2016-06-16 15:20:00

Vita inasababisha mahangaiko makubwa kwa watu!


Vita imeendelea kuwa ni sababu kubwa ya watu kupoteza maisha na mali zao; mahangaiko ya watoto na watu wasiokuwa na hatia; vita inaendelea kusababisha ulemavu pamoja na kudumaza maendeleo, utamaduni, historia na madhara yake kusikika ndani na hata nje ya Ukraine. Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 16 Juni 2016 alipokutana na kuzungumza na Kamati ya viongozi wa kidini mjini Zaporizhia, huko Ukraine wakati wa  ziara yake ya mshikamano kwa wananchi wa Ukraine kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwa Kanisa zima.

Mahangaiko ya wananchi wa Ukraine ni changamoto inayosuta dhamiri za Jumuiya ya Kimataifa. Vatican inapenda kusimama kidete ili kusisitizia umuhimu wa kuheshimu Sheria za Kimataifa katika eneo na mipaka ya Ukraine, ili kujenga na kudumisha amani na utulivu kitaifa na kikanda. Sheria hizi hazina budi kujikita katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu. Kumbe, waamini wanadhamana ya kuendelea kusali ili kuombea amani pamoja na kuwasaidia waathirika kupata mahitaji yao msingi kadiri ya mashauri ya Kiinjili.

Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, aliwaalika waamini wa Kanisa Katoliki kutoka Barani Ulaya kumuunga mkono kwa kuchangia huduma za kiutu kwa ajili ya wananchi wa Ukraine, kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu. Jumuiya ya Ulaya inawajibika kuisaidia Ukraine ili kukabiliana na changamoto zake na wala si tu katika masuala ya kiuchumi na kimikakati.

Kardinali Parolin, amewasilisha mchango huu na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kuchangia pia kama kielelezo cha mshikamano. Mchango wa Baba Mtakatifu utaratibiwa na Kamati ya ufundi itakayosimamiwa na Askofu msaidizi Jan Sobilo wa Jimbo la Kiyiv Zaporizhia na Vatican kwa upande wake, itasimamia matumizi na utekelezaji wa miradi itakayokuwa imebainishwa. Msaada huu ni kwa ajili ya wakimbiz, wahamiaji; wazee na watoto pamoja na waathirika wengine waliolazimika kuyakimbia makazi yao, ili kusalimisha maisha yao bila kuwasahau wasiokuwa na makazi maalum na majeruhi. Msaada huu utatolewa kwa wote pasi na ubaguzi.

Kamati za majadiliano ya kidini zitahusika moja kwa moja ili kuwatambua wahitaji zaidi na ushauri wao utazingatiwa na kwamba, miundo mbinu ya msaada ambayo ipo itaendelea kutumiwa, kwa kuhakikisha kwamba, ukweli, uwazi na uadilifu vinazingatiwa na kwamba, msaada huu si chambo cha wongofu wa lazima, bali ni mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa wote kuweza kushiriki ukarimu na upendo wa Kanisa kwa waja wake kwa njia ya mshikamano wa huruma na upendo. Hii ni changamoto pia kwa wahusika mbali mbali kuondoa vikwazo vinavyogumisha utoaji na usambazaji wa misaada kwa waathirika kwa kuondokana pia na vitendo vya ubaguzi, ili kukazia sheria za kimataifa. Kardinali Pietro Parolin, amewashukuru wajumbe wote wa Kamati ya mchango wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya wananchi wa Ukraine kwa sadaka na majitoleo yao, ili kuwasaidia maskini na wote wanaoteseka kwa kujikita katika mshikamano wa upendo unaohitajika sana nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.