2016-06-18 17:02:00

Majandokasisi wapewe majiundo makini!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Ukraine, Jumamosi jioni, tarehe 18 Juni 2016 amekutana na umati mkubwa wa Majandokasisi wanaojiandaa kwa sala, mang’amuzi ya maisha; malezi makini ya kiakili na kichungaji, tayari kuwekewa mikono kama Mapadre, ili hatimaye kuonesha ukarimu na uwajibikaji.

Umati huu mkubwa wa Majando kasisi ni mwaliko wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu sanjari na kuendelea kujimega bila kujibakiza kwa ajili ya majiundo makini yanayiojikita katika ubora wa mafundisho tanzu ya Kanisa na utamadunisho wa tunu msingi za maisha ya kiroho kutoka kwenye Makanisa ya Mashariki. Majiundo makini ni huduma muhimu sana kwa Wakleri watakaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya za Kikristo nchini Ukraine.

Kutokana na ukweli huu, Kardinali Parolin, amezishukuru taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyosaidia katika mchakato wa majiundo ya awali na endelevu kwa ajili ya viongozi wa Kanisa. Malezi yapewe kipaumbele cha pekee pamoja na kuwa makini katika kuwachagua na kuwateuwa waombaji katika Daraja Takatifu ili waweze kuwa ni Wakleri watakaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya walezi na walelewa, ili kuweza kuwa na ukomavu wa maisha unaojikita kwa Kristo mwamba wa maisha yao.

Majandokasisi wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa Kanisa nchini Ukraine, Kanisa ambalo limejikita katika ushuhuda, tayari kusimama kidete katika mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, kwa kutambua kwamba, wao ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Vijana wawe tayari kuitikia mimi hapa, mwito ambao unapaswa kupyaishwa kila siku ya maisha, tayari kuwasikiliza na kuwahudumia watu wa Mungu, kielelezo cha wahudumu wa mafao na ustawi wa wengi na kamwe si kama mbwa mwitu! Wasikubali kamwe kumezwa na malimwengu hali ambayo imesababisha vita, kinzani na machafuko nchini Ukraine. 

Wawe kweli ni mashuhuda na wahudumu wa Injili ya Kristo ndani na nje ya Ukraine kwa kuendeleza mchakato wa utamadunisho, ili imani iweze kuota mizizi katika akili na nyoyo za watu, huku wakidumisha: huruma, upendo, ukarimu na umoja wa Kanisa. Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin, ametoa salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.