2016-06-20 12:03:00

Matunda ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo la Musoma


Katika mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo Mama Kanisa anakazia dhana ya Sinodi kama jukwaa pana zaidi linaloikutanisha familia ya Mungu ili kusali, kutafakari na kupanga pamoja mikakati ya maisha na utume wa Kanisa. Jimbo katoliki Musoma katika maadhimisho ya Miaka 100 ya Imani Katoliki, limeadhimisha pia Sinodi ya kwanza ya Jimbo kwa kuongozwa na kauli mbiu “imani na matendo”. Jimbo Katoliki Musoma limetoa será, maazimio na matamko ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo: kwa kuzingatia: Imani ya Kanisa, Sakramenti, Ushuhuda na hatimaye changamoto katika ulimwengu mamboleo.

SURA YA KWANZA

 

IMANI TUNAYOIKIRI NA KUIENEZA

 

Utangulizi

 

  1. Imani ya Kikristo ni mwambatano wa nafsi ya mtu kwa Mungu.  Ni kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu ameufunua.  Kwa sababu hii Waraka kwa Waebrania hueleza “…. imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”  (Ebr. 11:1).  Uhakika huu hutokana na mtu kuambatanisha nafsi yake na Mungu na kuukubali kabisa ukweli unaofunuliwa naye.

 

Baba Mtakatifu Francis anaeleza kuwa imani hii kwa Kristo ni mwanga, na wote walionayo huona na kuangazwa kwa mwanga huo katika safari yao yote.  Wale waliokwisha kuupokea mwanga huu wa imani hawawezi kwa haki kukaa nao peke yao tu bali huwa kwao mwitikio na ungamo linalosambaa kwa wengine likiwaalika nao kuamini.2  Huu ndio mwanga ambao Kristo mwenyewe anasema hauji ili kuwekwa chini ya pishi au uvunguni bali huja ili kuwekwa juu ya kiango (rejea Mk. 4:21).

 

  1. Katika Jimbo letu, tumekwisha kuadhimisha miaka 100 ya imani ya Ukristo.  Kama ilivyokuwa mwanzo, hata sasa tunao wajibu wa kuieneza imani hiyo kama tulivyo na wajibu wa kuzidi kuishuhudia kwa matendo na maisha yetu yote.  Katika Sinodi hii, tumeainisha njia kuu mbili ambazo kwazo tunapenda kutekeleza wajibu huu wa kuieneza imani tunayoikiri.  Njia hizi ni Katekesi na Huduma za Jamii.

 

 

 KATEKESI

 

3.  Katekesi imezingatiwa daima na Kanisa kama moja ya wajibu wake wa msingi.  ni wajibu mtakatifu na ni haki ambayo Kanisa haliwezi kunyang’anywa.  Wajibu huu unatoka kwa agizo la Kristo Mwenyewe kwa mitume wake “… enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, …na kuwafundisha kuyashika yote nilowaamuru ninyi. ....” (Mt. 28:19-20).  Ndiyo maana tangu awali jumla ya shughuli zote za Kanisa za kuwafanya wanafunzi, kuinjilisha na kuujenga Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, iliitwa Katekesi.

 

4.  Katekesi ni wajibu wa Kanisa zima na kila mbatizwa anaalikwa kuushiriki kadiri ya nafasi yake.

 

  1. Askofu wa Jimbo:  huyu ndiye mchungaji mkuu wa Jimbo na mwalimu haswa wa imani.  Kwake upo wajibu na mamlaka ya kufundisha na kuhakikisha kuwa wahudumu wa Katekesi wanapatikana kote jimboni.

 

  1.  Mapadre: hawa huwekwa wakfu kwa ajili ya kuihubiri injili, kuwachunga waamini na kuadhimisha ibada kwa Mungu.  Sakramenti ya Daraja Takatifu inawafanya mapadre kuwa walimu wa imani kwa muunganiko na Askofu wa Jimbo na kwa msaada wa wahudumu weninge wa Katekesi.  Mapadre, hasa maparoko, wajione wanao wajibu wa kwanza kufundisha imani na kuratibu ufundhishani wa imani hiyo katika parokia na taasisi hasa shuleni na vyuoni.

 

  1. Watawa:  Watawa ni washiriki wa namna ya pekee katika Katesi.  Kihistoria, mashirika mengi ya kitawa yalianza kuwapo kwa nia ya kutoa elimu ya Kikristo kwa watoto na vijana hasa waliokuwa katika mazingira magumu.  Hata leo watawa huendelea kutoa Katekesi kwa ushuhuda wa maisha yao ya wakfu, kwa huduma za jamii wanazotoa na kwa kufundisha imani moja kwa moja katika shule na vyuo.  Ni matamanio ya Kanisa kwamba jumuiya za kitawa zitaendelea kujitoa kadiri iwezekanavyo kwa uwezo na nyenzo walizonazo kwa kazi hii maalumu ya Katekesi.

 

  1. Makatekista Walei:  Wakristo walei hushirikishwa kazi za Kristo mwenyewe za kikuhani, kinabii, na kifalme kwa njia ya Ubatizo.  Kutekeleza kazi ya kinabii ndiyo kufundisha imani.  Walei hutekeleza wajibu huu kwa namna wanavyoyaingia malimwengu.  Wanapaswa kuzingatia na kutekeleza wajibu huu katika nyanja zote za maisha yao.  Katika kazi za kuajiriwa na kujiajiri, katika biashara, siasa, uchumi, uongozi wa Serikali na jamii wasisahau kutekeleza wajibu huu wa kuwa waalimu wa imani kwa matendo yao.

 

Miongoni mwa walei wapo walioitwa na Mungu na kuteuliwa na Kanisa kulingana na mahitaji ya Kanisa ili kufundisha imani na kuongoza ibada mbalimbali bila Padre.  Hawa huitwa makatekista.  Wanao mchango mkubwa na wa muhimu katika Katekesi na kwa mchango huu hutengeneza ushirika na mapadre katika uchungaji maparokiani.

 

v. Wazazi na familia:  Familia ndiyo shule ya kwanza ya imani na wazazi ndio walimu wa kwanza wa imani kwa watoto wao.  Mafundisho ya imani anayoyapata mtoto katika familia huwa hayana mbadala na huacha alama ambazo hudumu maisha yao yote.  Familia hutoa mafundisho haya kwa watoto kwa namna wazazi wanavyotoa ushuhuda wa maisha ya Kikristo katika familia, kusali pamoja kifamilia na kuwapa malezi bora ya Kikristo.

 

5.  Sinodi yetu imelichukulia suala la Katekesi katika uzito wa pekee.  Kwa kuzingatia kuwa Katekesi katika undani wake ni kuelimisha katika imani watoto, vijana na watu wazima, tumebainisha maeneo manne tunayopenda kujikita katika kutoa Katekesi.  Maeneo haya ni yale yanayogusa makuzi na malezi ya mwanadamu, nayo ni katika:

 

  1. Taasisi za Elimu
  2. Matayarisho ya Kupokea Sakramenti
  3. Maisha baada ya Kupokea Sakramenti
  4. Vyama vya Kitume

 

 

 

Katekesi katika Taasisi za Elimu

 

  1. Taasisi za elimu, yaani shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo ni maeneo mahususi ambapo watoto na vijana hupata elimu na malezi.  Tunapenda kuhakikisha kuwa elimu na malezi wanayopata vinaenda sambamba na elimu ya Imani Katoliki.  Elimu hii itatolewa kwa kufundisha “Somo la Dini” kama ambavyo imekuwa inafanyika kimapokeo.  Somo hili litafundishwa katika taasisi zetu zote za elimu.  Jitihada ifanyike kuwafikia hasa Wakatoliki walio katika taasisi za serikali, madhehebu na hata katika taasisi binafsi ili nao wasikose nafasi ya kupata Katekesi.

 

7.  Bila kuhimiza Katekesi hatuwezi kuwa na Wakristo hodari na imara katika imani na matendo na hatuwezi kuwa na jamii iliyo na hofu ya Mungu.  Ni dhahiri kuwa kukosekana kwa Katekesi hii kutasababisha ubaridi katika maisha ya imani, kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana na kushamiri kwa mila, desturi na mazoea yanayopingana na Ukristo.

 

8.  Ili kuhimiza Katekesi na kuipa umuhimu wa pekee Jimboni Musoma, kwa kuzingatia fursa na hali halisi tuliyonayo, tunaazimia yafuatayo:

 

  1. Katika shughuli za uchungaji maparokiani, Katekesi ipewe kipaumbele.  Mapadre na hasa maparoko wafanye jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa taasisi za elimu zilizoko katika maeneo ya parokia zao zinakuwa maeneo ya kutoa katekesi.  Wanapaswa kuwashirikisha watawa na walei kuhakikisha wahudumu wa Katekesi wanapatikana na wao wenyewe kujitoa kufundisha dini katika taasisi hizi.

 

  1. Idara ya Katekesi ianzishe UWAKA (Umoja wa Walimu Katoliki).  Umoja huu uwaunganishe walimu wote Wakatoliki, uwawezeshe na kuwahamasisha kufundisha dini katika taasisi za elimu.  Kijimbo umoja huu uwe chini ya Mkurugenzi wa Katekesi Jimbo na kiparokia umoja huu uwe chini ya paroko.  Umoja huu waweza kujumuisha pia wastaaafu wa ualimu au wa taaluma mbalimbali ambao bado wana nguvu na majitoleo ya kufundisha.

 

Idara ya Katekesi iwe pia kiungo kati ya umoja huu na uongozi wa taasisi za elimu.  Ibuni mbinu za kushughulikia changamoto mbalimbali za kiutendaji zinazoweza kuwa kikwazo kwa utoaji wa Katekesi katika taasisi hizo.

 

  1. Kuwepo na mitihani ya kijimbo ya Katekesi kwa shule za msingi, sekondari na vyuo.  Mitihani hii iendane na ile ya kitaifa na ifanyike kwa darasa la nne na la saba kwa shule za msingi na ifanyike kwa kidato cha pili, cha nne na cha sita kwa shule za sekondari.  Katika vyuo, Idara ya Katekesi iandae mitihani hiyo na ifanyike kwa wakati muafaka kulingana na mazingira ya pekee ya kila chuo.  Mitihani hii iambatane na vyeti vya kijimbo vinavyoonesha alama za ufaulu za kila mtahiniwa.

 

  1. Iandaliwe Katekisimu ya Jimbo.  Katekisimu hii iwe ni mkusanyiko wa mafundisho ya Kanisa na yale yanayogusa mahitaji ya pekee ya Jimbo letu.

 

  1. Duka la Vitabu la Jimbo liwe kituo cha upatikanaji wa vitabu na matini mengine ya Katekesi.  Ni vema kila parokia ikaanzisha duka la vitabu ili waamini wapate rejea za vitabu vya Katekesi katika parokia zao.

 

  1. Chuo chetu cha Katekesi Komuge kiendelee kuwa msaada kwa kuwajengea uwezo makatekista wetu.  Kionwe kuwa ndio moyo na kitalu cha kuwaandaa makatekista na tena kiwe na ukaribu wa kiutendaji na Idara ya Katekesi.  Pamoja na kuendelea kutoa kozi ndefu kadiri ya mpango wa Baraza la Maaskofu zitolewe pia kozi fupifupi hasa nyakati za likizo.

 

Katekesi katika Matayarisho ya Kupokea Sakramenti

 

  1. Katekesi ina muunganiko wa pekee na matendo yote ya liturujia na maadhimisho ya sakramenti.  Ni katika sakramenti hasa Ekaristi Takatifu, Kristo anatenda kwa ukamilifu zaidi kazi ya kuugeuza ubinadamu mzima.  Katika Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo, Katekesi ni hatua muhimu na tangu mwanzo Kanisa limewaandaa wanawe kupokea sakramenti hizo kwa kuwapa Katekesi.  Hatua hii huitwa ukatekumeni.

 

10.  Katika Jimbo letu desturi hii njema inaendelezwa.  Kote maparokiani Katekesi hutolewa kwa wanaojiandaa kupokea sakramenti za awali na nyinginezo.  Hata hivyo kuna upungufu uliojitokeza mintarafu kutofautiana kwa muda wa kutoa mafundisho, kutokuwepo kwa muhtasari wa kijimbo na uhaba wa walimu wa Katekesi.

 

11.   Ili kukabiliana na changamoto hizi na kufikia ufanisi unaotakiwa katika Katekesi tunaagiza kuwa Idara ya Katekesi iratibu utaratibu mzima wa mafundisho yaani iandae muhtasari wa mafundisho ya Katekesi kwa watu wazima na vijana walio mashuleni wanaojiandaa kupokea sakramenti za awali.  Muhtasari huu ndio utakokuwa unatumiwa kote jimboni na uandaliwe hivi kwamba:

 

  1. Mafundisho ya Ubatizo kwa watu wazima na vijana walio mashuleni yatolewe kwa miaka miwili.

 

  1. Mafundisho ya Komunio ya kwanza kwa waliopokea Ubatizo wa watoto wachanga yatolewe kwa miaka miwili.

 

  1. Mafundisho ya Kipaimara yatolewe kwa muda wa miezi mitatu.

 

  1. Mafundisho kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa yatolewe kwa muda wa mwezi mmoja.

 

     Umri wa chini wa kuanza mafundisho haya utakuwa ni miaka 10 au darasa la nne katika shule za msingi.

 

 

Katekesi baada ya Kupokea Sakramenti

 

12.  Baada ya kupokea sakramenti za awali, Wakristo huanza safari ya kuishi imani na kushiriki kikamilifu katika Kanisa.  Hatua hii huanza kwa “mistagojia”, kipindi cha mafundisho ya kina na huendelezwa kwa malezi endelevu.  Tunahitaji kurejea mapokeo ya Kanisa na kurejesha mistagojia kwa Wakristo wapya.  Sambamba na hilo malezi endelevu ya imani yawekewe mfumo na yatiliwe mkazo.

 

13.  Malezi haya endelevu yafanyike kwa njia za semina, makongamano na warsha mbalimbali zitakazoratibiwa na Idara ya Katekesi Jimbo.  Idara hii iandae mada na kuratibu utolewaji wa mada hizo kiparokia na kwa kufuata mahitaji ya makundi mbalimbali ya wana wa Mungu jimboni Musoma kama vile watoto, vijana, wanandoa na wazee.

 

Katekesi kwa Vyama vya Kitume

 

14.  Vyama vya kitume ni namna ambayo waamini huungana bila nadhiri za kitawa kutekeleza utume wao kwa kuishi na kufuata karama maalumu ya utume.  Vyama hivi ni vya msaada mkubwa katika uinjilishaji na uenezaji imani.  Vipo vyama vya kulea miito, vyama vya kuchochea moyo wa Ibada na vyama vya huduma katika Kanisa.

 

15.  Vyama vya kulea miito hujumuisha vyama vya kuwalea na kuwasaidia Wakristo kung’amua miito yao.  Hivi ni pamoja na Utoto Mtakatifu, Chama cha Wito, Ushirika wa Mtakatifu Aloisi, Shirika la Bikira Maria, TYCS na VIWAWA.  Hujumuisha pia vyama vya kuwasaidia walio tayari katika miito mbalimbali kuishi vema miito yao.  Hivi ni pamoja na Marriage Encounter, WAWATA na Shirika la Wazee na Wastaafu.

 

        Vyama vya kuchochea moyo wa Ibada hujumuisha Rozari Hai, Utume wa Sala, Lejio Maria, Ushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Shirika la Mitume wa Huruma ya Mungu na Undugu wa Skapulari.  Vyama vya huduma hujumuisha Chama cha Mtakatifu Vicent wa Paulo na Caritas.

 

16.   Kila chama cha kitume kina katiba na mafundisho yake msingi yanayokubaliwa na Kanisa.  Ni vema maparoko na viongozi wa vyama hivi wakahakikisha kuwa wanachama wanafuata katiba na wanapata mafundisho kuhusu vyama ili wazidi kuvielewa na kutekeleza vema karama mahusui za kila chama.  Juhudi zifanyike kuanzisha vyama hivi katika parokia zetu na waamini wahamasishwe kujiunga.  Zaidi ya hayo tunapenda vyama hivi viwe pia nafasi ya wanachama kupewa Katekesi endelevu juu ya mafundisho ya Kanisa.

 

 

HUDUMA ZA JAMII

 

17.   Katekesi ni namna ya moja kwa moja ya kueneza kweli za kiimani.  Ipo pia njia nyigine isiyo ya moja kwa moja ya kueneza kweli hizi.  Hii ni njia ya kutoa huduma kwa jamii.  Tangu mwanzo, Kanisa ni washirika pamoja na serikali na asasi nyingine katika kuhudumia jamii.  Limefanya hivi kwa kutoa huduma za elimu, afya, kilimo bora, maji na kushiriki harakati za kuiletea jamii maendeleo halisi.  Kanisa huingia katika kutoa huduma hizi kwa mlengo wa kichungaji likiongozwa daima na tunu za kiinjili.

 

         Lengo na sura hii ya Kanisa inaakisiwa katika Jimbo letu kwa uwepo wa taasisi zetu nyingi zinazoshughulika na huduma za jamii.  Tunazo taasisi za elimu na afya, vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, vituo vya kutokomeza mila potofu na vingine vingi.

 

18.    Haitoshi tu kuwa na taasisi na vituo hivi ikiwa huduma zitolewazo hazina ubora na haziihudumii jamii ipasavyo.  Taasisi na vituo vyetu vinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora na kuendeshwa kwa kuzingatia tunu za kiinjili na za kimaadili.  Kwa hiyo tunaagiza yafuatayo:

 

  1. Katika kila parokia ziwepo taasisi zetu za kutoa huduma za jamii kadiri ya mahitaji ya eneo husika hasa elimu na afya.

 

  1. Iandaliwe Sera ya Jimbo kuhusu Huduma za Jamii.

 

  1. Ili kuongeza ufanisi katika taasisi na vituo vyetu vya kutoa huduma kwa jamii, vituo hivi viendeshwe na visimamiwe na wale walio na weledi katika huduma husika.

 

  1. Kianzishwe Chama cha Wanataaluma Wakristo (CPT) ambao kwa majitoleo yao watakuwa ni msaada mkubwa katika utume wa Kanisa katika masuala yahusuyo jamii.

SURA YA PILI:

 

IMANI TUNAYOIADHIMISHA

 

LITURUJIA

 

Dhana ya Liturujia

 

19.    Adhimisho la Misa Takatifu ambalo ni utendaji wa Kristo na taifa la Mungu liloundwa Kihierakia, ndiyo kiini cha maisha yote ya Kikristo, kwa Kanisa lote au kwa Kanisa Mahalia na kwa waamini wote kila mmoja peke yake.  Adhimisho hili ndicho kilele cha utendaji wa Mungu, ambamo Mungu huutakatifuza ulimwengu katika Kristo na ni kilele cha ibada ambayo wanadamu humtolea Baba, kwa kumwabudu kwa njia ya Kristo Mwanae, katika Roho Mtakatifu.  Na hii ndiyo huitwa Liturujia.  Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana adhimisho la Liturujia hasa Misa takatifu kufanyika katika hali na mazingira ya maanani zaidi tangu maandalizi yake hivyo kwamba kusanyiko zima liwe na ushiriki wa utendaji hai na mkamilifu, yaani mwili na roho.  Ushiriki wa namna hii ni haki na wajibu walio nao taifa la Kikristo kutokana na Ubatizo wao.

 

20.    Liturujia ni tendo la Kanisa zima na huadhimishwa kwa kufuata miongozo na kanuni ambazo zimeheshimiwa na kuhifadhiwa kiaminifu katika mapokeo ya Kanisa.  Tunapenda kuendeleza mapokeo haya ili kukuza ushiriki hai na mkamilifu wa watu katika Liturujia.  Ili kufanikisha haya tunadhamiria kuanzisha na kuimarisha vyombo vya utendaji na utekelezaji vitakavyotoa, vitakavyoelekeza na kusimamia miongozo na kanuni mbalimbali za kiliturujia.  Hivyo:

 

  1. Idara ya Liturujia Jimbo iimarishwe na ipewe ushirikiano ili iendelee kutimiza majukumu yake.

 

  1. Iundwe Kamati ya Liturujia Jimbo.  Kamati hii, pamoja na mengine, ishughulikie yafuatayo:

 

 

 

 

 

            iii. Kwa ngazi ya parokia ziundwe pia Kamati za Liturujia za parokia chini ya maparoko ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa hapo juu.

            Aidha Sinodi inaagiza kuwa malezi na mafunzo ya Liturujia katika vituo vya malezi vilivyoko jimboni vipewe mkazo mahsusi.

 

Muziki Mtakatifu

 

21.    Kuimba kutakatifu kumesifiwa katika Maandiko Matakatifu na pia mababa wa Kanisa ambao kwa nyakati mbalimbali wamesisitiza kwa dhati karama na huduma ya kuimba kutakatifuza katika ibada ya Liturujia.  Kwa hiyo muziki mtakatifu utazidi kuwa mtakatifu pale uunganikapo na tendo la Liturujia; maana utafanya sala kuwa tamu zaidi na kuonyesha umoja wa mioyo, pia utaleta heshima zaidi katika maadhimisho matakatifu.  Tena Kanisa linakubali na kuingiza katika ibada kwa Mungu mitindo yote ya sanaa ya kweli, lakini yenye sifa zinazotakiwa.

 

22.      Kwa kuzingatia mwaliko huo wa Mtaguso wa pili wa Vatikano, Sinodi inaona ni vyema wazo hili likapewa msukumo wa pekee ili kupunguza au kuondoa kabisa baadhi ya kasoro mintarafu machezo wakati wa uimbaji hasa kwa wanakwaya na Utoto Mtakatifu wa Yesu.  Pili, kuondoa nyimbo zisizo na teolojia ya Kikatoliki.  Tatu, uwepo uratibu makini wa nyimbo za Litutujia kwa ngazi za parokia na Jimbo hasa kuptia kwa Paroko/Kamati ya Liturujia.

 

23.       Hivyo tunaazimia yafuatayo:

 

            i.    Liundwe shirikisho la kwaya Jimbo chini ya Idara ya Liturujia.

 

            ii.   Kwaya zote ziwe na katiba moja.

 

            iii. Watunzi wa nyimbo wafahamike na wapewe semina kwa kuzingatia sheria na kanuni za utunzi wa nyimbo za Liturujia kwa mujibu wa miongozo ya Kanisa.

 

            iv. Iwekwe miongozo ya machezo wakati wa Misa kwa wanakwaya na watoto wa utamadunisho.

 

            v. Nyimbo zenye mtindo wa ki-Gregoriana zipewe kipaumbele zaidi hasa kwa wimbo wa katikati katika Misa kwani ndio mtindo rasmi wa Kanisa la Roma na ni mtindo rahisi kuimbwa na wengi.

 

MAISHA YA SAKRAMENTI

 

24.     Imani tunayoiadhimisha katika Liturujia hurutubishwa na kupata kiini chake katika Sakramenti na maadhimisho yake.  Kristo ameweka Sakramenti saba: Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja Takatifu na Ndoa.  Sakramenti hizi zinagusa hatua zote na nyakati zote muhimu za maisha ya Mkristo.  Kwake yeye anayezipokea kwa imani, sakramenti ni tendo la Kristo mwenyewe ambaye kwa njia na ndani ya Kanisa hutoa neema.

 

25.      Maisha ya imani ya Mkristo na maisha ya Kanisa zima ni maisha ya sakramenti.  Kanisa lenyewe ni sakramenti, yaani ni alama hai ya uwepo wa Kristo ulimwenguni.  Katika maadhimisho ya sakramenti Kanisa linatenda alivyotenda na kukusudia Kristo Mwenyewe.  Kwa jinsi hii utume wote wa Kanisa unapaswa kuwaelekeza watu kwenye sakramenti; kuziadhimisha, kuzipokea na kuziishi.

 

            Tukirejea msisitizo ule ule wa mafundisho ya Kanisa kuhusu sakramenti, tunaona ni vema kufafanua baadhi ya taratibu tunazoona zitasaidia waamini kuzielewa, kuziadhimisha, kuzipokea kuziishi vema zaidi sakramenti.

 

Sakramenti ya Ubatizo

 

26.       Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho, na mlango unaowezesha kuzipata sakramenti nyingine.  Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru toka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume wake: Ubatizo ni sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika neno.22

 

Ubatizo wa Watoto Wachanga

 

27.     Watoto wachanga, kwa kuwa wanazaliwa na hali ya kibinadamu iliyoanguka na kuchafuliwa na dhambi ya asili, wana lazima ya kuzaliwa upya katika Ubatizo ili wawekwe huru na nguvu za giza na kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu ambamo watu wote wameitwa.  Hatuna budi kuisisitiza na kuiendeleza desturi hii njema na ya kimapokeo ya kuwabatiza watoto wachanga ili kuwapa neema isiyopimika ya kuwa waana wa Mungu.  Hivyo tunapenda iwe ni sera ya Jimbo letu kuwa Ubatizo wa watoto wachanga uadhimishwe katika parokia zetu walau mara moja kwa mwezi.

 

28.      Kabla ya Ubatizo maandalizi ya kutosha yafanyike.  Maandalizi haya ni pamoja na kukusanya taarifa zote muhimu kuhusu mtoto na familia yake ili baada ya Ubatizo taarifa hizi ziingizwe katika vitabu vya parokia.  Hali kadhalika ni muhimu sana wazazi na wasimamizi wa Ubatizo wapewe mafundisho ya kutosha.  Tunaagiza Idara ya Katekesi iandae muhtasari huu ambao utakuwa ukitumika Jimbo zima.

 

29.   Ubatizo ni sakramenti ya imani.  Watoto wachanga hubatizwa kwa imani ya wazazi wao na imani ya Kanisa.  Kwa mbatizwa imani hii ni lazima ikue kusudi neema ya Ubatizo iweze kukua.  Hapa msaada wa wazazi, waliokomaa katika imani na wanaoweza kuonesha mfano mzuri wa imani hii kwa mwenendo wao wa maisha, ni wa lazima.  Alama mojawapo na yenye maana sana kwa mwenendo unaoakisi imani ya wazazi ni kuishi katika misingi ya Kikristo ya familia iliyojengwa katika ndoa takatifu.  Kwa hiyo, isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali cha Baba Askofu, Ubatizo wa watoto wachanga wasiotokana na ndoa za Kikristo uahirishwe hadi watakapokua na kupata mafundisho ya ukatekumeni.

 

Ubatizo wa Watu Wazima

 

30.  Watu wazima hubatizwa baada ya ukatekumeni.  Hiki ni kipindi cha mafundisho, maandalizi na malezi kwa ajili ya maisha yote ya Kikristo.  Kwa kuzingatia muunganiko wa pekee uliopo katika sakramenti za kuingizwa katika Ukristo (Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu), tunaazimia kuwa watu wazima wanapobatizwa wapokee siku hiyo Sakramenti hizi zote tatu.  Kwa vile utaratibu huu unaanza kwa mara ya kwanza jimboni Idara ya Kichngaji na ya Liturujia zitoe kwanza taratibu na miongozo itakayokuwa inafuatwa katika kulitekeleza hili.

       

         Aidha kwa kuwa Ubatizo wa watu wazima hutanguliwa na hatua na matakaso wakati wa ukatekumeni, na kwa kuwa hatua na matakaso hayo yameandaliwa hivi kwamba yafanyike wakati wa kipindi cha Kwaresima, tunaagiza kuwa Ubatizo wa watu wazima ufanyike katika kipindi cha Pasaka kama taratibu za kiliturujia zinavyoelekeza.

 

Sakramenti ya Kipaimara

 

31.   Kipaimara hukamilisha neema ya Ubatizo; ni sakramenti inayomtoa Roho Mtakatifu kwetu ili kututia mizizi ya kina kwa uthabiti zaidi katika Kristo; huufanya muungano wetu na Kanisa uwe wenye nguvu zaidi, hutuhusisha kwa karibu zaidi na utume wake na hutusaidia kuishuhudia imani kwa maneno yanayofuatana na matendo.  Kipaimara sawa na Ubatizo huchapa ndani ya Roho ya Mkristo alama ya kiroho au mhuri usiofutika, kwa sababu hiyo sakramenti hii hupokewa mara moja tu katika maisha.

 

32.   Kwa kuwa tulishaazimia kuwa watu wazima wanapopokea sakramenti ya Ubatizo wapokee siku hiyo hiyo sakramenti zote tatu za kuingizwa katika Ukristo, utaratibu wa kupokea Kipaimara hasa kwa Wakristo waliobatizwa wakiwa watoto wachanga utakuwa kama ifuatavyo:

       

         i. Baada ya Komunio ya kwanza, Wakristo watafuata mafundisho kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu ili kupokea sakramenti ya Kipaimara.  Muhtasari wa mafundisho haya utaandaliwa na Idara ya Katekesi.

 

         ii.   Umri wa chini wa kupokea sakramenti hii ni walau miaka 11 ya kuzaliwa.

 

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu

 

33.   Ekaristi ni chemichemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo.  Sakramenti nyingine, kama zilivyo pia huduma zote za Kanisa na kazi za utume, zaungana na Ekaristi na zaelekezwa kwake.  Kwani katika Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu.  Hivyo ni muhimu adhimisho la Ekaristi lipangwe kuonesha hadhi na umaana wake.  Waadhimishaji wa Ekaristi na wote walio na majukumu ya pekee katika adhimisho hilo ni vema wakafuata daima miongozo (rubrics) ya kiliturujia.  Hali kadhalika, waamini wahimizwe kushiriki na kupokea Ekarist Takatifu mara nyingi na tena kwa uchaji.

 

Komunio ya Kwanza

 

34.  Yataendelea kutolewa mafundisho ya Katekesi kabla ya kupokea Komunio ya Kwanza.  Mafundisho haya yatolewe kwa muda wa miaka miwili na muhtasari wake uandaliwe na Idara ya Katekesi.  Umri wa chini wa kujiandikisha kwa mafundisho haya utakuwa ni miaka 10 ya kuzaliwa.

 

Wahudumu wasio wa kawaida wa Kugawa Komunio

 

35.   Wahudumu wa kawaida wa kugawa Komunio Takatifu ni Maaskofu, Mapadre na Mashemasi.  Kulingana na mahitaji ya kichungaji baadhi ya walei, hasa watawa na makatekista, hupewa kibali cha kugawa Komunio Takatifu kama wahudumu wasio wa kawaida.  Wahudumu hawa wasio wa kawaida wataendelea kugawa Komunio Takatifu baada ya kupata kibali kwa maandishi kutoka kwa Baba Askofu.  Kibali hiki wataombewa na Paroko mahalia na kitadumu kwa muda wa mwaka mmoja tu.  Muda huo ukishapita, Paroko atapaswa kuomba tena kibali endapo bado kuna hitaji.

 

         Kabla ya kuomba kibali hicho wahudumu hawa wasio wa kawaida watapaswa kuhudhuria semina elekezi itakayokuwa inaratibiwa na kuandaliwa na Idara ya Liturujia Jimbo.

 

Sakramenti ya Kitubio

 

36.   Kwa njia ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu mtu hupokea uzima mpya wa Kristo.  Lakini kama anavyofundisha Mtume Paulo, tunaupokea uzima huu katika vyombo vya udongo (rejea 2Kor. 4:7).  Kwa kuwa tumo bado katika makao ya duniani, uzima huu mpya wa mtoto wa Mungu waweza kudhoofishwa na hata kupotezwa kwa dhambi.  Bwana Yesu Kristo, mganga wa roho zetu na miili yetu alitaka Kanisa lake liendeleze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kazi yake ya uponyaji na ya wokovu.  Kazi hii huendelezwa kwa sakramenti mbili za uponyaji ambazo ni Kitubio na Mpako wa Wagonjwa.

 

37.   Kanisa daima hutualika kuzichunguza dhamiri zetu kwa unyenyekevu na ukweli wote mbele ya Mungu ili kuubaini na kuukiri udhaifu wetu mbele yake.  Kwa maana Maandiko Matakatifu hutufundisha “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.  Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1Yoh. 1:8-9).

 

38.   Hali halisi inaonesha kupungua kwa mwamko wa waamini kupokea sakramenti ya kitubio.  Lipo hitaji kubwa sasa la kukuza mwamko huo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya watu kuipata huduma hiyo katika parokia zetu.  Ili kukuza mwamko huu ni muhimu kwa mapdre kutoa mafundisho ya mara kwa mara kuhusu sakramenti ya kitubio na kuwahimiza waamini kuipokea kwa uchaji.  Mafundisho haya yanapaswa pia kutolewa sambamba na elimu juu ya vikwazo vya kisakramenti na mikakati ya kiparokia kuwakwamua walio katika vikwazo hivyo.

 

         Mwamko wa waamini kupokea sakramenti ya kitubio unahitaji pia kuwepo kwa mazingira mazuri katika parokia.  Hivyo tunaagiza kuwa katika kila parokia iwepo ratiba kwa wiki inayoonesha uwepo wa mapadre kwa ajili ya huduma ya kitubio.  Pamoja na hayo, kitubio kwa dhambi zilizotengwa kitatolewa kufuatana na mwongozo utakaotolewa na Baba Askofu.

 

Mpako wa Wagonjwa

 

39.   Kwa mpako mtakatifu wa wagonjwa na sala za makuhani, Kanisa lote huwakabidhi wagonjwa kwa Bwana aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaoka.  Na kwa hakika lawahimiza wajiunge kwa hiari na Mateso na kifo cha Kristo ili kutoa mchango wao kwa manufaa ya Taifa la Mungu.  Kwa sakramenti hii Mkristo anayepata magumu ya ndani yatokanayo na ugonjwa wa hatari au na uzee, hupewa neema ya pekee: “…. kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua na hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”  (Yak. 5:15).  Kila mara Mkristo anapougua ugonjwa wa hatari anaweza kupokea Mpako Mtakatifu.28

 

40.   Katika Jimbo letu tunahitaji bado kutoa Katekesi kuhusu sakramenti hii kwani baadhi ya waamini wanaogopa kuipokea sakramenti kwa kuihusianisha na kifo.  Changamoto nyingine iliyopo ni kwamba bado hapajawa na mfumo mzuri unaohakikisha kuwa wagonjwa katika familia na JNNK wanapata huduma hii.  Hali hii inapelekea wengine kutokuhudumiwa kabisa na baadhi hufa bila kupokea sakramenti.

 

41.    Ili kuondoa upotofu juu ya sakramenti hii na kuhakikisha kuwa utume wa Kanisa kwa wagonjwa unatekelezwa vema Jimboni Musoma, tunapenda kurejea msisitizo kuwa shina la huduma kwa wagonjwa ni JNNK.  Kila JNNK iwe na mtu katika safu ya uongozi wake atakayekuwa anahusika na wagonjwa.  Mojawapo ya majukumu yake yatakuwa ni kuwasiliana na mapadre kuhusu huduma za kisakramenti kwa wagonjwa walio katika Jumuiya yake.

 

         Katika kila parokia pawe na ratiba ya huduma ya sakramenti kwa wagonjwa walau mara moja kwa wiki.  Katika ngazi ya Jimbo, tutakuwa na siku moja kwa mwaka ambapo kote Jimboni patakuwa na Misa na kutolea sala kwa ajili ya wagonjwa.

 

Mazishi

 

42.  Mazishi ya Kikristo ni adhimisho la Liturujia ya Kanisa.  Kanisa, ambalo kama mama limemzaa Mkristo kisakramenti katika hija yake duniani, linamsindikiza mpaka mwisho wa safari yake, ili kumweka mikononi mwa Baba.  Linamtolea Baba katika Kristo mtoto wa neema yake, na katika tumaini linaikabidhi ardhi mbegu ya mwili utakaofufuliwa katika utukufu.

 

43.  Ipo miongozo ya jumla ya Kanisa, kisheria na kiliturujia, kuhusu mazishi ya Kikristo.  Tunahimiza kuwa miongozo hii ifuatwe daima na kwa kuzingatia mahitaji halali ya mahali yatakayopimwa kwa busara ya kichungaji.  Katika kuyabainisha mahitaji hayo ni vema yafuatayo yakazingatiwa:

 

  1. Viongozi wa JNNK alimokuwa anasali Mkristo wapeleke parokiani ombi la mazishi ya Mkristo kwa kujaza fomu za mazishi.  Fomu hii iambatane na uthibitisho wa Paroko endapo marehemu atasafirishwa kwanda parokia au Jimbo lingine.

 

  1. Ni vema Misa ya mazishi ikafanyika kanisani au kigangoni ambapo marehemu alizoea kusali.

 

  1. Mazishi yafanyike katika makaburi ya Parokia au ya familia kama familia inalo eneo lake la kuzika.  Mazishi yanapofanyika katika makaburi ya familia, paroko aweza kuridhia Misa ifanyike nyumbani kwa marehemu.

 

  1. Matanga yafanyike kadiri ya mila na desturi njema za jamii mahalia zisizopingana na Ukristo.

 

Sakramenti ya Daraja Takatifu

 

44.   Daraja ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati: Hivyo hiyo ni Sakramenti ya huduma ya kitume.  Ina ngazi tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi.30  Sakramenti hii humfanya mpokeaji afanane na Kristo ili ahudumie kama chombo cha Kristo kwa ajili ya wokovu wake na wa kundi analokabidhiwa.

 

45.   Ni wajibu wetu kulinda hadhi na utakatifu wa huduma ya kipadre ambayo taifa lote la Mungu linaihitaji kwa ajili ya wokovu.  Awali ya yote tunawaalika mapadre kuzidi kuitambua hadhi yao na utakatifu wa huduma wanayoitoa ili kwamba mwenendo na maisha yao yote yaakisi hadhi na utakatifu wa huduma hiyo.  Katika kusaidia kutekeleza hili tunaagiza uandaliwe mwongozo wa kijimbo kuhusu maisha na utume wa mapadre (Norma vitae).

 

         Ni jukumu la waamini kuwahudumia wachungaji wao, kuwategemeza, kuwaombea na kuwashauri vema kwa kutumia vyombo vya ushauri vilivyowekwa na Kanisa.  Wajibu huu hutekelezwa pia kwa njia ya sala.  Hivyo tunaazimia kuwa na siku ya sala kwa ajili ya kuwaombea wahudumu wa daraja ili wanapoimarishwa kiroho na kimwili kwa msaada wa sala waendelee kulichunga, kulifundisha na kulitakasa kundi walilokabidhiwa. Siku hii ya sala kwa ajili yao itakuwa ni kila alhamisi ya kwanza ya mwezi.

 

Sakramenti ya Ndoa Takatifu

 

46.   Agano la ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto.  Agano hili, kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti.

 

Maandalizi ya kupokea Sakramenti ya Ndoa

 

47.   Sinodi imebaini hitaji kubwa la kuboresha maandalizi kwa wanaojiandaa kupokea sakramenti ya ndoa ili kuwasaidia wanandoa kuzikabili vema changamoto mbalimbali zinazoibuka katika nyakati zetu mintarafu maisha ya ndoa.  Hivyo tunaagiza na kusisitiza kuwa:

 

  1. Kiwepo kipindi cha kutosha kwa wachumba kupewa mafundisho ya kina kabla ya kufunga ndoa.  Muhtasari wa mafundisho haya uandaliwe na Idara ya Katekesi.

 

  1. Vituo vinavyotoa mafundisho ya ndoa vibainishwe na vifuate muhtasari utakaoandaliwa na Idara ya Katekesi.

 

Ndoa Mseto na Ndoa za Mchanganyiko wa Dini

 

48.   Ndoa Mseto ni ndoa kati ya Mkatoliki aliyebatizwa na Mkristo asiye Mkatoliki.  Ndoa ya Mchanganyiko wa Dini ni ndoa kati ya Mkatoliki na yule asiyebatizwa.  Katika kundi la wasioatizwa wamo Waislalm, Wasabato, waamini wa madhehebu ambayo Ubatizo wao hautambuliwi na Kanisa Katoliki pamoja na waamini wa dini za asili.

 

         Japokuwa katika mazingira yetu ndoa mseto na za mchanganyiko wa madhehebu hutokea mara nyingi na pia tofauti za imani kati ya wafunga ndoa si kizuizi kikubwa sana kwa ajili ya ndoa, tunahimiza kuwa vijana Wakatoliki wahimizwe kuchagua wachumba Wakatoliki ili kuepuka migogoro ya kifamilia na hasa inayohusiana na malezi ya watoto kwa sababu ya utofauti wa imani za wazazi.

 

         Kwa sababu za kichungaji inapolazimika kufungwa ndoa mseto na za mchanganyiko wa dini taratibu kadiri ya sheria kanuni za Kanisa zifuatwe.  Kwa ndoa mseto inahitajika barua ya ruhusa kutoka kwa askofu na kwa ndoa ya mchanganyiko wa dini kinahitajika kibali wazi kinachoondoa kizuizi toka kwa askofu.  Maparoko waombe ruhusa na vibali hivi kabla ya kuanza kutangaza ndoa hizi.

 

KUKUZA MAISHA YA SAKRAMENTI

 

49.   Kwa njia ya sakramenti tunapata uzima wa kimungu ndani yetu.  Uzima huu unahitaji kujengewa mazingira mazuri ili ukue na kuzaa matunda mema na yanayodumu.  Katika kujenga mazingira haya, zipo njia nyingi ambazo Kanisa daima huelekeza.  Njia hizi ni pamoja na sala, Neno la Mungu mazoezi mbalimbali ya kiroho na mfumo mzuri wa maisha.

 

Sala

 

50.    Sala ni kuinua moyo na roho kwa Mungu.  Ni ombi kwa Mungu kwa mema yafaayo na ni tendo la Mungu na la Mwanadamu linalobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kutoka kwetu, yote ikielekezwa kwa Baba katika umoja wa utashi wa kibinadamu wa Mwana wa Mungu aliyefanyika mwanadamu.  Hivyo, maisha ya sala ni desturi ya kuwa mbele ya uwepo wa Mungu Mtakatifu na katika umoja naye.  Umoja huo unawezekana siku zote kwa sababu, kwa Ubatizo, sisi tumekuwa kitu kimoja na Kristo.34

 

51.   Moyo wa sala unapaswa kutawala maisha ya kila mmoja wetu; mtu binafsi, familia, JNNK, parokia na Jimbo zima.  Kukuza moyo huu kwa mazoezi mbalimbali ya kiroho na ili kujipatia rehema tunaagiza kuwa kila parokia iwe na walau siku moja kwa mwaka kufanya hija na mafungo katika moja ya vituo vyetu vya hija Kiabakari na Nyakatende kulingana na utaratibu wa vituo hivyo.

 

         Katika parokia zetu kuwe na ibada za kuabudu Ekaristi Takatifu walau mara moja kwa wiki.  Na kila Alhamisi ya kwanza ya mwezi ambayo kwa kauli moja tunaagiza Jimbo zima liwe katika ibada hiyo ya maabudio ndani ya parokia zetu.  Aidha siku ya Mtakatifu Somo msimamizi wa Parokia itazamwe kuwa ni siku ya kujitakatifuza kwa maombezi ya Mtakatifu husika.  Parokia ziandae mpango wa kujitakatifuza kwa mafundisho na mazoezi mbalimbali ya kiroho kuelekea siku hiyo.

 

         Kijimbo tutakuwa na Siku ya Jimbo.  Katika siku hii, tutakuwa na adhimisho la Misa ya Kijimbo ambapo tutatolea sala kwa ajili ya Jimbo letu kwa maombezi ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, msimamizi wa Jimbo letu.  Kuelekea siku hiyo, waamini waandaliwe kwa njia ya mafundisho na maadhimisho mbalimbali kwa utaratibu utakaowekwa na Idara ya Kichungaji kwa kushirikiana na vyombo vingine husika.  Siku ya Jimbo ndiyo itakuwa pia na siku ya Mshikamano na kutegemeza Jimbo.

 

Neno la Mungu

 

52.   Neno la Mungu huchukua nafasi ya kwanza kati ya maandishi yote ya kiroho yawezayo kukuza uzima wa kimungu ndani ya waamini.  “Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kwa kuwaadhibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” (2Tim. 3:16-17).

 

53.   Uchaji kwa Neno la Mungu unahitaji kukuzwa katika maisha ya Wakristo ili kwa kulisoma na kulitafakari Neno hilo kama desturi ya maisha wazidi kukua na kukomaa katika hekima ya kimungu ipatikanayo humo.  Kukuza uchaji huu tunaazimia yafuatayo:

 

  1. Iwekwe hamasa ya pekee kwa waamini kupenda kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu.

 

  1. Katika kila familia ya Mkristo isimikwe Biblia Takatifu katika utaratibu utakaoratibiwa kiparokia na wanafamilia wahimizwe kulisoma Neno la Mungu katika sala ya familia nyumbani.

 

  1. Kianzishwe chama cha utume wa Biblia maparokiani ili kutoa elimu ya Biblia na kuzima kiu ya watu kujua Neno la Mungu kwa ufasaha.

 

  1. Parokiani wawepo wahudumu wa Neno watakaokuwa wanasoma masomo wakati wa Misa.  Hawa waandaliwe na wasimikwe na wawe na mavazi maalumu.

 

Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (JNNK)

 

54.  JNNK ni mahali ambapo Kanisa kama familia ya Mungu inaishi.  Ni Jumuiya ambazo watu wanasaidiana katika kumtafuta kwao Mungu kwa pamoja katika maisha ya kila siku.  Ni njia ambayo kwayo Kanisa linaishi katika mfumo unaowagusa waamini katika furaha na majonzi ya watu wanapoishi pamoja na ni njia ambayo kwayo waamini wanawezeshwa kutambua fumbo la Kristo aliyeko katikati yao na anayeonekana kwao kwa njia na sura ya jirani.

 

55.   Tangu mwaka 1976, Maaskofu Katoliki wa AMECEA waliamua kwamba JNNK ziwe vitovu vya uinjilishaji ndani ya Kanisa.  Walitambua kuwa JNNK ni shule ya Neno la Mungu, ni mahali ambapo waamini wanaweza kulimwilisha Neno hili katika uhalisia wa maisha na vipaumele vyao, ni mahali pa kukuza na kulea miito mitakatifu na ni jukwaa la huduma ya kidugu na mapendo kwa jirani.

 

56.   Maisha katika JNNK ni maisha yanayoweza kumsaidia mtu kukua kiroho na kukuza uzima wa kimungu ndani yake.  Ndiyo maana tunaziweka JNNK kuwa ni mojawapo ya vipaumbele cha uchungaji katika Jimbo letu.  Hapo hapo tunaazimia kuhakikisha kuwa JNNK zinajengewa mazingira mazuri ili kweli ziwasaidie waamini kukua kiroho na kukuza uzima wa kimungu ndani yao.  Hivyo tunaagiza kuwa:

 

  1. Idara ya Kichungaji iwe na Padre mratibu wa JNNK kijimbo.  Huyu ahusike kushughulikia ustawi, changamoto na maendeleo ya JNNK Jimboni.

 

  1. Uandaliwe mapema mwongozo kuhusu JNNK.  Pamoja na mengine, mwongozo huu ufafanue yahusuyo muundo, sala, fedha na huduma za jamii katika JNNK.

 

  1. Maombi yote ya huduma za sakramenti yapitie katika JNNK.

 

UTAMADUNISHO

 

57.   Tangu mwanzo wake, Kanisa limekubali kupokea tunu za tamaduni mbalimbali na kuziingiza katika maisha yake.  Umwilisho ndilo fumbo lililo msingi thabiti wa kazi ya utamadunisho.  Neno wa Mungu alichukua hali kamili ya kibinadamu akaifanya iwe yake pasipo kuacha kuwa Mungu.  Kwa njia hii aliinua ubinadamu wetu, papo hapo akatushirikisha umungu wake.  Kwa mithili ya umwilisho, tunu bora za utamaduni wa watu zinapoingiliana na kweli za Injili, tunu hizo zinasafishwa na kutakaswa zipate kuwa sehemu ya Ukristo wenyewe.  Kwa hiyo utamadunisho ni muingiliano wa aina mbili:

 

  1. Mambo mazuri ya utamaduni yanatakaswa na kuhuishwa na Ukristo.

 

  1. Thamani za Ukristo zinapenyezwa katika tamaduni za watu.

 

58.   Utu wa mtu huonekana katika utamaduni.  Kwa jinsi dhana ya utamaduni ilivyo pana vivyo hivyo na dhana ya utamadunisho.  Utamadunisho unagusa utu wa Mkristo katika ujumla wake na maisha yake yote.  Ni kwa bahati mbaya kwamba mara nyingi umehusishwa zaidi katika ibada na maadhimisho ya Sakramenti na kuacha nyanja nyingine za maisha ya Mkristo ambazo ni muhimu pia ili kuupa utamadunisho maana kamili.

 

         Katika Sinodi yetu tumelitazama suala la utamadunisho katika upana wake.  Tumeona wazi kuwa lipo hitaji la kuziingia tamaduni za maisha yetu na kuziinjilisha na lipo hitaji pia ya kuitazama imani yetu katika mwanga wa tamaduni zetu ili kuitamadunisha.  Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa yapo mazoea mema katika tamaduni zetu ambayo yanaweza kutusaidia kuiishi vema zaidi imani yetu.  Hali kadhalika yapo mazoea mabaya katika tamaduni zetu ambayo yasipoondolewa yanaweza kuififisha imani yetu.

 

59.   Kwa kufuata nyayo za mababa wa Sinodi ya kwanza ya Afrika juu ya utamadunisho, nasi tunapenda utamadunisho ufanyike kwa umakini mkubwa.  Ufanyike utafiti wa kina na makini ili kuchuja na kupembua ni yapi yafaayo kwa imani yetu.  Nyanja zinazoweza kuhusishwa katika tafiti hizo ni pamoja na zifuatazo:

 

  1. Maisha ya jamii: undugu, uwajibikaji na mshikamano katika familia na ukoo, miiko na vitu vinvyolinda tunu njema katika familia na ukoo n.k.

 

  1. Thamani ya maisha ya mwanadamu: utakatifu wake, kulindwa kwake, dhana ya kifo, maradhi na fanaka katika maisha.

 

  1. Ndoa, uzazi, thamani ya watoto, malezi, mahusiano, jinsi, jinsia n.k.

 

  1. Ibada: mahali pa ibada, mavazi ya ibada, wahusika wa ibada, nafasi ya makundi mbalimbali ya jamii katika ibada (watoto, akina mama, akina baba, wazee), sadaka katika ibada, n.k.

 

60.   Ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na mazingira mazuri ya kufanya tafiti za kina kuhusu utamadunisho, tunaazimia kuwa iundwe Tume Jimbo ya Teolojia.  Tume hii itakuwa chini ya Idara ya Kichungaji na itahusika kuratibu tafiti zote kuhusu utamadunisho.  Pamoja na hayo tume hii itashughulikia yote yahusuyo teolojia jimboni: tafiti, semina, tafsiri ya mafundisho na machapisho.

SURA YA TATU:

 

USHUHUDA WA IMANI KWA MATENDO

 

Utangulizi

 

61.   Mwaliko wa Kristo kwa wanafunzi wake; “Ninyi ni nuru ya ulimwengu; … nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”  (Mt. 5:14, 16) ni wa maana sana katika maisha ya Mkristo.  Humwalika kutambua kuwa matendo na maisha yake yanapaswa daima kuwa ni ushuhuda wa Imani yake.

 

         Tukiongozwa na mwaliko huo tunapenda matendo yenu katika kila nyanja ya maisha yazidi kuwa ushududa wa imani yetu.  Tuishuhudie imani yetu katika kukuza Haki na Amani, katika mahusiano na watu tunaoishi nao, katika Huduma tunazozitoa kwa Jamii inayotuzunguka na katika kuliendeleza na kulitegemeza Jimbo letu.

 

HAKI NA AMANI

 

62.  Utangazaji wa haki na amani ni sehemu ya msingi katika uenezaji wa Injili.  Kupinga na kuyakataa yale yote yanayodhalilisha utu wa binadamu, kupinga maovu na yale yote yasiyo ya haki ni sehemu ya utume wa uenezaji wa Injili na unabii wa Kanisa.  Kanisa halina tu wajibu wa kutangaza haki na amani bali pia linao wajibu na jukumu la kushiriki kikamilifu katika kuleta haki na amani katika jamii kwa kutumia njia zote zinazowezekana.

 

         Amani ni matokeo ya haki na itapatikana ikiwa watu wote wanaishi vile Mungu anavyotaka.  Amani huja polepole kadiri ya watu wanavyoshinda maelekeo yao mabaya na wakubwa wanatumia utaratibu bora katika kutawala.  Zaidi ya hayo amani inataka watu washirikiane katika utendaji wao, wapendane na kuheshimiana kama vile ndugu  (Vat. II, GS. 78).

 

         Neno “haki” humaanisha stahili ya mtu kupata kutoka kwa au kupewa au kutendewa jambo fulani na mtu mwingine au jamii anamoishi.  Pia haki inaweza kutokana na sheria ya nchi, mila, haki za msingi, mahusiano ya kawaida baina ya wananchi katika jamii inayohusika au mikataba.  Hatuwezi kuzungumzia kuhusu haki bila kueleza kuhusu wajibu.  Neno wajibu lina maana ya kupasika kutekeleza shughuli au jambo fulani kwa kujituma bila ya kungoja kusukumwa au kusimamiwa.  Kwa maana nyingine kuwajibika ni kule kukubali kutekeleza jambo fulani ulilokabishiwa au kupasika kwa hiari, uadilifu na kwa ukamilifu.  Hakuna haki bila wajibu wake.

 

         Amani humaanisha hali ya watu kuishi bila mafarakano.  Haki zote za msingi za binadamu zinakaziwa na kuchukuliwa kama ndio mhimili wa amani.  Amani inaweza kudumishwa iwapo tu haki itazingatiwa.

Elimu ya Haki na Amani Jimboni Musoma

 

63.    Kutoa elimu ya Haki na Amani ni mojawapo ya namna ifaayo ya kutekeleza wajibu wa kutangaza na kushiriki kikamilifu kustawisha Haki na Amani ndani ya mipaka yetu na kwingineko.  Hivyo tunaazimia kuwa na mikakati ya kuwawezesha waamini kupata uelewa kuhusu haki zao ambazo zinapatikana katika sheria mbalimbali kuanzia na katiba ya nchi na Sheria Kanuni za Kanisa ambazo ni sheria msingi inayoainisha haki mbalimbali za raia na waamini kwa ujumla.  Tume ya jimbo ya haki na amani itahusika kuratibu utoaji wa elimu hii.

 

         Katika kutoa elimu hii ni bora msisitizo wa pekee uwekwe katika maeneo ambamo migogoro huibuka kwa wingi.  Haya ni pamoja na umiliki wa ardhi, ajira, mahusiano kazini, watoto, ndoa na mirathi.

 

Mfumo wa Kanisa Kulinda Haki zake Kisheria

 

64.   Kanisa huwa na taratibu za kulinda haki zake na za waamini wake kisheria.  Hutunza nyaraka za umiliki wa mali zinazohamishika na zisizohamishika pamoja na nyaraka za kumbukumbu mbalimbali kuhusiana na haki za waamini.  Tunakiri kuwa katika baadhi ya taasisi zetu ulegevu katika kulinda haki hizi umesababisha upotevu wa baadhi ya haki zake kisheria.  Ukosefu wa hati na nyaraka za kumiliki ardhi, kwa mfano, kimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi na pengine kusababisha kupoteza ardhi za Kanisa.  Kwa jinsi hii tunaazimia na kuhimiza yafuatayo;

 

  1. Kila ofisi katika ngazi ya Jimbo, Parokia na taasisi iwe na mfumo wa kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu zote muhimu za kisheria kuhusiana na ofisi hiyo.

 

  1. Kila parokia iwe na vitabu vyote vinavyotakiwa katika kutunza taarifa za waamini na kumbukumbu za sakramenti na za familia.  Desturi ya vitabu hivi kukaguliwa na kusainiwa na Askofu wakati wa ziara za kichungaji maparokiani ipewe mkazo zaidi.

 

Ajira katika Taasisi za Jimbo

 

65.    Kutangaza na kushiriki kuleta haki na amani ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya ajira katika taasisi zetu za Jimbo yanaakisi tunu hizo.  Hivyo tunaazimia kuwa iandaliwe sera ya ajira katika taasisi za Jimbo kuanzia ngazi ya parokia.  Hali kadhalika tunaazimia kuunda bodi ya ajira na ya usuluhishi ili kushughulikia masuala ya waajiriwa katika taasisi hizo.

 

MAHUSIANO

 

66.  Jimbo letu lipo katika mkoa ambao ni miongoni mwa mikoa yenye dini na madhehebu mengi hapa nchini.  Hali hii inaleta kuwa na mwingiliano mkubwa na watu wa dini na madhehebu mbalimbali katika mazingira tunayoishi na katika taasisi na maeneo mengine ya kijamii.  Mwingiliano huu upo hata katika familia zetu katika ndugu na jamaa tuanoishi nao.

 

         Ushuhuda wa imani kwa matendo unapaswa kuonekana bayana katika namna tunavyohusiana sisi kwa sisi na namna tunavyohusiana na wenzetu wa imani mbalimbali tunaoishi nao katika mazingira yetu.  Historia inatuonesha kuwa panapokosekana uhusiano mzuri huwa ndio mwanzo wa chokochoko na machafuko ya kidini ambayo huiathiri jamii kwa kiasi kikubwa.  Tunaamini kuwa kama vile ujio wa Kristo ulivyotangaza “utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema” (Lk. 2:14), hali kadhalika maisha ya ushuhuda wa imani kwake yataendelea kumpa Mungu utukufu na kuleta amani duniani.

 

         Ili kuboresha mahusiano hayo na ili kuendelea kuishi maisha ya ushududa wa imani yetu kwa matendo katika mazingira yenye mchanganyiko mkubwa wa dini na madhehebu, tunapenda kuainisha sera itakayokuwa ikituongoza kama ifuatavyo:

 

Mahusiano Baina ya Wakatoliki wao kwa wao

 

Uhusiano katika Familia na Jamii

 

67.   Familia za Kikristo huitwa Kanisa la Nyumbani kwa sababu hufanya ufunuo na udhihirisho maalum wa ushirika wa Kanisa.  Ni familia za imani, za matumaini na za mapendo.  Uhusiano ndani ya familia huleta udugu wa hisia, upendano na moyo wa ushirikiano utokanao hasa na kuheshimiana kwa wanafamilia.41  Kila familia ya Kikristo ijitahidi kudumisha mahusiano mazuri, kuishi mafundisho na maadili ya Kikristo na ifuate desturi njema za Kikristo katika familia.

 

68.   Familia za Kikristo ziendeleze ushirikiano mwema katika jamii katika matukio na maisha mazima ya jamii iliyomo.  Zishirikiane katika matukio ya furaha na huzuni, katika kuonesha mshikamano kwa mafaa ya jamii nzima na katika matukio mbalimbali ya kibinadamu kwani “furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, yote ni furaha na matumaini, uchungu na faadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.” Ziungane na makundi yoyote ya kijamii yenye nia na njia njema za kuinua hali na hadhi ya binadamu kiuchumi, kisiasa, kijamii na kadhalika.

 

69.   Familia za Kikristo ziwe mstari wa mbele katika kuepuka, kupinga na kutokomeza mazoea mabaya, imani, mila na mafundisho potofu yanayoendeleza chuki, visasi, ubinafsi, siasa chafu na yote yanayowagawa watu kwa misingi ya dini, kabila na mengineyo.

 

Uhusiano kati ya Waamini na Viongozi wao wa Dini

 

70.   Uhusiano mzuri kati ya waamini na viongozi wao wa dini ni kiini cha utendaji wenye ufanisi na utekelezaji mwema wa utume ambao Kristo ameliachia Kanisa lake.  Viongozi hawa wanapotekeleza vema utume wao hudhihirisha sura ya Kristo mwenyewe anayetenda kazi ndani yao na pamoja nao.

         Katika maeneo ya kiutendaji ambapo uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji vimekosekana, daima mahusiano hayakuwa mazuri na sura ya Kristo katika utendaji imefifia.  Hivyo katika sera hii, ili kulinda tunu hizo na nyinginezo zitakazoboresha mahusiano baina ya waamini na viongozi wao wa dini, tunaazimia yafuatayo:

 

  1. Kabla ya kusimikwa, viongozi wa ngazi mbalimbali katika taasisi na parokia zetu wanapaswa kupewa semina ya Uongozi katika Kanisa.

 

  1. Uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji viwe kipaumbele katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya uongozi katika taasisi na parokia zetu.

 

  1. Tume ya Haki na Amani ihusike moja kwa moja katika kuepusha na kusuluhisha migogoro mbalimbali inayozorotesha mahusiano kati ya waamini na viongozi wao.

 

Uhusiano kati ya Parokia na Taasisi za Kanisa zilizoko Parokiani

 

71.   Taasisi mbalimbali za Kanisa zinazojihusisha na Elimu, Afya na huduma nyinginezo za jamii huwa daima ndani ya mipaka ya kijiografia ya parokia.  Hali halisi inaonesha kuwa kukosekana kwa mwongozo wa kijimbo juu ya mahusiano kati ya parokia na taasisi zilizo ndani ya mipaka yake kumezorotesha mahusiano kwa baadhi ya parokia na taasisi, hivyo tunaagiza kuwa uandaliwe mwongozo wa kijimbo utakaoainisha mahusiano ya kiutendaji na uwajibikaji katika eneo hilo.

 

Mahusiano na Madhehebu ya Kikristo na Wasio Wakristo

 

72.    Kinachotuunganisha Wakatoliki na Wakristo wa madhehebu mengine ni imani kwa Yesu Kristo.  Kristo alianzisha Kanisa moja na pekee lakini kwa sababu za kibinadamu madhehebu mengi ya Kikristo yemeibuka na yanazidi kuibuka siku hata siku.  Kristo mwenyewe alisali ili wote wanaomwamini wawe na umoja (rejea Yoh. 17:20 – 21).  Kwa sababu ya nia hii ya Kristo na imani moja kwake ambayo Wakristo wote wanayo, zimeundwa harakati ziitwazo Ekumene ili kurejesha umoja kati ya wote wanaomwamini Kristo.

 

73.    Pamoja na Wakristo wa madhehebu mengine, tunao pia ndugu zetu wasio Wakristo.  Miongoni mwao wamo wafuasi wa dini za asili, Wahindu, Wabudha, Waislanu na Wasabato.  Kanisa hutambua mema ya kiroho na ya kimaadili, na tunu za kijamii na za kitamaduni ambazo hupatikana kati ya wasio Wakristo.  Ndiyo maana daima hutualika kwa busara na mapendo, kwa njia ya dialojia na ushirikiano nao kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha ya Kikristo.

 

         Kanisa hutualika kutambua kuwa sisi sote ni jumuiya moja.  Asili yetu ni moja, Muumba wetu ni mmoja na tena kikomo chetu ni kimoja tu, yaani Mungu ambaye maongozi yake, ushuhuda na wema wake na azimio lake la wokovu yawaelekea watu wote hadi wateule wapate kukusanyika katika Mji Mtakatifu ambao utukufu wa Mungu utautia nuru na ambapo mataifa watatembea katika nuru yake.

 

74.  Kwa kufuata misingi iliyokwisha kuwekwa tayari na Kanisa na kwa kuzingatia mahitaji yetu mahalia, ili kuendeleza mahusiano mazuri kati yetu na waamini wa mashehebu mengine ya Kikristo na pia kati yetu na wasio Wakristo tunaazimia yafuatayo:

 

  1. Tuendelee kushirikiana na kufanya kazi pamoja katika shughuli zote za kijamii na za kibinadamu zinazolenga kuinua hali na hadhi ya binadamu kama anavyokusudia Mwenyezi Mungu muumba wetu sote.

 

  1. Harakati za Ekumeni na Dialojia na Wasio Wakristo zikuzwe.  Idara ya Ekumeni na ya Dialojia na Wasio Wakristo ihakikishe kuwa miongozo na misingi ya Kanisa juu ya Ekumeni na Dialojia inafahamika kwa waamini wote ili wanapoingia katika harakati hizo misingi ya Kikatoliki isimezwe.

 

  1. Katika Juma la Sala kwa ajili ya Umoja wa Wakristo (Januari 18 – 25) kila mwaka, pawepo na maadhimisho, kijimbo na kiparokia, yanayoratibiwa na Idara ya Ekumene.

 

MAENDELEO NA KUJITEGEMEA

 

Kanisa Mahalia

 

75.  Kanisa mahalia huwa na sifa kuu tatu: kujiongoza, kujieneza na kujitegemea.  Hujiongoza kwa kuwa na uongozi wake wa Askofu, mapadre, watawa na walei katika nafasi zao halisi, hujieneza kwa kushika hatamu za uinjilishaji wa kina kwa kuwa na roho ya utume na hujitegemea kwa kutambua mahitaji yake na kuwa tayari, kwa kushirikishana majaliwa ya hali na mali, kuendesha shughuli za kichungaji na kijamii.  Kwa kujitegemea na kushughulikia maendeleo yake, Kanisa mahalia hutoa ushuhuda kamili wa kuliakisi na kulijenga Kanisa zima – mwili wa fumbo wa Kristo.

 

         Katika Jimbo letu tunadhamiria kuimarisha juhudi za kujipatia maendeleo na kujitegemea kama alama ya ushuhuda wa ukomavu wetu kiimani na ukomavu kama Kanisa mahalia.  Ndio maana katika Sinodi hatukukosa nafasi ya kuingalia hali yetu, mintarafu maendeleo na kujitegemea, kuitathmini na kuipangia mikakati.

 

Hali Halisi

 

76.   Tangu kuanzishwa Jimbo la Musoma mwaka 1957, juhudi kubwa imefanywa ili Jimbo lijitegemee na lijiendeleze.  Juhudi hii ni dhahiri katika vitega uchumi na taasisi za kimaendeleo zilizoanzishwa jimboni kwa nyakati mbalimbali.  Hata hivyo kwa muda mrefu huhudi hizi zimefanikiwa sambamba na upatikanaji wa ruzuku na ufadhili kutoka mashirika mbalimbali ya wafadhili wa nje.  Kwa sasa ruzuku na ufadhili huu unapungua kadiri siku zinavyoenda.  Kupungua huku ni matokeo ya sababu nyingi zikiwemo kupungua kwa wachangiaji wa miradi, kupungua kwa wamisionari waliokuwa kiungo kikubwa cha upatikanaji wa misaada lakini pia ni kwa sababu ya mashirika hayo kuhamisha uelekeo wa ufadhili.

 

         Hali hii inaonesha kuwa sasa tunahitaji kujenga kwa kasi zaidi ndani yetu moyo wa kujitegemea na kushughulikia wenyewe maendeleo yetu.  Jimbo letu si changa tena kwani tayari tumekwisha kuadhimisha miaka 100 ya Ukristo na miaka 50 ya kuwa Jimbo.  Moyo huu tutazidi kuujenga kwa kuelimishana na kuhamasishana.  tena tunahitaji kufanya juhudi za pekee za kuwafanya waamini washiriki katika mipango endelevu ya kiuchumi kwa ajili ya Jimbo letu.

 

Kupunguza Utegemezi wa Nje

 

77.   Kujenga moyo wa kujitegemea na kushughulikia wenyewe maendeleo yetu ni suala linalopaswa kwenda sambamba na kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili wa nje.  Kama vile katika familia mtu huonesha ukomavu anapoanza kujitegemea, hali kadhalika kama Kanisa mahalia tutaonesha ukomavu wa kiimani kwa kujitegemea wenyewe.

 

         Kijimbo tumekwisha kupiga hatua nzuri mintarafu kujitegemea.  Waamini wamekweisha kufanikiwa kuunganisha nguvu zao na kuchangia ujenzi wa makanisa, mashule, vituo vya afya na taasisi nyingine za Kanisa.  Uchangiaji huu daima umekwenda sambamba na kuwategemeza wahudumu wa daraja, watawa na makatekista katika parokia zetu pamoja na kutegemeza taasisi zetu mbalimbali.  Hata hivyo juhudi zaidi inahitajika bado ili tufikie kiwango cha juu katika kujitegemea.

 

78.  Tumeainisha mikakati mbalimbali ya kutusaidia kufikia kiwango cha juu cha kujitegemea.  Mikakati hiyo ni kama ifuatavyo:

 

  1. Kujenga uwezo kwa watu binafsi na vikundi kwa kutoa elimu ya ujasiriamali na kuwawezesha kutumia fursa zilizopo ili kujiongezea kipato.  Hii itakwenda sambamba na kuwaunganisha katika vikundi mbalimbali vya kimaendeleo kama SACCOS, VICOBA na vinginevyo kadiri ya mazingira na uhitaji.

 

  1. Kuimarisha miradi yetu ili iweze kujiendesha na isaidie uendeshaji wa huduma nyingine kijimbo.  Tutaimarisha miradi kwa kuwa wabunifu, kwa kuboresha huduma zitolewazo na kwa kuboresha miundombinu ili iendane na wakati na kustahimili ushindani wa watoa huduma wengine.  Hali kadhalika tunadhamiria kuimarisha utaratibu wa kutathmini miradi hiyo na kuhakikisha kuwa wanaopewa kuiendesha ni miongoni mwa wenye uwezo wa kitaaluma na kimaadili.

 

  1. Kukuza moyo wa majitoleo kwa waamini.  Ni ukweli usiopingika kuwa uasilia wa Kanisa katika suala la mapato upo katika majitoleo.  Majitoleo ni tendo la imani na ni wajibu pendwa unaotokana na ukomavu wa kiimani (rejea 2Kro. 9:6).  Misaada ya wafadhili wa nje ni matokeo ya majitoleo ya waamini wa huko.  Hatuna budi nasi kukuza moyo huu ili kulitegemeza Kanisa la nyumbani.  Hivyo waamini waendelee kutolea kwa ukarimu sadaka, matoleo, zaka, ada ya stola (shukrani ya huduma mbalimbali ya sakramenti na nyinginezo) na michango kadiri ya taratibu halali za kikanisa.

 

  1. Kuimarisha mfuko wa “Mshikamano”.  Mfuko huu una lengo la kukusanya fedha kwa kiwango kilichoainishwa kwa mwaka kutoka kwa kila mbatizwa na kuziweka katika “kapu moja” kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo.

 

  1. Kutuma miradi, parokia na taasisi zetu kuchangia uendeshaji wa ofisi ya askofu kutoka sehemu ya mapato yao.

 

Kuwategemeza Wahudumu

 

79.  Wajibu wa kuliendeleza na kulitegemeza Kanisa mahalia huenda sambamba na wajibu wa kuwategemeza wahudumu wake.  Tunamshukuru Mungu kwamba katika Jimbo laetu suala la kuwategemeza wahudumu wa daraja limekwisa kuwekewa utaratibu.  Pamoja na taratibu zinazoweza kuwapo kiparokia, katika ngazi ya Jimbo wahudumu wa daraja hutegemezwa na waamini wanaowahudumia siku ya kubariki mafuta matakatifu.  Tunahimiza tu kwamba utaratibu huu uendelezwe na uzidi kupewa mkazo ili wahudumu hawa wasitindikiwe mahitaji yao muhimu.

 

         Pamoja na wahudumu wa daraja, tunao utaratibu wa kulitegemeza Shirika la Kitawa la Jimbo (Immaculate Heart Sisters of Africa) katika dominika iliyo katibu na tarehe 29 Julai iliyo sikukuu ya Mtakatifu Marta, Msimamizi wa Shirika.  Tunahimiza kuwa utaratibu huu utiliwe mkazo katika parokia zetu na ufanyike kwa uratibu mzuri wa viongozi wa shirika na maparoko.

 

         Makatekista walei kwa nafasi na utendaji wao huunganika kwa karibu sana na wahudumu wa daraja na watawa katika shughuli za uinjilishaji parokiani.  Kwa kuwa hatujawa na mfumo mmoja kijimbo kwa ajili ya kuwategemeza makatekista, tunaagiza kuwa Kamati ya Fedha Jimbo pamoja na Idara ya Katekesi waandae mfumo utakaotumika kuwategemeza makatekista walei.

 

Maazimio

 

80.   Baada ya kuiangalia hali yetu, kuitathmini na kuipangia mikakati ya kulitegemeza na kuliendeleza Jimbo letu, tunaazimia yafuatayo.

 

  1. Kamati ya Fedha Jimbo iimarishwe na iwe na jukumu la kubuni vyanzo vipya vya mapato jimboni kulingana na fursa tulizonazo.

 

  1. Kamati ya Fedha kwa kushirikiana na vyombo husika iandae viwango vya Mchango wa Mshikamano, Shukrani kwa Sakramenti, Zaka na Huduma nyingine za Kanisa.  Viwango hivi viwe vinaboreshwa kulingana na wakati.

 

  1. Taasisi zetu za Elimu, Afya na miradi mbalimbali ichangie maendeleo ya Jimbo kwa kutoa 5% ya mapato yao kwa mwaka.  Hali kadhalika Parokia zetu zichangie maendeleo ya Jimbo kwa kutoa 15% ya mapato yao kwa mwaka.

 

  1. Taarifa ya michango iliyoainishwa kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo iwasilishwe kwa hadhara katika Sala ya Jimbo tare 3 Oktoba kila mwaka.

 

  1. Ili kukuza uwajibikaji, kila parokia na Taasisi itoe bajeti na taarifa ya mapato na matumizi kwa mwaka.  Taarifa hii ijadiliwe katika vikao vya dekania na vya wakuu wa dekania jimboni.

 

  1. Kwa kuwa maendeleo halisi ya Kanisa hayapimwi kwa nyanja moja tu ya kiuchumi, shughuli zote za kimaendeleo jimboni lazima ziwe na mwelekeo wa kichungaji.

 

MIITO YA UPADRE NA UTAWA

 

81.   Ushuhuda wa Imani kwa Matendo hutolewa pia kwa miito ya Upadre na Utawa ambayo baadhi ya waamini huiitikia.  Hawa hutolea maisha yao yote kumshuhudia Kristo “… ambaye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”  (Mk. 10:45).  Pamoja na kuwa mashuhuda kwa mafundisho na maadhimisho ya kiliturujia, mapadre na watawa hutoa ushuhuda kwa nadhiri na mtindo wao wa maisha ufuasao mashauri ya Injili kwa namna ya pekee kabisa.  Kanisa mahalia linahitaji kuwa na watu hawa kwa wingi ili liendelee kujieneza na hivi kutekeleza utume wake.

 

Mwitikio ma Miito ya Upadre na Utawa Jimboni

 

82.   Katika Jimbo letu, mwitikio wa miito ya upadre na utawa bado ni mdogo.  Kwa hakika tunahitaji kuzidi kumwomba Bwana wa mavuno ili aongeze watendakazi katika shamba lake (rejea Lk. 10:2).  Sala yetu hii inapaswa kusindikizwa na mikakati madhubuti inayoonesha uthabiti wa nia yetu ya kuongeza mwitikio katika miito hii.  Tunapaswa kuwa na mikakati kwa sababu upembuzi wa sababu zinazopelekea mwitikio kuwa mdogo unaonesha pia kuwa kama Jimbo hatujatoa hamasa ya kutosha na hatujaimarisha mikakati yetu katika suala hili.

 

         Kwa sababu hiyo tunaazimia kuwa:

 

i.Suala la kuhamasisha miito si suala la Mkurugenzi wa Miito pekee.  Ni kulifanya wajibu wetu sote wanafamilia ya Mungu jimboni Musoma.  Hivyo Kamati ya Miito Jimbo pamoja na majukumu yake ihusike kuratibu mpango mzima wa uhamasishaji wa miito jimboni.  Hali kadhalika kila parokia iwe na kamati ya miito ili kuratibu shughuli hizi kiparokia.

 

ii.Kwa kuwa chimbuko la miito yote ni familia zinazotoa malezi bora na zilizo na ukarimu wa kiimani.  Tutazidi kuwahimiza wazazi kuzitunza vema familia zao na kukazania sana malezi bora kwa watoto ili kutoka humo Kanisa liwapate wengi wanoitikia miito hii mitakatifu.

 

  1. Vyama vya miito maparokiani viimarishwe.  Katika parokia awepo Padre au mlezi anayefaa kwa kundi hili ili watoto na vijana wapewe mafundisho na walelewe vema ili wawe wakarimu katika kuitikia mwito wa Mungu.

 

  1. Kongamano la vijana (TYCS na VIWAWA) litakuwa pia jukwaa la kuwasaidia vijana kuisikiliza sauti ya Mungu na kuwahamasisha kujiunga na miito hii mitakatifu.

 

Nyumba za Malezi

 

83.  Miito ya upadre na utawa hulelewa katika vituo maalum viitwavyo Nyumba za Malezi.  Katika nyumba hizo, vijana wanaosikia kuitwa na Mungu hupokelewa, hufundishwa na hulelewa hatua kwa hatua kufuata sauti ya mwito wa Mungu.  Katika Jimbo letu tunavyo vituo vingi vya kuwaandaa vijana kwa miito hii mitakatifu ndani ya Jimbo na katika mashirika mbalimbali ya kitawa.

 

         Hitaji letu na hitaji la Kanisa zima ni kuona kuwa kazi ya malezi inafanywa kwa mshikamano na vituo hivi vinaandaa watu ambao kweli watakuwa mashuhuda wa Imani katika ulimwengu wa leo.  Kwa hiyo tunaazimia kuwa:

 

  1. Walezi katika vituo vya malezi wawe ni miongoni mwa wale walioandaliwa kwa kazi ya kulea.

 

  1. Nyumba zote za malezi zilizoko jimboni Musoma ziwe zinaandaa taarifa yao ya mwaka na taarifa hii ipelekwe kwa askofu.  Taarifa hii iwe inajumuisha mpango mzima wa malezi katika nyumba husika.

 

  1. Kamati ya Miito Jimboni iwe na utaratibu wa kutembelea vituo vyote vya malezi vilivyomo Jimboni Musoma walau mara moja kwa mwaka ili kujionea na kutoa taarifa kwa Askofu juu ya maendeleo ya vituo hivyo.

 

Kuchangia Gharama za Masomo na Malezi ya Walelewa

 

84.   Utaratibu wa waamini kuchangia gharama za masomo na malezi kwa walelewa si mgeni katika Jimbo letu.  Tangu zamani tumekuwa na utaratibu wa kuchangia chakula kwa walelewa walioko seminari yetu ndogo ya Makoko zoezi ambalo limewasaidia waseminaristi hao kupata masomo na malezi katika mazingira mazuri.  Tunahimiza kuwa utaratibu huu mzuri uendelee na uratibiwe vizuri.

 

          Aidha, tunavialika Vyama vya Kitume Jimboni kujipanga na kutoa michango yao ya hali na mali kusaidia Nyumba za Malezi zilizomo jimboni kwa utaratibu utakaowekwa na Kamati ya Miito kwa ushirikiano na uongozi wa Nyumba hizo walau mara moja kwa mwaka.

 

85.   Mafrateri wetu walioko seminari kuu watachangiwa kwa utaratibu maalumu.  Kwa muda mrefu ada za kuwasomesha mafrateri zilikuwa zinatoka Vatikano Roma katika kongregasio ya Uenezaji wa Injili.  Ruzuku hii imekuwa inapunguzwa siku hadi siku na kwa sasa ada yote inapaswa kutoka majimboni wanakotokea mafrateri wenyewe.  Baada ya kulitazama suala hili kwa kina tunaazimia kuwa ada hii ilipwe kutoka katika parokia na taasisi zetu.  Kila parokia na taasisi iwe na mfuko wa ada ya mafrateri.  Kiwango ambacho kila parokia na taasisi itachanga kwa mwaka kitakuwa kinaainishwa na Kamati ya Fedha kwa ushirikiano na Idara ya Miito.

SURA YA NNE:

 

CHANGAMOTO ZA NYAKATI ZETU

 

Utangulizi

 

86.   Tunaishi katika ulimwengu ambao daima hubadilika katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.  Hata sasa tunashuhudia mabadiliko makubwa na ya haraka yanayosababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.  Mabadiliko yote haya humrudia mwanadamu mwenyewe iwe ni kwa namna chanya au namna hasi nayo huathiri mawazo yake, maazimio yake binafsi na ya kijamii, namna ya kufikiri na kutenda na namna anavyohusiana na vitu na watu.

 

         Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatukumbusha kuwa kila mara mageuzi yanapofanyika katika harakati za maendeleo, huambatana na matatizo makubwa na tena inaonekana kuwa kadiri binadamu anavyoukuza uwezo wake ndivyo anavyozidi kushindwa kuuweka chini ya mamlaka yake.

 

87.   Kama Wakristo, wajibu wetu ni kuendelea kushuhudia imani kwa matendo yetu na kuendelea kuwa sauti ya kinabii ya Mwenyezi Mungu katikati ya mabadiliko haya yanayoukumba ulimwengu, mabadiliko ambayo mara nyingi huwa changamoto kwetu kuishuhudia imani na kutoa sauti ya kinabii.  Hivyo tunaona kuwa tunao wajibu wa kudumu wa kuchunguza alama za nyakati zetu na kuzifafanua katika mwanga wa Injili ili kwa mwanga wa Roho Mtakatifu tuendeleze kazi ya Kristo mwenyewe ambaye alikuja ili kuushuhudia ukweli, tena kukomboa wala si kuhukumu na kutumikia wala si kutumikiwa.

 

         Tukisukumwa na imani ambayo kwayo tunaamini kuwa tunaogozwa na Roho Mtakatifu anayeujaza ulimwengu, na kwa kuyashiriki matukio, madai na matarajio pamoja na wanadamu wote wa nyakati zetu tunajibidisha ili kutambua zipi ni ishara halisi za uwepo wa Mungu au za mpango wake katika nyakati zetu.

 

         Katika mwanga huo tunaazimia kuimarisha misingi katika maeneo ya kijamii tuliyoyapa kipaumbele kwani “kama misingi ikiharibika, mwenye haki atafanya nini?” (Zab. 11:3).  Tunaamini kuwa ni kwa uimara wa misingi hiyo tunaweza kupita salama katika changamoto za nyakati zetu na kuendelea kuishuhudia vema imani kwa matendo na maisha yetu yote.  Maeneo hayo ni katika Familia, Maadili, Utandawazi, Jinsia na Mazingira.

 

Utume wa Ndoa na Familia

 

88.    Familia ni chembe ya kwanza katika maisha ya jamii ina umuhimu wa pekee katika maisha na ustawi wa Kanisa na jamii kwa ujumla.  Ustawi wa mtu binafsi na wa jamii ya kibinadamu na ya Kikristo hutegemea sana ustawi wa maisha ya ndoa na familia.  Tunaamini kuwa hata kama jamii itashambuliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa, inaweza tu kubaki imara kama inaundwa na familia imara.

 

         Familia imara na bora huundwa na ndoa bora iliyo katika mpango wa Mungu.  Hizi hazipatikani hivi hivi tu bali zinapaswa kuhimizwa, kulelewa, kusaidiwa na kukingwa na hatari mbalimbali ambazo daima huzisonga.  Katika misingi hii, tunaazimia kuanzisha utume maalum utakaoitwa “Utume wa Familia” ili kuzipa familia zetu misaada mingi ya kichungaji kuzisaidia ndoa na familia zetu kupita salama katika changamoto za wakati.  Aidha tunarudia msisitizo katika vipengele kadhaa vya mafundisho ya Kanisa juu ya ndoa na familia kama ifuatavyo:

 

  1. Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia yasisitizwe.  Maandalizi ya ndoa yafanywe kwa umakini na wachumba waandaliwe kwa kupewa mafundisho kadiri ya miongozo iliyopo.

 

  1. Yaandaliwe makongamano na semina mbalimbali kuhusu Ndoa na Familia katika Parokia zetu.

 

  1. Vijana waandaliwe vya kutosha katika kuchagua wachumba na kuingia katika maisha ya ndoa.

 

Maadili

 

89.  Maadili kwa Mkristo ni kuishi kadiri ya miongozo iliyofunuliwa na Mwenyezi Mungu na kama avyofundisha Yesu Kristo.  Katika nyakati zetu kumekuwa na kilio kikubwa kuhusu mmomonyoko wa maadili katika jamii.  Sinodi inaguswa na kilio hiki na inaona inao wajibu wa kuweka wazi na kuagiza yafuatayo ili kujenga misingi imara ya maadili katika jamii yetu:

 

  1.  Jukumu la kulinda maadili ni la Jamii na Kanisa zima.  Kila mmoja ajione anao wajibu kwanza wa kuishi maadili mema na pili kusimamia maadili mahala alipo kulingana na nafasi yake.

 

  1.  Wazazi katika familia wahimizwe kuzingatia maadili mema katika kulea watoto na wao wenyewe wawe mfano wa kuishi maadili mema.

 

  1.  Ziundwe kamati za malezi na maadili katika Halmashauri za walei kuanzia ngazi ya JNNK hadi ya Jimbo.

 

  1.  Taasisi zetu zitambulike pia kwa kuwa kielelezo cha maadili mema.

 

  1.  Vyama vya kitume, vya malezi ya watoto, utoto Yesu, Wito na vijana, TYCS, VIWAWA, viwe vikundi mahususi vya kutoa mafundisho ya makuzi kiimani na kimaadili .

 

 

Utandawazi

 

90.   Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, dunia inafanywa kuwa kama kijiji.  Mabadiliko makubwa yanashuhudiwa katika mifumo ya biashara, siasa, utamaduni, miundombinu na mawasiliano.  Kwa jinsi hiyo jamii kubwa ya watu sasa inakimbizana na kasi ya mabadiliko hayo.

 

         Sinodi inatambua kuwa utandawazi si matokeo ya ghafla ya misukumo ya kihistoria isiyo na mwelekeo bali ni matokeo ya kiu hai na ya ndani kabisa ya wanadamu kukua na kupata muunganiko wa kiroho.  Pamoja na kuwa si sahihi kuuangalia tu katika ubaya wake, yafaa kujihadhari na madhara ambayo tayari yamekwisha kuikumba jamii yetu kutokana na kuuendea utandawazi kwa pupa.

 

         Hivyo tunasisitiza kuwa tuzienzi kanuni msingi na za kimapokeo hasa katika Liturujia, maadhimisho ya sakramenti na katika Ibada.  Wakati huo huo, kwa uangalifu mkubwa na halisi tukaribishe mabadiliko yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma katika taasisi zetu za elimu, afya na huduma nyingine za kijamii kama vile hosteli ili zitoe huduma kulingana na mahitaji na viwango vya juu kadiri ya wakati.

 

Ujinsia

 

91.   Jinsia ni hali ya nje ya maumbile ya kibinadamu inayomwezesha mtu kubeba wajibu mahususi wa kuendeleza kizazi kadiri ya mpango wa Mwenyezi.  Hali hiyo haikusudii kufisha, kushusha au kupuuza hadhi ya huyu na kuikweza hadhi ya yule.  Kule kuwa mtu mke au mtu mme hakupunguzi sura na mfano wa Mungu maana Maandiko yasema: “… kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” (Mwa. 1:27).

 

         Kwa hiyo namna au matendo yoyote yenye kutendwa kinyume na makusudi ya kazi ya Mungu ni tabia ambayo haivumiliki madhali yanakinzana na mpango wa Mungu na yanachochea ubaguzi na chuki miongoni mwetu.

 

92.    Ni ukweli usiopingika kuwa katika baadhi ya jamii ndani na nje ya Jimbo letu yako mambo mengi yenye kushusha au kufisha hadhi ya mwanamke kwa kumnyanyasa, kumnyima haki zake hata zile za msingi kama vile elimu na haki ya kumiliki mali.  Upo pia ukeketaji na biashara ya kuwatumia hasa mabinti wadogo kuuza miili yao kwa kisingizio cha ufadhili.  Tunakemea vikali matendo haya na mengine yote yanayofanana na haya.  Aidha tunaalika ushirikiano na asasi nyingine zenye nia thabiti za kutokomeza haya yote ili mwanadamu aendelee kuishi kwa hadhi na hali ile aliyokusudia Mwenyezi Mungu.

 

Mazingira

 

93.  “…. Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na chi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi …. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana …”.  (Mwa. 1:26, 31)  Ufunuo huu wa Neno la Mungu unatualika sisi sote kutwaa dhamana hiyo na kuwa mawakili wa uhifadhi mazingira.  Tunawajibika kutunza zawadi hii ya ulimwengu na vyote vilivyomo katika uzuri wake unaoakisi hekima na wema wake Mungu kwetu tukitambua kuwa dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana (rejea Zab. 8, 24:1-2).

 

94.   Kwa msukumo wa dhamana hiyo kutoka kwa Mungu, tunalaani matumizi mabaya ya kazi ya uumbaji ya Mungu kwa wale wote wenye kuharibu mazingira kwa kuharibu vyanzo vya maji, uvuvi haramu, kukata miti hovyo, uchimbaji usio rafiki kwa mazingira wa madini na mchanga pamoja upasuaji mawe na kokoto usiojali uasili wa mazingira yetu.  Kinyume na hayo, tunahimiza moyo wa kujali na kuhifadhi mazingira.  Tunaazimia kuwa kila parokia iwe na kamati ya uhifadhi mazingira.  Kamati hii ihusike kubuni na kuendeleza mbinu za utunzani bora wa mazingira katika parokia zetu.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.