2016-06-18 16:38:00

Haki msingi za wanawake na maendeleo endelevu!


Mkutano wa thelathini na mbili wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa uliofanyika hivi karibuni, uliongozwa na kauli mbiu “Haki msingi za wanawake na Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa Mwaka 2030: hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma”. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba haki msingi za wanawake zinalindwa na kuendelezwa kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu; mambo yanayojenga umoja katika familia ya binadamu. Inasikitisha kuona kwamba, hata leo hii, kuna wanawake wengi ambao haki zao msingi haziheshimiwi wala kuthaminiwa.

Huu ni mchango ambao umetolewa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa mataifa zenye makao yake makuu mjini Geneva. Ili kufikia azma hii, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutokomeza ubaguzi na ukosefu wa usawa miongoni mwa wanawake na wasichana, ilikujenga mazingira ya haki na amani kwa sasa na kwa siku za usoni. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia na kuwajengea wanawake uwezo pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya dhuluma na nyanyaso kwa wanawake, mambo ambayo yamekemewa vikali na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia, ili kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Ushirikiano na mshikamano ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani Kanisa lina miundo mbinu mingi ambayo inaweza kutumika kuwajengea wanawake na wasichana uwezo, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu hususan katika nchi changa zaidi duniani. Kumbe, utu na heshima ya binadamu ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Kanisa linatambua na kuheshimu mchango wa wanawake hivyo wanapaswa kujengewa uwezo ili washiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto mamboleo dhidi ya umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi. Wanawake washiriki kikamilifu katika uongozi, masuala ya elimu na siasa na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya jirani zao, ili kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti katika jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.