2016-06-18 17:31:00

Majibu "feki" yalivyomchefua Yesu!


Pazia la Injili ya leo linapofunguka tunamwona Yesu anasali kama ilivyoandikwa: “Yesu alipokuwa akisali kwa faragha.”Baada ya kutoka kusali mazungumzo yake yanakuwa tofauti na fikra za wafuasi wake kutokana na majadiliano yafuatayo: Yesu akaanza kuwahoji wafuasi wake, “Je! Watu wanasema ya kuwa mimi ni nani?” au “Watu wanategemea nini kutoka kwangu?” Wanafunzi wanajibu kirahisi sana kwa sababu ni muda mfupi tu walirudi toka vijijini walikoenda kumnadi na kuhubiri Utawala wa Mungu. Wakamjibu kuwa wanakufananisha na nabii Eliya, Yohane mbatizaji na kama nabii mmojawapo wa kale.

Yesu na nabii Eliya. Nabii huyu hakuwa mtu wa kuyumba katika imani yake. Alisadiki na kumfuata Mungu mmoja tu na hivi akahubiri kutofuata miungu wengine. Kadhalika Yesu alikuwa na msimamo huohuo anaposema: “Huwezi kutumikia mabwana wawili, Mungu na pesa.”  Eliya alihusiana na Mungu kwa sala. Alipoacha kusali akatenda dhambi, lakini alipoingia katika pango la mlima Horebu kusali akatoka humo mtu mpya. Kadhalika Yesu ingawa hakuwa na dhambi, daima aliungana sana na Mungu katika sala za binafsi upwekeni.

Eliya aliingia katika historia ya watu wa taifa lake pale alipopambana na Ahabu, Jezabeel, na dini ya mungu Baal. Yesu anafanana na Eliya kwa jinsi alivyokuwa anachafuana nyongo na Waandishi na Mafarisayo. Alipambana sana na unafiki wa makuhani juu ya ibada za hekaluni. Eliya alikuwa mtu safi na mwenye haki. Hakupenda unyanyasaji wa fukara, wajane, yatima kama ilivyokuwa kwa shamba la Naboti. Yesu anafanana na Eliya jinsi alivyowapendelea fukara, wajane, yatima, watoto nk.  Eliya alikuwa mtu wa siasa kali, aliwaangamiza wapinzani wake. Katika kipengee hiki wafuasi wanamlinganisha Yesu na Eliya, pale wanapomtaka aagize moto na kuwaangamiza watu wa kijiji kilichokataa kumpokea.  

Nabii Eliya alikuwa mtangulizi wa Masiha aliyesubiriwa na Waisraeli. Ndiyo maana wakati wa chakula cha Pasaka, ilikuwa desturi kwa mama wa familia kutoka nje ya nyumba usiku na mtoto wake huku ameshika mshumaa. Akatazamatazama angani akisikiliza upepo unaovuma labda amgeweza kuona dalili za ujio wa  Eliya mtangulizi wa Masiha. Kadhalika watu walimwelewa Yesu kuwa kama mtangulizi mmojawapo wa karibu sana wa Masiha. Kwa hiyo Yesu hakuwa bado na hadhi ya Masiha bali alikuwa mtangulizi tu.

Yesu na Yohane Mbatizaji: Hata huyo alifanana sana na nabii Eliya. Malaika Gabriel anapomweleza Zakaria juu ya kuzaliwa kwake anasema: “mtoto huyu atakuwa na roho ya Eliya.” Manabii hawa wawili wanalingana katika fikra kuwa Mungu ni mwenye haki na ataangamiza wabaya wote. Kadhalika Yesu ni mwenye haki lakini anatofautiana nao katika kuwaangamiza mabaya wa Mungu. Yesu haangamizi wabaya bali anaangamiza ubaya, anaunguza ndago na magugu yaliyo rohoni mwa mtu.

Yesu anawauliza swali la pili linalowaelekea wafuasi wake kijumla na mmoja-mmoja: “Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani?” Petro anajibu “Ndiwe Kristo wa Mungu.” Lakini baada tu ya jibu la Petro tunasikia kuwa Yesu “akawaonya akawakataza wasimwambie mtu neno hilo.” Jibu la Petro lilikuwa ni hatua moja mbele ukilinganisha na majibu waliyotoa watu wengine wa kawaida waliomchukulia Yesu kuwa analingana na manabii wengine na nimtangulizi tu. Lakini anawaonya vikali na “kuwakataza wasimwambie mtu neno hilo.” Yesu alilitumia neno kukataza pale tu anapowinga mashetani yaliyomwingia mtu kwa kigiriki kukataza ni pitimao (epitimesas).  

Hapa yaoneka Petro naye amepagawa na mapepo. Shetani wa Petro ni ile picha ya masiha aliyokuwa nayo. Masiha wa Petro na wafuasi wote ni yule anayetawala, anayelipiza kisasi. Masiha namna hiyo ni shetani. Huyo ni shetani aliyemshawishi jangwani. Kumbe Masiha halisi wa Mungu ni mtumishi. Ndugu zangu kuna Wafuasi wengi wa Yesu tunaojiita Wakristu, tunashiriki liturjia ya misa, tuna majukumu katika kanisa, tunashiriki kiaminifu jumuia ndogondogo na vyama mbalimbali vya kidini, lakini pengine bado hatuifahamu bado hadhi halisi ya Yesu.

Baada ya hapo Yesu anaanza kutambulisha hadhi yake halisi: “Imempasa Mwana wa Adamu.” Jina hili “Mwana wa Adamu” linatokea karibu mara tisini hivi katika Injili kila mara Yesu anapojitambulisha. Maana yake, Yesu ni binadamu mwenye utu kweli wa mtu mwenye tabia ya utu siyo tabia ya kinyama. Binadamu wenye tabia ya mnyama hawana utu, wanayo sirika ya binafsi ni wadhulumu, waonezi, wauaji, nk. Yesu ni binadamu aliyejijulisha kama binadamu halisi mwenye utu, na anayestahili kuishi katika ulimwengu wa ufalme wa Mungu.

Kisha anasema kuwa mwana wa mtu. “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa’ Kwa vile mtu huyu ataishi kati ya mbwa mwitu itabidi ateseke sana, kwani atapambana na kugombana na watu wenye mamlaka na nguvu za kuendeleza ubabe wa kinyama wa ulimwengu huu. Kama vile wababe wa uchumi na wenye nguvu za pesa kama Wasinendrio na Mafarisayo. Wataalamu wenye nguvu za kidini na sheria kama vile Makuhani na Waandishi wanaotaka kuendeleza mfumo potovu wa udini. Yesu atapishana sana na watu hao na mwisho watamwua tu. Baada ya kuuawa, “siku ya tatu atafufuka.” Namba tatu ni kamili yaani hatima. Hapo katika ukamilifu wake wa mambo ndipo tutakapomwona nani ni mtu halisi na nani mtu feki (mnyama). Mtu wa kweli atatukuzwa yaani atafufuka. Hadhi hii ya Yesu iliwashtua Petro na wafuasi wengine waliyemsubiri masiha waliomfikiria wao. Halafu akawapa mapendekezo yake kwamba: “Mtu yeyote akitaka kunifuata.” Hilo ni pendekezo, halazimishi, wala kushawishi, wala kuhamasisha. Ni hiari yako kusuka au kunyoa. Kujikana haina maana ya kuacha utu wako, la hasha bali ni kuwa mtu zaidi, yaani kujitoa na kuishi maisha ya upendo kwa jirani.

Tena akalitamka jambo linalomtatanisha kila mtu hadi leo kuwa: Mtu anayetaka kunifuata ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.” Hakusema kuvumilia misalaba, la hasha, bali alisema kuchukua au kujitwike msalaba wako. Yesu anatoa mwito huu wa kubeba msalaba karibu mara tano katika Agano jipya, lakini inasikika na kueleweka vibaya. Watu wanasema: “Kila mtu atauchukua msalaba wake mwenyewe”. Wengine wananung’unikia “Mungu amenipa msalaba mzito.” Kumbe Mungu hamgawii mtu yeyote yule msalaba, mateso, machungu, kuachwa, maonezi, manyanyaso, upweke, kufukuzwa kazi. Matatizo hayo ni changamoto na sehemu ya maisha ya binadamu.

Kumbe, Msalaba anaoumaanisha Yesu utauelewa katika maelezo yafuatayo. Wakati wa Yesu hata kabla yake wale magangwe waliojidai kuhoji na kukosoa sheria na katiba ya nchi au kukosoa misahafu na sheria za dini walibebeshwa msalaba na kwenda kunyongwa hadharani. Kwa hiyo Msalaba anaomaanisha Yesu ni kuishi maisha ya Injili yake yanayopingana na maisha mabovu ya ulimwengu huu. Hapo mkristu utateseka,  utatoka jasho la kujaribu kuwa mkristu, fatiki ya kuwa mwaminifu na kuunganisha maisha yako na ya Yesu wa Ekaristi tofauti na hali halisi ya ulimwengu. Msalaba huo unakuwa hata kwa yule aliyetengwa na wengine kutokana na kuwa kinyume na ulimwengu. Kwa hiyo yabidi kujikwinda hasa katika kuunda ulimwengu mpya wa haki, wa kutumikia, wa amani, wa upendo na wakusaidia aliopendekeza Yesu yaani kujikana, kinyume na ulimwengu wa ubinafsi, wa kutawala, wa kujilundikia mali na utajiri.

Yesu anahitimisha: “Atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu atakayasalimisha.” Kwa upande wa Yesu, kujitoa na kutoa siyo kupoteza bali kujihalalisha mwenyewe. Kitu pekee kitakachombakia mtu katika maisha ni upendo ulioutoa. Hayo ndiyo mapendekezo ya Yesu kwa wafuasi wake wote.

Na Padre Alcuin Nyirenda OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.