2016-06-18 07:40:00

Iweni na huruma!


Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, Ijumaa tarehe 17 Juni 2016 limezindua kampeni ya kukusanya fedha kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na kugharimia miradi mbali mbali inayohudumiwa na Shirika hili la kipapa sehemu mbali mbali za dunia. Kampeni ya ukusanyaji wa fedha ni kuanzia tarehe 17 Juni hadi tarehe 4 Oktoba 2016 na unaongozwa na kauli mbiu “ Iweni wenye huruma ya Mungu”.

Kampeni hii imezinduliwa kwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video iliyooneshwa kwenye Ukumbi wa mikutano wa Radio Vatican na kuhudhuriwa na Kardinali Mauro Piacenza, Rais wa Kimataifa wa Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji, Bwana Philipp Ozores, Katibu mkuu, Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican pamoja na Padre Imad Gargees kutoka Iran.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuazisha na kutekeleza tendo la huruma, kwa kutambua kwamba, binadamu wote wanahitaji huruma ya Mungu katika maisha yao. Hata binadamu pia anapaswa kuonesha matendo ya huruma na mapendo kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa vita sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema, mbele yake kuna makabrasha ya miradi mbali mbali ambayo inatekelezwa na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Kanisa hitaji sehemu mbali mbali za dunia, ili kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa mataifa. Baba Mtakatifu anapenda kulikabidhi Shirika hili dhamana ya kusambaza huruma na upendo wa Mungu kwa wahitaji sehemu mbali mbali za dunia, ili kuendeleza ari na moyo wa huruma na mapendo ulioanzishwa na Padre Werenfried Van Straaten, aliyeonesha ukaribu kwa kujikita katika wema, upendo na huruma.

Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali katika umwilishaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu pamoja na kushirikiana na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji. Matendo haya yame ni ya kudumu, ili kujibu kili ona mahitaji ya misaada kwa watu mbali mbali na kamwe watu wasiogope huruma ya Mungu kwani hiki ni kielelezo cha upendo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.