2016-06-18 08:26:00

Uekumene katika huduma ya upendo!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa hija yake nchini Ukraine, Ijumaa jioni, tarehe 17 Juni 2016 ametembelea na kukutana na wajumbe wa Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki huko Kiev, kwenye kituo cha umoja baina ya Makanisa haya mawili na hivyo kuwasilisha salam na baraka za Baba Mtakatifu Francisko. Kituo hiki ni kielelezo cha majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili, alama ya umoja na utofauti unaojenga na kuliunda Kanisa la Kristo. Umoja wa Kanisa unapata utambulisho wake katika utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyepewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, wafiadini na mashuhuda wa imani wanaendelea kufurahia kuona kwamba uhuru ambao wa kuabudu na changamoto ya kuendelea kulijenga Kanisa, tayari kushikamana kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vita, nyanyaso na dhuluma; sanjari na kuombea amani, ili kweli amani inayotoka kwa Mwenyezi Mungu iweze kutawala akili na nyoyo za watu wa Ukraine. Lengo ni kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu, uhuru, haki, usawa na uaminifu.

Makanisa haya mawili kwa sasa yanashikamana ili kusaidia mchakato wa kuwahudumia waathirika wa vita nchini Ukraine na kwamba, Makanisa yote mawili yameonesha nia ya kweli kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, kazi inayotekelezwa kwa moyo wa huruma na upendo na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Ukraine. Upendo na huduma ni chanda na pete ni utambulisho wa maisha na ushuhuda unaotolewa na Kanisa, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mshikamano wa upendo na huduma kwa maskini na wahitaji zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.