2016-06-18 08:00:00

Epukeni uchu wa mali na madaraka!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa ziara yake ya kikazi, nchini Ukraine Ijumaa tarehe 17 Juni 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Alexandri huko Kiev na kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wanaokumbana na mahangaiko mengi kwa wakati huu.

Anasema, Injili inawachangamotisha waamini kutojilimbikizia mali hapa duniani, jambo ambalo si rahisi sana kutekelezwa kutokana na watu kuwa na uchu wa mali na madaraka, kiasi hata cha kubeza: ukweli, uwazi na uaminifu kwa dhamana ambazo viongozi wa umma wamekabidhiwa kuzitenda. Duniani kuna mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; ukosefu wa haki na amani na kwamba, kuna watu wachache ndani ya jamii wanajilimbikizia mali kwa kutumia migongo ya maskini, ambao wanaendelea kuogelea katika dimbwi la magonjwa, ukosefu wa uhuru sanjari na kujikatia tamaa kwa ajili ya kujipatia maisha bora zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni, haki msingi kwa kila binadamu!

Kardinali Parolin anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea haki pamoja na kuachana na mambo ambayo yanawafanya kukosa uhuru wa kweli kutokana na kukita maisha yao katika mali na malimwengu. Wataweza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki na amani, ikiwa ndani mwao hakuna wivu, uchoyo, uchu wa mali na madaraka. Waamini wawe na ujasiri wa kuondokana na maovu yanayowanyima uhuru wa kweli kwa kujikita katika unafiki.

Macho na mawazo yao, yawe ni kielelezo cha ukweli pasi na unafiki, changamoto kubwa kwa viongozi wa Kanisa, ili kuondokana na kashfa zinazoweza kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Wasikubali kamwe kumezwa na malimwengu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.  Fedha haramu inafisha utu na heshima ya binadamu na badala yake, waamini wawe na ujasiri wa kujiwekea utajiri mbinguni na kubeba vyema Misalaba na changamoto za maisha yao.

Kardinali Parolin, katika Ibada hii ya Misa Takatifu amemkumbuka na kumwombea Askofu mkuu Petro wa Jimbo kuu la Kiev, aliyefariki ghafla hivi karibuni. Waendelee kumwombea ili aweze kuifikia hazina aliyokuwa amejiwekea mbinguni kwa njia ya maisha na utume wake. Liwe ni fundisho kwa wote kwamba, hapa duniani mwanadamu ni mpita njia na wala hana makazi ya kudumu. Hazina ya kweli ya mwanadamu ni Mwenyezi Mungu anayewajalia amani na utulivu wa ndani. Ekaristi Takatifu wanayoadhimisha inakuwa ni chakula cha mbinguni, amana ya maisha ya milele, ambayo ni Kristo Yesu mwenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.