, wakristu na yeyote anayemhubiri Yesu. Wajumbe hao wanaweza kuandaa vizuri au vibaya huo ujio wa Yesu katika jamii.

Kumbe kweli bwana, eti wapambe nuksi! Wajumbe waliotumwa kumtangulia, waliiandaa vibaya sana safari ya Yesu. “Wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha.” Ingawaje Yesu alikuwa na uzoefu kukataliwa kuanzia nyumbani kwake Nazareti, lakini alishangaa kukataliwa katika kijiji hiki ambacho daima walikuwa wanampokea. Hata wakati fulani wakataka abaki hapohapo wamfanye mfalme. Lakini kipindi hiki wanamkataa kwa hoja kwamba eti kwa vile “alikuwa anaenda Yerusalemu.” Hapa ni dhahiri sintofahamu hii imesababishwa na wajumbe waliotumwa pale Samaria kuandaa mapokezi. Yaonekana hao ndugu waliongeza fikra zao binafsi juu ya Yesu, yaani wakaunganisha mambo kwamba Yesu anaenda Yerusalemu na hapo atafanya kupitia tu. Kumbe, unapotamka Yerusalemu wote walijua kuwa huko ni makao makuu ya dini na serikali. Kumbe, fikra za mitume na za Waisraeli juu ya Masiha wanayemtazamia zilikuwa ni za atakayeleta ushindi wa kidunia huko Yerusalemu.

Kwa upande wao, waliona sasa Yesu ametoa maamuzi mazito ya kwenda Yerusalemu kuanzisha mapinduzi ya kuwalipiza kisasi maadui zake, kuwaletea uhuru na kuendeleza hali nzuri ya udini na ya utawala wa Waisraeli. Propaganda hizi zikawachefua Wasamaria, nao wakatoa maamuzi mazito ya kumkatalia kuingia kijijini kwao. Kwa hiyo kuonesha kuwa mitume walimwona Yesu kuwa ni masiha mshindi, shujaa, mtawala na wa kulipiza kisasi maadui wake hapo walipoona Yesu amekataliwa kumkaribisha, Yakobo na Yohane wakaja juu, wakataka kuwashika adabu na kuwaonesha cha moto kumwambia Yesu: “Bwana wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni uwaangamize [kama alivyofanya nabii Eliya]?” Mitume walitaka kuagiza moto kama alivyofanya Eliya alipoagiza moto kuangamiza maadui wake. Hii ndiyo kasoro ya kumwelewa vibaya Masiha wa kweli, daima mtu huyo anakosa uvumilivu juu ya Mungu, anakuwa na msimamo mkali wa dini, kwa sababu anajiona kuwa mtu safi. Kwa hiyo anawataka watu wote wampokee huyo Mungu kwa lazima, la sivyo waangamizwe. Kumbe, mkristo hana budi awe mwangalifu sana ajitahidi zaidi yeye mwenyewe kuishi maisha yatakiwayo bila kulazimisha wengine.

Hapo “Yesu awageukia na kuwaonya.” Kwa Kigiriki neno kuonya ni bitimao, linatumika pale tu Yesu anapowafukuza mashetani. Kumbe ndani ya mitume kuna ushetani wa kutaka kuangamiza maadui na kueneza Habari njema kwa mabavu. Ndipo Yesu anawaambia: “Hamjui ni roho ya namna gani mlio nayo. Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa.” Baada ya kukataliwa Samaria wakaondoka na kwenda kijiji kingine.  Wakiwa bado safarini tunashuhudia aina tatu ya watu wanaotakiwa watoe maamuzi mazito ya kuishi ya maisha ya Yesu kwa dhati.

Mwito wa kwanza, “mtu mmoja alimwambia, ‘Nitakufuata kokote utakakokwenda.” Haya ni maamuzi mazito sana ya maisha, yaani kufuata uchaguzi atakaofanya Yesu. Jibu la Yesu ni Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake.” Yaani, anayetoa maamuzi ya kumfuata Yesu, budi apime “vizuri unga na maji.” Yaani budi kuacha yote, kuacha miradi, kuacha utajiri, kuacha maraharaha. Kama kilivyo kiota  cha ndege, hapo ni makao, pana joto, pana utulivu na pana amani. Kwa hiyo kufuata Yesu usitegemee maisha mazuri na ya utulivu, ya kujijenga, bali ni maisha ya kuwajibika  na kushughulika. Yesu hakuwa na uhakika wa pahala pa kulala, siku nyingine alipokewa lakini pengine alikataliwa kama nyumbani kwake Nazareti na sasa Samaria. Kwa hiyo, hata mfuasi wa Yesu anaweza kupokewa au kukataliwa, maana yake unaweza kupambana na chochote kile katika maisha haya na wewe huna budi kujiandaa daima kutoa sadaka.

Mtu wa pili anaitwa na Yesu: “Nifuate” naye akasema, “Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu.” Kadiri ya utamaduni wa Waisraeli kuzika wazazi lilikuwa ni tendo azizi na tukufu. Hata sheria ya Tora iliweza kuvunjwa na kuhani ili kumruhusu kwenda kumzika mzazi wake siku ya sabato. Baba anawakilisha utamaduni, ukale na mapokeo ya familia. Kwa hiyo mtu huyu anajitetea kuwa atafika tu kumfuata Yesu pale atakapoachana na mila na desturi za wazazi wake. Yesu anatumia mwanya huohuo na kubeza mila na desturi za utamaduni potovu na kusema: “Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe endenda ukautangaza ufalme wa Mungu.” Haya ndiyo yanayoweza kumpata mkristu, yaani atapenda kusubiri hadi anastaafu kazi ndipo anaanza kufuata dini kikamilifu au mbaya zaidi kuchanganya mila na desturi za ovyo pamoja na kushika sakramenti. Yesu anasema ni budi kutoa maamuzi mazito ya kuachana na mila na mapokeo ya ovyo, kadhalika kuachana na vigezo vya ulimwengu  huu na kumfuata.

Mtu wa tatu anasema: “Bwana nitakufutata; lakini nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani kwangu.” Hapa ni tatizo jingine la kuachana na mazoea  mazuri ya zamani. Huu ndiyo ugonjwa uliowapata Waisraeli walipokuwa jangwani. Kwa vile walipambana na maisha magumu ya jangwani wakaanza kufikiria mabakuli ya nyama ya Misri. Waisraeli walikuwa wanaotea mabakuli ya nyama kumbe ukweli wa mambo walikuwa wanapewa kula vitunguu sumu. Yesu anasema: “Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu.” Yaani maisha ya kufuata Yesu ni ya maamuzi ya dhati na ya kuwajibika kwa uhakika. Kuchukua maamuzi ya kufuata Injili ya Yesu maana yake kuamua kumfuata moja kwa moja bila kurudi nyuma kwenye maisha ya awali.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.