2016-06-20 09:50:00

Waislam na Wakristo shikamaneni kuwahudumia maskini!


Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pamoja na Siku kuu ya Id al Fitri ni matukio muhimu sana ya kidini kwa waamini wa dini ya Kiislam sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kipindi cha kufunga, kusali na kutenda matenda mema; mambo ambayo yanaheshimiwa sana na Wakristo, marafiki na majirani. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linapenda kutuma salam na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam wakati huu wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaopambwa kwa matendo mema, heri na baraka kwa Siku kuu ya Id al Fitri.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika maadhimisho haya linapenda kwa namna ya pekee kuimarisha mahusiano ya maisha ya kiroho ili kujikita katika huruma ya Mungu. Kauli mbiu ya salam na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam inasema “Wakristo na Waislam walengwa na vyombo vya huruma ya Mungu”. Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa njia ya wema na huruma yake na kila siku anawakirimia mahitaji yao msingi kama vile: chakula, malazi na usalama bila kusahau msamaha pale wanapomkosea.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa upendo na huruma ya Mungu ameitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yaliyozinduliwa kunako tarehe 8 Desemba 2015 na yatahitimishwa hapo tarehe 20 Novemba 2016. Hiki ni kipindi cha kuganga na kuponya madonda; kuwaonesha watu uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya matendo ya huruma; ni muda muafaka wa kusamehe na kujikita katika mchakato wa upatanisho.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linasema hija za waamini wa dini ya Kiislam huko Mecca na Medina ni nyakati za kuonja huruma na upendo wa Mungu. Hiki ni kipindi cha baraka ili kukimbilia na kuambata msamaha wa dhambi kwa walio hai na wale waliotangulia mbele za haki. Wakristo na Waislam wanahamasishwa kujifananisha na Mungu kwa kuwa ni watu wenye huruma, msamaha na mapendo kama Yeye mwenyewe alivyo.

Katika ulimwengu mamboleo kuna watu wanaoteseka sana na wengi wao ni wazee, watoto na wanawake; kuna baadhi ya watu wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na mamillioni ya watu wanateseka kutoka na umaskini, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na majanga asilia. Waamini wa dini hizi mbili kamwe hawawezi kufumbia macho mateso na mahangaiko ya watu hawa, changamoto ya kushirikiana na kushikamana kwa pamoja ili kuwasaidia watu wenye shida mbali mbali, ili kutekeleza amri ya upendo kwa Mungu na jirani, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani katika maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Mwishoni, Baraza la Kipapa linawapatia waamini wote wa dini ya Kiislam salam na matashi mema ya Mfungo Mtukufu wa Mwezi wa Ramadhan na Siku kuu ya Id al Fitri kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.