2016-06-18 06:47:00

Utume wa waamini walei na changamoto zao ndani ya Kanisa!


Baraza la Kipapa kwa ajili yaWalei katika kipindi cha miaka hamsini ya uwepo wake, limekuwa ni msaada mkubwa katika kupyaisha maisha na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa, kwa kukabiliana na changamoto pamoja na matatizo mbali mbali yaliyokuwa yanaibuka siku kwa siku. Baraza hili ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kupata ushauri wa kina kutoka kwa  Wakleri na waamini walei katika maisha na utume wao.

Mwenyeheri Paulo VI akakiri kwamba, Baraza hili ni kati ya matunda makubwa ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni Baraza ambalo limesaidia kuratibu, kufanya tafiti na kutafuta ushauri wa kina ili kuwahamasisha waamini walei kuwa na ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama vyama, mashirika na mtu binafsi. Baada ya miaka 50, Baraza hili litakuwa na mwono mpya, lakini limechangia kwa kiasi kikubwa kuwasindikiza waamini walei katika maisha yao, likasaidia mchakato wa ukomavu na mabadiliko ya waamini walei ndani ya Kanisa Katoliki mara baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Juni 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Walei, kwa kumshukuru Mungu kwa matunda mengi ambayo ameliwezesha kupata bila kusahau changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika kipindi cha miaka hamsini zilizopita. Kumekuwepo na uanzishwaji wa mashirika na vyama vya kitume ambavyo vimekuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari; na Baraza hili likavisaidia na kuviongoza taratibu hadi kufikia kutambuliwa rasmi na Kanisa.

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mchango na majitoleo ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa bila kusahau maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, chombo madhubuti cha uinjilishaji wa vijana wa kizazi kipya, dhamana ambayo waliitekeleza kwa moyo na ari kuu. Katika kipindi cha miaka 50 waamini walei wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujisadaka katika mchakato wa Uinjilishaji, unaowashirikisha katika kazi ya Ukombozi mintarafu Sakramenti ya Ubatizo.

Mkutano huu umekuwa ni fursa ya kuwakumbuka wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Baraza hili la Kipapa; hussan wale ambao wamekwisha tangulia mbele za haki, waliotekeleza dhamana na wajibu huu nyeti kwa moyo wa ukarimu na weledi ili kuwawesha waamini walei kushiriki vyema katika utume na maisha ya Kanisa.

Sasa ni wakati wa kuangalia mbele kwa matumaini zaidi, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa waamini walei. Baba Mtakatifu anasema, Baraza la Kipapa la Familia na Taasisi ya Kipapa ya maisha yataunganishwa pamoja na kuwa ni Baraza la Kipapa la Familia, Walei na Maisha, ili kuendeleza na kuimarisha wito na utume wa waamini walei. Baraza hili litaendeleza dhamana ya waamini walei, Furaha ya Injili pamoja na Furaha ya upendo ndani ya familia; Nyaraka ambazo ni nguzo msingi katika maisha na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa ili kukuza na kudumisha kazi, tunu msingi za maisha ya familia pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Kanisa linahamasishwa kuwa ni nyumba ya wote; Kanisa linatoka kifua mbele ili kuinjilisha kama Jumuiya ya Wainjilishaji bila kuwatenga watu, huku waamini walei wakipewa kipaumbele cha pekee. Wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya familia kwa kuzionjesha familia zinazoogelea katika shida na magumu huruma ya Mungu. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema iwe ni fursa ya kuwahamasisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini walei wanapata majiundo makini, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani, baada ya wao kukutana na huruma na upendo wa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.