2016-06-21 08:57:00

Kongamano la Ekaristi lilete upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa!


Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Argentina wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yamekuwa ni muda muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu ushuhuda wa maisha ya Kikristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Imekuwa ni fursa kwa waamini kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza hija inayowaelekeza kwenye utakatifu wa maisha kwa kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi; kwa kusimama katika kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Kardinali Giovanni Battista Re, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Argentina, lililohitimishwa Jumapili, tarehe 19 Juni 2016. Fumbo la Ekaristi Takatifu liwe ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa, mahali ambapo waamini wanajichotea nguvu na ari ya kuwa kweli ni mwanga na chumvi ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Kongamano hili limeadhimishwa kwenye mji wa San Miguel de Tucuman.

Kardinali Re, amewataka Wakristo kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, na kamwe wasione kigugumizi cha kumshuhudia na kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kuna haja kwa Wakristo nchini Argentina kujenga na kuimarisha imani yao katika mwamba ambao ni Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Watambue kwamba, binadamu ana kiu ya kutaka kupata: ukweli, upendo, uhuru, mshikamano, haki na amani. Kwa maneno machache Kardinali Re anasema, binadamu ana kiu ya kutaka kumwona Mwenyezi Mungu.

Ibada ya kufunga maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Argentina yamehudhuriwa na zaidi ya waamini 150, 000 kutoka sehemu mbali mbali za Argentina. Kardinali Re, amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewataka waamini kukita mizizi yao katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, huku wakiwa na matumaini kwa siku za usoni.

Mahubiri ya Kardinali Re yalijikita zaidi katika Fumbo la Ekaristi, ambamo Mwenyezi Mungu anajisadaka kwa ajili ya ustawi wa waja wake, ambao pia wanapaswa kuwa ni mkate unaomegwa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Waamini wajitahidi kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha yao, ili waweze kuandamana pamoja katika mchakato wa ushuhuda unaojikita katika matendo, tayari kushiriki kikikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.