2016-06-20 06:51:00

Mashuhuda wa Injili ya ukarimu!


Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumamosi jioni alitembelea Jumuiya ya Domenico Tardini, maarufu kama makazi ya Nazareth, kwa ajili ya wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu na wale wanaotoka katika familia maskini mjini Roma. Jumuiya hii ilianzishwa kunako mwaka 1946 na kwa mwaka huu inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutafakari pamoja na wanajumuiya hawa mfano wa Msamaria mwema kwa kuonesha jinsi ambavyo waamini wanapaswa kumwilisha imani yao katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu amewachambua wahusika wakuu katika mfano huu, ili kutaka kufahamu ni nani haswa aliyekuwa jirani ya yule mtu aliyeangukia kwenye mikono ya wanyang’anyi. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, hapa Msamaria mwema si Kuhani aliyekuwa anaharakisha kwenda kwenye Ibada, au Mwalimu wa Sheria ambaye hakupenda kuisaidia sheria kwa kutoa ushuhuda mahakamani, bali Msamaria ambaye aliyehesabiwa kuwa mdhambi na wala hakua ni sehemu ya watu wa Mungu. Huyu ndiye aliyemwonea huruma yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’aji ambao walimtenda vibaya.

Baba Mtakatifu amemkazia macho mtunza nyumba ambaye alipigwa na bumbuwazi kuona ujasiri wa Msamaria mwema, aliyejitaabisha kumsaidia na kumhudumia Mwisraeli, akamfunga jeraha kwa mikono yake na kumpeleka hadi kwenye nyumba ya wageni, ili aweze kuhudumiwa zaidi kwa kulipia gharama zote, huyu akawa ni shuhuda wa Neno la Mungu katika maisha yake, kwa kugundua ukarimu wa mdhambi aliyekuwa na huruma na mapendo. Alikuwa na wasi wasi moyoni lakini kwa njia ya Roho Mtakatifu akapata ujasiri wa kushiriki kutenda mema.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukarimu hauna gharama wala malipo ni ushuhuda wenye mashiko na mvuto kwa watu wanaoona na kuguswa na matendo haya, kiasi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwani Baba yao aliye mbinguni anaona kile kilichofichika sirini na katika sakafu ya moyo wa mwanadamu kama Kristo Yesu anavyosema katika Maandiko Matakatifu. Hivi ndivyo Makazi ya Mfuko wa Nazareth yanavyotekeleza matendo ya huruma kwa kutoa hifadhi kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu na wale wanaotoka katika familia maskini zaidi.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, aliwahi kusikia uwepo wa Mfuko huu, lakini Askofu mkuu Claudio Maria Celli ndiye aliyemfahamisha zaidi kuhusu historia, malengo na mchango wa kituo hiki kama kielelezo cha ushuhuda wa matendo ya huruma yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Hapa ni mahali ambapo watu wanafika si kwa ajili ya kutafuta “mshiko” bali kuwa ni sehemu ya mashuhuda wa Injili ya Kristo, ili kupandikiza katika maisha ya watu mbegu ya ushuhuda itakayozaa matunda kwa wakati wake. Hii huduma inayotekelezwa katika hali ya ukimya bila kutafuta makuu. Mwenyezi Mungu kwa wakati wake anaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuitunza mbegu hii ili hatimaye iweze kukua na kukomaa na hatimaye kuzaa matunda ya ushuhuda.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kituo hiki kitaendelea kuwa ni kielelezo cha ushuhuda kwa wote. Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwasalimisha watu wake dhidi ya mikono ya majambazi na wanyang’anyi wanaoendelea kuongezeka siku kwa siku, ili waweze kutubu na kuiacha njia yao mbaya, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu unaogusa, unaoponya na kumwokoa mdhambi, tayari kuanza kutembea katika njia ya utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anawaombea pia Makuhani wenye haraka zao, wasioguswa na shida wala mahangaiko ya watu wanaowazunguka, ili waweze kujenga utamaduni wa kusikiliza, kuona na kutenda kadiri ya uwezo wao. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo, awanusuru watu wake na Walimu wa sheria wanaotaka kufundisha imani kwa Kristo na Kanisa lake kama mahesabu magumu yanayowashinda watu kukokotoa. Awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao, tayari kuwasaidia kwa hali na mali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.